Daktari Abdullah, mshindani aliyemsumbua rais Karzai


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 November 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Dk. Abdullah Abdullah

ILIKUWA 6 Mei mwaka huu, Dk. Abdullah Abdullah alisajili jina lake kama mmoja wa wagombea kiti cha urais wa Afghanistan akichukuliwa mshindani mkubwa wa Hamid Karzai, rais wa nchi hiyo iliyoathirika mno na vita.

Dk. Abdullah aliteua watu wawili wengine kama wasaidizi wake iwapo atachaguliwa na wananchi. Hawa ni Humayun Shah Asefi, ambaye angekuwa makamu wa kwanza wa rais, na Dk. Cheragh Ali Cheragh makamu wa pili.

Katiba ya Afghanistan inaruhusu kuwepo makamu wawili wa rais kwa lengo la kuimarisha utendaji wa serikali huku mkazo mkubwa ukiwa katika haja ya kujali uwiano wa kimakabila katika kuwakilishwa kwenye nafasi za juu za uongozi wa taifa.

Matokeo ya uchaguzi yasiyo rasmi yalipotangazwa 16 Septemba, yalionyesha Dk. Abdullah alishika nafasi ya pili akipata asilimia 27.8 ya kura zilizopigwa kabla ya matokeo rasmi kuonyesha alipata asilimia 31.

Rais Karzai alipata chini ya asilimia 50 ambayo ingemwezesha kutangazwa mshindi bila ya kulazimika kusubiri awamu ya pili ya kura ya urais.

Isitoshe, matokeo yalionyesha uchafu mwingi katika usimamizi wa uchaguzi na hivyo kuzusha maswali mengi kuhusu umadhubuti wa Tume ya Uchaguzi ya Afghanistan (IEC). Vilio vya kuitaka irekebishe uchafuzi huo yalipata sauti ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi.

Kauli za kutaka marekebisho ya matokeo ya uchaguzi huo, zilianza kwa Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown. Viongozi wa mataifa mengine ya Ulaya waliwafuata.

Hatimaye, rais Karzai alikubali kuitishwa kwa kura ya awamu ya pili ili wananchi wa Afghanistan wapate haki ya kuchagua kiongozi wamtakaye. Alijua fika kwamba Dk. Abdullah ndiye atakuwa mshindani wake katika uchaguzi uliopangwa 7 Novemba.

Ilipofika Novemba mosi, Dk. Abdullah alishangaza ulimwengu kwa kutamka kutoshiriki awamu ya pili ya kura ya urais. “Sina imani na serikali ya Rais Karzai kama ina uwezo wa kusimamia uchaguzi huru na wazi,” akasema.

Hapo ndipo Tume ya Uchaguzi ilipositisha uchaguzi mwingine na kuamua kumtangaza rasmi Karzai kama rais mpya. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitafsiri uamuzi wa Dk. Abdullah kama pigo kwa uhalali wa Karzai kushika urais kwa awamu ya pili ya miaka mitano.

Nani Dk. Abdullah

Dk. Abdullah, daktari wa macho mwenye umri wa miaka 49 aliyezaliwa mjini Kabul, alikuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya rais Karzai. Alitokea kujishughulisha na harakati za kusaidia wakimbizi nchini Pakistan na baadaye akaibukia katika kundi la upinzani nchini Afghanistan lililoongozwa na Jenerali Ahmed Shah Masood.

Alikuwa mshauri wake mwandamizi miaka ya 1980. Katika serikali iliyoongoza kipindi kifupi chini ya kundi la Muungano wa Kaskazini (Northern Alliance), Dk. Abdullah aliteuliwa waziri wa mambo ya nje.

Aliendelea na wadhifa huo nje ya nchi baada ya serikali ya Taliban kushika hatamu za uongozi. Taliban waliangushwa mwaka 2001 pale Marekani na washirika wake walipovamia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na Al Qaeda, kundi la magaidi lililoongozwa na Osama bin Laden.

Dk. Abdullah alikuwa msemaji mkuu wa Jenerali Masood ambaye aliuawa wakati rais Karzai aliposhika madaraka chini ya mikakati ya majeshi ya washirika. Aliendelea na kazi hiyo.

Serikali ya muda baada ya Taliban kuangushwa, ilidhibitiwa na kundi la kaskazini, hali aliyotaka kuibadili rais Karzai. Wafuasi wake walisema alinuia kuleta uwiano lakini wapinzani walisema alidhoofisha kundi hilo lililochangia kung’oka Taliban.

Dk. Abdullah hakuwa na ngome ndani ya Northern Alliance, ikithibitisha sababu za kubaki muda mrefu katika serikali ya rais Karzai. Ila hiyo pia huenda ilikuwa sababu ya kuondolewa kuwa waziri wa mambo ya nje.

Katika kipindi cha kampeni ya urais mwaka huu, Dk. Abdullah alisema, “(Rais) Karzai aligeuza bahati ya dhahabu kuwa msiba. Hakuna sababu ya kumpa kipindi kingine cha miaka mitano.”

Dk. Abdullah alihisi rais alijitenga na umma kutokana na namna alivyoshughulikia tatizo la ufisadi na harakati za wapinzani. Hata hivyo, uhusiano wake wa karibu naye, ulichelewa kumuonyesha kama akimpinga kisawasawa.

Bado msimamo wa Dk. Abdullah, ambaye alifukuzwa uwaziri wa mambo ya nje mwaka 2006, ni kwamba rais Karzai hana uwezo wa kubadilisha chochote kiuongozi. Atashindwa na tatizo la ufisadi na upinzani.

Kwanza, anasema uamuzi wa awali wa tume ya uchaguzi kutoitisha uchaguzi mpya baada ya uchafuzi, ulimaanisha uvunjaji katiba. Serikali inayotokana na uchafu kama huo “haiwezi kujiita ni halali, haiwezi kumaliza rushwa.”

Lakini hakutamka kupinga kisheria ushindi wa Karzai baada ya kutangazwa na tume hiyo.

"Mchakato umekamilika katika hali hiyohiyo ya uvunjaji sheria,” anasema… ninaachia wananchi wa Afghanistan kuamua."

Mara tu alipotamka hivyo, Dk. Abdullah aliulizwa kuhusu mauaji ya wanajeshi watano wa Kingereza yaliyotokea Jumanne iliyopita katika shambulizi kusini mwa jimbo la Helmand. Alisema polisi alishambulia askari hao kwenye kizuizi.

Dk. Abdullah alituma salamu za rambirambi kwa familia za wanajeshi hao na kuelezea masikitiko yake na kushindwa uwajibikaji kwa upande wa serikali ya rais Karzai.

Alisema tukio hilo lililotokea miaka minane tangu majeshi ya kimataifa kusaidia kuimarisha usalama nchini Afghanistan, linathibitisha haja ya kuwepo msaada zaidi wa kijeshi.

Dk. Abdullah anatarajiwa kujumuishwa katika serikali mpya itakayoundwa, hasa kwa kuwa rais Karzai ameahidi ataunda serikali itakayoshirikisha kila kundi katika nchi. “Serikali ijayo itamridhisha kila mwananchi Afghanistan,” alisema.

Marekani na Uingereza, mataifa yanayoonekana kumuunga mkono rais Karzai, yametaka aunde serikali ya umoja wa kitaifa ili kuimarisha umoja katika nchi ambayo bado inatatizwa na vikundi vya upinzani.

Makala hii imeandaliwa na Mwandishi Wetu kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

0
No votes yet