Chuji, Boban fikirieni mara mbili

MIONGONI mwa habari zilizonishtua wiki iliyopita ni kitendo cha nyota wa soka Tanzania, Haruna Moshi ‘Boban’ wa Simba, Kigi Makasi na Athumani Idd ‘Chuji’ wa Yanga kuitema ofa ya kwenda kuchezea klabu ya Ligi Kuu ya Vietnam.
Nyota hao ilikuwa waungane na Uhuru Suleiman anayechezea Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hassan Salum ‘Banda’ wa Malindi ya Zanzibar na kiungo wa kimataifa wa Uganda, Hassan Keto wa KCC ya Uganda kwenda kujaribiwa katika timu ya Danan ya mjini Ho chi Minh (zamani Saigon).
Wakala wa kimataifa anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataia la Soka (FIFA), Ibrahim Lwembo, aliwahitaji nyota hao baada ya kufanya mipango ya kutosha kabla ya kumtumia mdau mkubwa wa soka Zanzibar, Ally Saleh, kuratibu safari yao. Walikataa, wakaachia waondoke Uhuru, Banda na Keto.
Nilistaajabu kuona nyota hao wamekataa safari hiyo kwa taarifa kwamba wana watu wao wa karibu watakaowapeleka Ulaya kufanya majaribio. Boban amethibitisha hilo alipozungumza na gazeti moja la michezo Jumapili iliyopita.
“Hawakuniambia sababu, lakini nadhani wachezaji wa Tanzania wanadhani kuwa wanaweza kucheza Serie A (Italia), Bundeliga (Ujerumani) au Ligi Kuu England kirahisi.
“Mimi nasema mchezaji wa kucheza ligi za Ulaya hapa Tanzania hajazaliwa. Huku Bara la Asia ndiko wangeanza au kama nchi za Norway, lakini si nchi zenye ligi za ushindani na ubaguzi,” anasema Ally Saleh alipozungumza na MSETO Jumatano iliyopita.
Hakika nukuu za mratibu huyo ambaye pia ni mwanahabari anayefanyia kazi Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), zilinigusa ndipo nikaingia kujadili.
Kwanza nikiri kwamba Vietnam iko nyuma kisoka katika viwango vya FIFA, lakini rekodi za timu waliyoitosa zinaipa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa barani Asia, kitu ninachodhani ilikuwepo nafasi kwao kutafuta mlango wa kuingilia Ulaya.
Taarifa zinasema kwamba timu hiyo inaongoza katika ligi ikiwa mzunguko wa pili, hivyo ilikuwa nafasi pekee kwa nyota hao kwenda kumalizia mkia kwa kutaraji mambo kunyooka baadaye kwa kucheza na timu za Japan, Korea Kusini, China na kadhalika. Lakini wanataka kuanza kuhesabu 10 badala ya moja.
Ukweli umedhihirishwa na Mrisho Ngassa wa Yanga. Pamoja na uwezo wake wa kusakata kandanda nchini katika kiwango kizuri kwa Afrika, ameshindwa kuchukuliwa na West Ham United ya England alikokwenda kufanya majaribio kwa wiki mbili.
Mwenyewe amethibitisha kupewa nafasi katika vikosi vyote viwili kwa maana ya kikosi cha kwanza cha West Ham, kadhalika wachezaji wa akiba.
Lakini ameshindwa kumshawishi Gianfranco Zola, kocha wa timu hiyo na jopo lake la ufundi. Amesema sababu zilizomfanya arejee nyumbani Tanzania ni stamina ndogo na umbile lake dogo.
La umbile itabaki kuwa sababu za imani kwamba Mungu amejalia umbo hilo lakini la stamina (nguvu), ameambiwa ajenge mwili kwa kula vyakula vitakavyompa nguvu na mazoezi yatakayomfanya asimame imara.
Mawazo ya akina Chuji si mabaya kama wana malengo ya dhati, lakini wajiulize viwango vyao vinafaa timu za Ulaya?
Ni vema wachezaji hao wakatambua kuwa ubora wa soka walionao hapa nchini si kigezo kuwa wanaweza kuingia katika ligi zenye ushindani na soka la kujituma kama za Ulaya.
Kina Chuji wanaweza kuwa bora hapa nchini lakini kwengineko mambo huwa ni magumu kwani Ngassa si wa kwanza kwenda na kurudi ameangukia pua.
Tumewahi kushuhudia akina Athumani China, Mohammed Mwameja waliokwenda England kabla ya winga machachari wa Yanga, Edibily Lunyamila, aliyejitosa Ujerumani. Wote hawa walirudi patupu.
Kwa mtazamo wao ni kwamba vijana wetu wanapotoshwa badala ya kutulia na kuangalia vigezo mbalimbali ambavyo vingewawezesha kucheza soka Ulaya.
Hakuna ubishi kuwa soka la Ulaya ambalo lina ushindani mkubwa, linahitaji wachezaji wenye vipaji, akili, jitihada na mbinu nyingi za kiufundi mchezoni, bila ya kusahau nidhamu nzuri.
Ulaya si mahali pa kuwafaa wachezaji wanaopenda soka la 'kuuza sura' huku wakiinuliwa na vyombo vya habari kwa kutegemea ushabiki wa kitimu.
Ubora wa kiwango cha wachezaji wa Tanzania hauendani na sifa wanazopewa na baadhi ya wanahabari.
Pamoja na kuwa na wachezaji wazuri wanaoweza kuleta ushindani katika soka la kimataifa kwa Afrika, ukweli unabaki pale pale kwamba mpaka sasa hatuna wachezaji wenye vigezo thabiti vya kuwawezesha kufaa kwa ligi za barani Ulaya.
Si kwamba Tanzania haiwezi kuzaa wachezaji wazuri na kuwaingiza katika ligi hizo. Wanaweza kuwepo lakini hiyo itategemea namna watakavyojiendeleza kwa kupitia mlango wa ligi nyingine kama vile za Asia.
Naam, baadhi ya wachezaji Tanzania wamekuwa wakiwania kwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa lakini, wameshindwa.
Nguvu, umbo, kasi na uwezo binafsi ni miongoni mwa vitu muhimu kwa yule anayetaka kushinda akili za makocha wa timu za Ulaya. Ngassa ambaye amerejea nchini baada ya kushindwa kupenya West Ham United, anatupa mfano hai wa ukweli huu.
Jinamizi la ufinyu wa upeo wa kusoma soka la Ulaya kwa wachezaji wetu, bado lingalipo kwani baadhi yao wanajiona wa juu kutokana tu na kuwepo timu ya taifa (Taifa Stars).
Lazima watambue kuwa kuchezea Taifa Stars ama timu kubwa hapa nchini kama Simba na Yanga si kigezo tosha kwao kukubalika Ulaya.
Kwa kiasi kikubwa soka la Tanzania huendeshwa katika mfumo wa kutawaliwa na wadau au watu wanaojiita “watu wa mpira” ambao wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu taswira ya soka halisi.