CUF yajiandaa kuvuruga upinzani bungeni?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Gumzo la Wiki
Hamad Rashid Mohammed

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaonekana kupumbazwa na “ndoa ya mkeka” kiliyofunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM)?

Hivi sasa kimeacha kusimamia misingi yake ya asili, badala yake, kimejivisha joho la uwakala wa kuvuruga upinzani bungeni. Mara hii katika bunge la Jamhuri.

Iko wapi ile CUF iliyokuwa ikijitambulisha mbele ya wananchi kuwa ni chama cha kutetea haki za wanyonge “kwa gharama yeyote,” ikibidi hata “jino kwa jino” na “ngangari kinoma?”

Wako wapi wanachama na mashabiki wa chama hiki, waliokuwa mstari wa mbele kutetea chama chao dhidi ya dhuluma, uonevu na manyanyaso, kutoka kwa viongozi wa CCM na wale waliowaita “vibaraka wao?”

Kwa zaidi miaka 18, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CUF kimejitambulisha mbele ya jamii na jumuiya ya kimataifa kuwa ni “chama imara” cha upinzani, Bara na Visiwani.

Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba aliwahi kusema, bila kutafuna maneno, kuwa chama chake kitaendelea kupigania “haki sawa kwa wote, katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.”

Hakuishia hapo: Alimtuhumu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame kuwa “goigoi” na ambaye alisema atastaafu akiwa hana la kukumbukiwa.

Lakini hata kabla ya katiba mpya kupatikana; tume huru kuundwa na haki sawa kwa wote kupatikana – katikati ya “haki sawa kwa wachache” – CUF tayari kimebadili mwelekeo wake.

Sasa kinatuhumiwa kudhoofisha upinzani – hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndani na nje ya bunge.

Kauli za viongozi wake wakuu, Maalim Seif Shariff Hamad na Hamad Rashid Mohammed, zinaonekana machoni mwa wengi kuwa zimelenga kutetea “ndoa” yao na CCM na siyo mabadiliko kwa manufaa ya umma wa Tanzania.

Ndoa ya CUF na CCM ilifungiwa Zanzibar ambako Maalim Seif na Rais Amani Abeid Karume walifikia “makubaliano” ambayo yameweka vyama hivyo viwili katika kapu moja la utawala wa “mashaka” – Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hadi leo, kilichojadiliwa hadi kulegeza na hatimaye kuua mishipa ya fahamu ya CUF; na kufikia mwafaka, hakijawekwa wazi kwa wanachama, wananchi na dunia kwa jumla.

Wachunguzi wa siasa za Tanzania wanasema mwafaka unaweza kuwa umeelekezwa na moja ya mambo mawili: mchoko wa viongozi wa CUF au tamaa ya kuwa serikalini kwa gharama yoyote ile, hata kuacha misimamo yao ya awali.

Bali sasa CUF imeanza kukunjua makucha ambayo haikuwa nayo hapo awali. Inayaelekeza kwa chama kikuu cha upinzani kilichochukua nafasi yake bungeni.

Kwanza, chama cha CUF kinalaani hatua ya wabunge wa CHADEMA kutoka bungeni wakati Rais Jakaya Kikwete anazindua bunge la 10, tarehe 18 Novemba 2010.

Kinasema hatua hiyo, ni fedheha kwa CHADEMA, viongozi wake, wanachama na mashabiki. Tangu lini CUF imekuwa na maoni ya aina hii? Tumezoea kauli hizi kutoka vinywani mwa viongozi wa CCM.

Historia inaumbua. Ni viongozi hawahawa wa CUF walioshinikiza chama chao kutotambua matokeo ya urais mwaka 1995; na hata rais mwenyewe Zanzibar. Hizi zilikuwa enzi za utawala wa Dk. Salmin Amour.

Kipindi hicho, CUF iliagiza wawakilishi wake katika Baraza, kususia vikao. Nao viongozi wakuu wa CUF waliamua kususia sherehe zote za serikali, hasa sherehe za Mapinduzi, 12 Januari 1964.

Katika chaguzi mbili zilizopita – ule wa mwaka 2000 na 2005, CUF iliendelea kutotambua matokeo ya uchaguzi na rais aliyetangazwa mshindi.

Zaidi ya hayo, CUF kilihamasisha wanachama wake kuandamana. Ni katika maandamano hayo, makumi ya raia walifariki dunia baada ya polisi kutumia silaha za moto kuzima maandamano hayo.

Kwa mara ya kwanza, matukio haya yaliingiza taifa katika historia nyingine. Baadhi ya raia walikimbilia nchini Kenya na hivyo Tanzania kupoteza sifa yake ya asili ya kuwa taifa linalopokea wakimbizi na kuwa taifa linalozalisha wakimbizi.

Katika mazingira haya, nani – kati ya Maalim Seif na Hamad Rashid –
anapata dhamira ya kweli ya kusema CHADEMA wamekosea kwa hatua yao ya kutoa kilio chao kwa taifa na dunia nzima, tena kwa njia ya ustaarabu?

Inawezekana kabisa kuwa kwa matamshi haya ya viongozi wa juu wa CUF, ni kweli kwamba chama hiki kimekuwa kikishinda uchaguzi kila mara.

Lakini wenzao wa CCM wanawafahamu kwamba hawana msimamo wa pamoja katika kutetea maslahi ya nchi. Ndiyo maana wameamua kuwapora ushindi wao kama wanavyodai wenyewe kila uchaguzi mkuu unapomalizika.

Pili, kwa CUF kupinga njia yoyote ile ya amani ya kudai katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na kuondolewa kwa sheria kandamizi, chama hicho kinadhihirisha kuwa kimeridhika na hali ya sasa ya utawala wa CCM.

Aliyaona mapema Fatma Maghimbi, mbunge wa CUF, aliyekuwa kiongozi wa upinzani bungeni, aliyeamua kuhamia CCM mara baada ya viongozi wakuu kufikia muwafaka.

Haya yanafanyika wakati Profesa Lipumba mwenyewe hajajua jinsi gani kura zake katika uchaguzi wa mwaka 2005 “zilivyohama” na hadi kupachikwa jina la kura za “kichinachina.”

Kila aliye makini anajua kuwa madai ya CHADEMA ni madai ya Watanzania na wapenda mabadiliko duniani kote. Hatua waliyochukua ni ile iliyomo katika uwezo wao lakini kuelelezea utashi, hisia na haki zao na jamii yao.

Hakuna shaka kwamba uchaguzi ulivurugwa. Wizi wa kura uligundulika. Matokeo ya baadhi ya majimbo yanafanana kwa kila kitu na majimbo mengine.

Mfano hai ni hatua ya NEC kubadilisha kura za mgombea ubunge wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema katika jimbo la Vunjo, wiki mbili baada ya kutangaza matokeo. NEC ilisema kulikuwa na kasoro katika ujumlishaji wa kura. Ikarejesha karibu kura 6,000 kwa Mrema.

Tatu, CUF wamegoma kuungana na CHADEMA kuunda kambi moja na yenye nguvu ya upinzani bungeni.

Hapa CUF wanasingizia kuwa CHADEMA wamekataa kuingiza chama cha NCCR- Mageuzi, na kwamba wao hawawezi “kuchaguliwa marafiki.”

Hivyo ndivyo Hamad Rashid, mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba na kiongozi wa zamani wa upinzani bungeni, anavyonukuliwa akisema.

Hamad anasema, makubaliano yaliyofikiwa na vyama vyote vya upinzani, kabla ya kufungwa kwa mkutano wa tisa wa bunge, ni kuundwa kwa kambi moja itakayoshirikisha vyama vyote. Hili lina utata.

Hoja ya Hamad inavunjika kwa urahisi. Upinzani bungeni ni “ngome” moja. Hili halina ubishi. Lakini siku zote kuna chama kiongozi cha upinzani huo.

Hata kama vyama vingine havikuingia kwenye uongozi wa juu wa “kambi rasmi ya upinzani” – yaani wale wanaosubiri kuingia kwenye utawala – bado wako chini ya mwavuli wa kiongozi wa upinzani.

Lakini vyama vya upinzani haviwezi kufikia makubaliano ya aina anayosema Hamad wakati vyama vyote vilitoka bungeni na kuingia katika uchaguzi kwa shabaha moja kuu: Kushinda uchaguzi na kutwaa madaraka ya nchi kila kimoja lwake.

Kwa msingi huo – wa kila chama kuingia katika uchaguzi kwa lengo binafsi la kushinda na kutwaa madaraka – nani ambaye angeweza kuingiza chama kilichopo ikulu katika makubaliano ya kuunda upinzani? Hamad ana mizaha.

Je, Hamad anataka kusema kwamba kwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya aina hiyo, CHADEMA wangeshinda uchaguzi wangewashinikiza kutekeleza makubaliano ya kuunda upinzani bungeni? Je, ingekuwaje kama CUF ingeshinda uchaguzi?

Au kwa mfano, CCM kingeshindwa uchaguzi, wangewalazimisha kuunda kambi kwa makubaliano waliyoingia wao – CUF na CHADEMA?

Ukweli ni huu. Kambi rasmi ya upinzani inakufa mara baada ya bunge kuvunjwa na mikataba yote iliyofungwa ya maandishi na kauli – kama kweli ilikuwepo – inakufa na bunge lililovunjwa.

Ni hivyo kwa sababu, kambi rasmi ya upinzani bungeni, si taasisi ya kudumu. Inabadilika kutokana na matokeo ya uchaguzi kwa kumtoa mpinzani kuwa mtawala na mtawala kuwa mpinzani; au mpinzani mmoja kubaki nje na mwingine kuongoza kambi.

Nne, kwa mazingira ya sasa, wenye uwezo wa kuingiza chama katika uongozi rasmi ni CHADEMA; siyo CUF. Hamad anajua kuwa kambi ya upinzani bungeni sasa, iko chini ya CHADEMA. Hawa ndio wenye uwezo wa kumuingiza wamtakaye na kumuondoa wasiyemtaka.

Hamad anajua vema kwamba mwaka 1995, chama chake kiliungana na UDP kuunda upinzani bungeni. Wakati huo, UDP ilikuwa na wabunge wanne ambao wengi hawakuwa mabingwa katika mijadala ya ndani na nje ya bunge.

Viongozi wakuu wa CUF waligoma kuungana na NCCR iliyokuwa na wanasiasa waliobobea na wasomi wa aina mbalimbali.

Wala CUF haikuona haja ya kuungana na CHADEMA ambayo wabunge wake walikuwa ni pamoja na Dk. Willibrod Slaa.

Hata mwaka 2005, CUF walianza kuunda kambi ya upinzani pekee yao. Walilazimika kuingiza vyama vingine baada ya kubanwa na kanuni za bunge kwamba sharti wawe na asilimia 12.5 ya wabunge wote.

Je, madai ya sasa ya CUF yanatoka wapi? Inapata wapi mabavu ya kulazimisha CHADEMA kuingiza NCCR katika chama kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani? Je, CUF inadhani wananchi hawakumbuki kile ambacho ilikuwa ikifanya?

Tano, hata hicho ambacho Hamad anajaribu kukitengeneza – urafiki kati ya NCCR na CUF – kimejaa utata. Ni ghiliba, hata kama katika siasa kuna usemi kuwa hakuna adui wala rafiki wa kudumu.

Ni James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR, aliyejitosa kuwekea pingamizi wabunge wa CUF kisiwani Pemba katika uchaguzi mdogo wa Pemba baada ya mauaji ya 26 na 27 Januari 2001, Unguja na Pemba,

Katika uchaguzi huo wa marudio na pingamizi la NCCR ya James Mbatia, ndimo ulizaliwa msamiati mpya wa “kura za maruhani.”

Hadi leo, Mbatia hajaeleza wanachama wa CUF, nani alimtuma kufanya kazi ile. Kazi chafu ya Mbatia ndiyo ilisababisha majimbo saba ya uchaguzi kisiwani Pemba kuchukuliwa na CCM.

Hadi sasa haijafahamika iwapo Mbatia alikuwa anajituma au alitumwa na wale ambao leo hii ndio wandani wa CUF katika serikali ya umoja wa kitaifa (CCM).
Wala siyo kweli kwamba Hamad ana mapenzi makubwa kwa NCCR. Anataka kuitumia kwa manufaa ya CUF na labda hata kuisajili katika muwafaka wake na CCM.

Kisichofahamika kwa wengi ni kwamba tangu mwaka 2005 Hamad amekuwa kiongozi wa upinzani ndani ya bunge. Kwa nafasi yake hiyo, serikali ilikuwa inampa gari, nyumba na marupurupu mengine.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka bungeni, kila mwaka kiongozi wa upinzani hutengewa na serikali karibu Sh. 200 milioni.

Baadhi ya wafanyakazi wa Bunge wanadai kuwa hakuna mahali popote katika kumbukumbu zao, panapoonyesha fedha hizo kutumiwa kwa kazi ya kuendesha shughuli za kambi ya upinzani.

Ni Hamad na maofisa wa bunge pekee wanaoweza kuzungumzia kwa ufasaha matumizi ya fedha hizo.

Sasa uchaguzi wa mwaka huu, umemuondoa Hamad katika kiti chake. Umechukua gari lake. Umebomoa nyumba yake. Umehamisha marupurupu yake.

Huo ndio msingi wa Hamad kutaka kuungana na NCCR. Anataka kulazimisha kuundwa “kambi ndogo” ambayo, kwa msaada wa CCM, anataka itambuliwe bungeni ili aendelee kupata marupurupu kwa “dirisha la banda la uwani.”

Je, Ofisi ya Spika itakuwa tayari kuingia katika gharama ambazo ziko nje ya bajeti ili kumfurahisha Hamad? Je, serikali iko tayari kuingia katika kinachoelekea kuwa aina fulani ya ufisadi kimatumizi?

Je, Spika Anna Makinda anaweza kujiingiza katika mchezo mchafu wa kusaidia kubadilisha kanuni za bunge ili kuibeba CUF na kuitia hasara serikali? Hekima inasema, “Hawezi.” Hawezi kukubali kufadhili mradi huu binafsi wa Hamad au CUF.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu:

NINAKUPA PONGEZI NDUGU SAED KUBENEA KWA MAKALA YAKO ULIYOANDIKA KWA UTUVU NA USHAHIDI ULIOKUWA WA WAZI, USIKATE TAMAA NA WATU WANAOKUPIGA VITA.HII NA BAHARI HAIKOSI MAWIMBI NA PIA HAIKOSI MISUKOSUKO,JITAHIDI KUSEMA UKWELI PALE PENYE UKWELI NA KERO NA IKIBIDI SIFIA PALE PANAPOSTAHILI KUSIFIA KILLA LA KHERI

Gazeti zuri. Waandishi wazuri ingawa si wote. Lakini linachelewa kuwekwa kwenye mtandao. Wanaomshambulia Kubenea wanamwonea. Hivi mnataka atoe sadaka kiasi gani kwa mapenzi ya nchi?

Si vizuri kumsifia mtu bila sababu. Kubenea ni miongoni mwa wachache tulio nao nchini kwa sasa.
Bila kumtaja mzee Tegambwage aliyekuwa na Kubenea siku ya kutupiwa tindikali ni usaliti. Huyu mzee hana mfano ukiachia mbali Kubenea. Soma maandishi yake. Naungana na waliosema kuwa Kubenea, Tegambwage, Nkwazi Mhango, Sued K Hilal, Ezekiel Kamwaga na kidogo Mwanakijiji si waandishi wepesi hata kidogo. Tuwape big up zao hata kama tunapingana na mawazo yao.

Nasema leo na kama mungu atazidi kuniazima pumzi yake tena na tena nitazidi kukupongeza Ndg Saidi Kubenea, kwanza ni kwa kukubali kwa moyo wako wote,pasipo kujali hatari yoyote inayoweza kuyakabili maisha yako binafsi pamoja na familia yako,na kuamuwa kwa moyo wako wote kusimama kidete kutetea haki ya mtanzania ambayo inaonekana dhahiri imeshaporwa na TABAKA TAWALA,naamini wa kukulipa hapa duniani hayupo ila thawabu yako iko kwa Mungu pekee.Mi kama mwanaharakati nasemaaa "NO RETREAT NO SURRENDER" Tuko pamoja kaka na AGENDA yetu inayowabeba Watanzania wote japo MAJORITY hawajui maana ya AGENDA hii KATIBA MPYA na TUME HURU ya uchaguzi.

KUBENEA NI MWANDISHI HODARI NA MCHAPAKAZI KWELI, LAKINI KWA SIKU ZA HIVI KARIBUNI UMEJIONYESHA WAZI UMEEGEMEA UPANDE MMOJA ZAIDI,KAMA GAZETI LA MWANANCHI YEYE NI MWANACHAMA KABISA WA CHADEMA NA NI KWELI MAANA ANAEKUFADHILI LAZIMA UMTUMIKIE HATA KAMA NI JAHILI,MAANA SIKU HIZI ANGALAU RUZUKU INAPATIKANA TOKA KWA BOSS MBOWE HONGERA SANA

wewe ni zaidi ya mwanaharakati mr kubenea, work hard bro..

pamoja na kukupongeza sana kubenea unatakiwa uwe tu unatupa habari za ukweli na sio mapenzi ya chama chako kama anavyofanya jabir yaani hajifichi katika hilo, kwa hiyo nawe usifike pahala ukaonyesha kujali zaidi mapenzi ya chadema kuliko ukweli ulivyo. uwe tayari kutueleza chadema inapoboronga na pia kama ulivyofanya kwa cuf safi. kuendelea kushabikia vyama vyenu tu nasi tutachoka kusoma habari zenu tutafahamu nanyi mupamoja na hao wanene wanaotafuta maslahi yao binafsi na si taifa kama wanavyojinadi.usifike pahala ukajaribu kutuonyesha kwamba hakuna chama ila ni chadema, hio sio kweli mana tunaona na tunasikia tunazo fursa za kuchagua chama ama kubaki bila chama. jitahidi kuchapa kazi kwa misingi ya uadilifu zaidi

Sales & Marketing
F.A.Glass Work

ninakupongeza mno saidi kubenea kwa makala yako ya hamad rashid aking'ang'ania uongozi wa kambi ya upinzani. ni kweli cuf huwa wanaimba nyimbo ya haki sawa kwa wote na kuzizungumzia shida za wapemba kana wao ndio wakombozi wao lkn ukweli ni kwamba sio wakombozi wa wapemba wala wazanzibar bali ni ukombaji wa maisha mazuri kwa kundi fulani ndani ya cuf. na hali inavyokwenda bungeni haileti uchangamfu kama upinzani ulivyotakiwa uwe kunaonekana watu kugombea utukufu na maslahi fulani why? tunahitaji watpinzani wa kuikosoa serikali kwa maslahi ya wananchi wote na sio ubabaishaji wa baadhi ya viongozi. said endelea kuwapa vibomu vyao hao usiwe kama waandishi wengine kazi yao kusifu tuu japo kiongozi wao ameboronga sina haja ya kuwataja kwa majina. ni lazima muonyeshe kwamba hili ni gazeti la umma kwa kuwapa michapo ya kitaifa zaidi na si mapenzi tu.
jitahidini vijana wangu kutupa elimu ya kweli na sio mambo ya ubabaishaji
big up kubenea na timu yako makini

Sales & Marketing
F.A.Glass Work

Makala hii imesimama na imenigusa sana nakupongeza sana Mr.Kubenea siku zote umekuwa ukisimamia ukweli tupo pamoja nawe,Watz tunahitaji waandishi wa wa type yako.Siku zote mti wenye maembe ndio hupigwa mawe tumeyaona haya kwako na pia gazeti la Mwanahalisi,kipindi cha nyuma tuliyaona kwa chama cha CUF na leo tunayaona kwa CHADEMA.Kinachonisikitisha ni CUF kujisahau na kuyasahau mateso waliyoyapata na kukubali kutumiwa kuwapiga mawe wenzao, watz tunajua kinachoendelea na tulio wengi tunajua CUF si chama cha upinzani kwa kimejionyesha chenyewe.

Mkombe umemuonea Kubenea bure. Yawezekana Jabir akawa mtu wa majungu na rafiki yake. Muhimu hapa tusimhukumu mtu kwa urafiki wa mwingine bali kazi yake. Toa mapungufu ya hoja ya Kubenea na si kumleta Jabir hata kama mna ugomvi naye.
Nimetokea kusoma makala za Jabir ambazo nyingi ni za kumfagilia maalim Seif kwa 'maridhiano ya chumbani'.
Kama Kubenea angekuwa anaendeshwa na umbea wa Jabir basi asingeigusa CUF kusema imeingia ndoa ya mkeka na CCM. Give the devil it due where necessary. Nimemheshimu Kubenea kwa kutokuwa na ushabiki wa kijinga kama ambayo wanaotetea vyama vyao wanavyofanya.
Kama tutaacha ushabiki, tutaona na kusema ukweli kuwa Mwanahalisi ni gazeti pevu lenye waandishi mahiri kama Kubenea, Nkwazi Mhango, Ndimara Tegambagwe, Hilal Sued na wengine.
Hakuna haja ya kufanya tathmini kinafiki na kuangalia watu badala ya hoja. Mkombe rudia kusoma makala husika ndipo useme vinginevyo hueleweki zaidi ya kuonekana kama mbabaishaji.

Wananchi wa Tanzania umakini ni kitu kidogo sana ila kinamsingi mkubwa mno ukweli ni kwamba siasa nijambo linalo haribu nchi na kujenga nchi. tusikalie kujaza bongo zetu mitazamo ya kimapenzi ya siyo kua na fikra za kujenga nchi ukijiuliza CCM ni Nini?,JE?chadema,Cuf,na majina mengine ya vyama.kati ya vyote hivyo utakuta nivimeundwa na watu kama sisi ila wenye mitazamo tofauti na asilimia ndogo sana ndio wenye kujali umati wa Watanzania milioni45,na sio kwenye chama kimoja tu bali ni kwa vyama vyote ukitaka kujua angalia walio toka chama kimoja kwenda kingine utakuta kuna sababu ya maslahi na si Watanzania sisi maskini. utashangaa kwa watu wapenda nchi bajeti ya kamati ya bunge la upinzani ni ya nini? au ya chama tawala inamaana gani? kama unapenda nchi kwanini? usiipinge? iende kwa walimu wa shule za msingi wananchi tumebakia ushabiki usiokua na maana wenzetu wanakula nchi siasa chafu watoto hawajui kusoma mpaka darasa la sita

Siku zote nilikuwa naamini kuwa Kubenea ni mtu mwenye uweledi na nikawa nashangaa sana vipi wataweza kuishi na mtu wa majungu tu kama mwandishi Idrisa Jabir.

Ama kweli washahili wamesema"..hata ukmta kwenye chupu ataonesha kidole tu na kusema nimo humu" Kubenea amenihakikishia kuwa ni mbumbumbu wa siasa, hana uweledi na mtaji wake ni majungu tu.

Endelea kusambaza "tumbaku" watu watakwenda chafya na mwisho watajitenga kunusa tumbaku yako. Na hicho ndio kifo chako.

Kubenea umelonga, kinachowaumiza CUF ni kupungua ruzuku yao ya kila mwezi, kukosa nafasi ya kiongozi wa upinzani, na kukosa hiyo bajeti ya 200m kwa mwaka. Hilo la bajeti ya mwaka kalitaja Hamad mwenyewe jana kwenye mdahalo kwani watu wengi tulikuwa hatulijui, nami namshukuru kwa kutufumbua macho.

Kazi nzuri sana kubenea, achana na hawa mavuvuzela wanaoandika wasichokijua, CUF si chama cha upinzani tena, nawashauri chadema waachane na hawa CUF watengeneze upinzani wao wenyewe wenye nguvu, wananchi wengi bado wanawaamini na wako nyuma yao. Pia wasifikirie kumuingiza Mbatia wala chama chake kwenye upinzani wao, sijapata ona mtu mnafiki kama mbatia, si mpinzani siku zote anapinga yale ya upinzani na kuishabikia CCM. Big up Kubenea, kazi nzuri

Chadema na Cuf yamalizeni chumbani mambo yenu. Niliona wakati wa Kampeni Mtu mmoja wa Cuf anaitwa Juma Duni ndo alikuwa anaishambulia Chadema sana. Chadema nayo ikajibu mapigo na inaelekea mapigo ya Chademaa yanaanza kuisambaratisha Cuf kwa bara na baadhi ya maeneo ya Visiwanio. Naomba wayamalize haya maomba chumbani wala wasilete huku sebureni. Tumechoka kusikia haya madudu .... Tunataka mabadiliko.

acha chuki binafsi Kubenea kumbuka Hamad na wenzake walisusia baraza la mawakilishi kwa zaidi ya miaka 3 bila kuchukua hata senti.
hata hao unaowapigia debe na kuwasem kwa uzuri hawawezi kuthubutu kimsingi chadema na cuf hawawezi kuwa pamoja coz kwenye issues za msingi wa tofautiana sio hizo propaganda zako unazoleta.
CUF wana msimamo thabiti kuliko chama chochote cha siasa uho ndio ukweli .
unanchojaribu kufanya ni kutujaribu kutujengea chuki na CUF na kutengeneza mapenzi kwa chama chako

Cuf kwa sasa ni CCM B. Wewe unayetetea Cuf inaonekaka Hujajua kwamba mgomo wa Cuf ndio uliokuwa na madhara kuliko uliochukuliwa na Chadema. Ni afadhali Chadema wanachukua posho zao bungeni ambazo ni haki yao ya kisheria, kuliko Cuf wanaosaliti damu za wale walioandamana kuwaunga mkono kule Zanzibar kwa kukubali kuwa CCM B. Ukweli ni Kwamba Cuf imesaliti upinzani na Chadema ndio wamebaki kuwa wapinzani wa kweli. Hivi sas hakuna tena upinzani kule Zanzibar, vilivyopo ni vyama tawala.

Kinachoniudhi mimi ni hawa "waandishi" wanaokimbilia kutujaza misiasa yao badala ya kuandika na kuacha wasomaji tuamue wenyewe. Wewe Kubenea, kwa nini unaupunguza "upinzani" wa kisiasa tanzania kwa vyama hivi witatu (CCM, CUF na CHADEMA)?
Halafu unaashiria kuwa kila "mpenzi" wa CHADEMA ndiye anayeitakia mema nchi yetu. Kumbukeni nchi ni yetu wote, si ya vyama. CHADEMA wana kazi kubwa sana ya "kufua nguo zao chafu" kabla hawajapewa nchi kuiongoza.