Chirac anaugua ugonjwa wa kusahau


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Jacques Chirac

RAIS wa zamani wa Ufaransa, Jacques René Chirac amepona kusimama kizimbani kutokana na kile kilichoelezwa mahakamani kwamba anaumwa ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Ripoti ya daktari iliyowasilishwa juzi mahakamani na wanasheria wake imeonsha kuwa rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 78 asingeweza kufika kortini kujibu tuhuma za ufisadi zinazomkabili kutokana na tatizo hilo.

Akitoa uamuzi juu ya suala hilo, Jaji Dominique Pauthe anayesikiliza kesi hiyo alisema Chirac hatalazimika tena kuwepo mahakamani wakati wa kesi hiyo inayosubiriwa kwa shauku kubwa na watu.

Jaji Pauthe alisema juzi Jumatatu kwamba ametoa uamuzi huo kwa kuzingatia utetezi wa jopo la wanasheria wa Chirac na kwamba kesi hiyo itakuwa ikiendelea kortini bila uwepo wa rais huyo wa zamani.

Kesi hiyo itakuwa ya kwanza kumkabili rais wa zamani wa Ufaransa tangu Vita Kuu vya II vya dunia ambayo itakuwa ikisikilizwa hadi 23 Septemba 2011. Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Machi mwaka huu ilisitishwa kwa muda kusubiri uamuzi wa rufaa ambayo mmoja wa watetezi alipeleka mahakama ya rufaa.

Baada ya kusikiliza utetezi huo, hasa ikizingatiwa kuwa tayari mahakama ilishaarifiwa kwa barua tangu Ijumaa iliyopita, Jaji Pauthe alisaliwa na uchaguzi mmoja kati ya tatu: kusitisha kwa muda mwenendo wa kesi hadi apate ushauri wa kina kutoka kwa wataalam au kuendelea na kesi hiyo bila uwepo wa Chirac au kutupa kesi.

Jaji Pauthe hakupata tabu kuamua kuendelea na kesi hiyo bila uwepo wa Chirac kortin kwani wanasheria wa rais huyo wa zamani waliwasilisha maoni ya mteja wao yakisema "itakuwa muhimu kwa demokrasia yetu" na kuonesha kuwa "watu wote ni sawa mbele ya sheria."

Maelezo ambayo Jaji Pauthe alisoma yalikuwa pamoja na viambatanisho vya ripoti ya tiba katika kurasa nne ikiwemo picha ya uchunguzi wa kichwa aliyopigwa Aprili.

Mwanasheria wa Chirac, Jean Veil aliiambia mahakama kwamba mteja wake anasumbuliwa na “tatizo kali la kukosa kumbukumbu" linalohusishwa na hali ambayo “haiwezi kurejewa”. Alisema tatizo la Chirac si kuumwa bali ni “dalili” inawezekana inayohusishwa na kiharusi alichopata mwaka 2005 au “vyanzo vingine”.

Jopo la wanasheria wa Chirac liliwasilisha barua mahakamani hapo Ijumaa iliyopita kusisitiza kwamba Chirac “hakuwa na uwezo wa kuhudhuria kikamilifu kufuatilia mwenendo wa kesi” hivyo wakaomba asiwepo.

Hata hivyo, mwanasheria kutoka kikosi cha kupambana na rushwa (Anticor), Jerome Karsenti amependekeza ufanyike uchunguzi huru ili kuthibitisha kama kweli Chirac anakabiliwa na tatizo hilo au ni “ucheleweshaji chungu nzima” katika jaribio la kukwepa mkono wa sheria.

Katika kesi hiyo Chirac anakabiliwa na mashtaka mawili ya ufisadi aliofanya City Hall kwa kuunda nafasi kadhaa bandia za ajira kwa lengo la kupata fedha za kugharimia chama chake cha conservative alipokuwa meya wa Jiji la Paris kuanzia mwaka 1977 hadi 1995.

Katika kipindi chote cha miaka 12 alipokuwa Rais wa Ufaransa hakubughudhiwa kwa vile alikuwa na kinga ya kutoshtakiwa.

Pamoja na Chirac katika kesi hiyo wapo wafanyakazi wawili wa zamani wa City Hall na saba wengine ambao wamekiri kunufaika na malipo hayo ya kifisadi. Vilevile wapo kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi Marc Blondel  na mjukuu wa Jenerali Charles De Gaulle, Jean ilihali Waziri wa Mambo ya Nje Alain Juppé ametajwa kama shahidi
Ikiwa atapatikana na hatia, Chirac atatupwa jela miaka 10 na kulipa faini ya dola za Kimarekani 215,000 (Sh. 344,000,000).

Kesi nyingine iliyowahi kumkabili Chirac alipokuwa meya ni pamoja na madai kwamba alikula chakula cha thamani ya euro 2.1 milioni kwa gharama za Jiji kati ya 1987 na 1995. Kesi hizo zilitupwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Chirac aliyezaliwa 29 Novemba 1932 ni mwanasiasa mashuhuri. Amekuwa Rais wa Ufaransa kuanzia 1995hadi 2007. Amekuwa waziri mkuu wa Ufaransa kuanzia 1974 hadi 1976 na kuanzia 1986 hadi 1988 hivyo kuwa mwanasiasa pekee aliyeshika nafasi ya waziri mkuu mara mbili. Amekuwa meya wa Paris kuanzia 1977 hadi 1995.

Mbali ya kesi ya Chiraq, kati ya Septemba na Desemba mahakama za Ufaransa zinatarajiwa kushughulikia kesi zinazohusu majina makubwa.

Baadhi ya watu mashuhuri wanaokabiliwa na kesi ni Waziri mkuu wa zamani, Dominique de Villepin; meya aliyerithi mikoba ya Chirac, Jean na mkewe Xavière Tibéri ambao hawapatani na Rais Nicolas Sarkozy;  nyota wa mitindo, John Galliano; na gaidi maarufu wa miaka kati ya 1970 na 1980, Ilich Ramírez Sánchez maarufu kama Carlos the Jackal.

0
No votes yet