Daladala na dhuluma kwa abiria


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe ametangaza alichokiita “kiama” kwa wamiliki wa daladala na madereva wasiofuata sheria.

Dk. Mwakyembe aliyasema hayo wiki iliyopita katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Alisema, “…sasa muda umefika wa kutekeleza sheria zilizopangwa.”

Amesema amekuwa akipokea simu za malalamiko kutoka kwa wananchi wakielezea kero wanazozipata kutoka kwa madereva wa daladala wanaowatoza nauli kinyume cha utaratibu na wengine kukatisha njia.

Kauli ya Dk. Mwakyembe inadaiwa kutokana na taarifa za wanachi wanaompigia simu kumweleza kero wanazozipata barabarani naye kuamua kuchukua hatua.

Wananchi wamechukua uamuzi wa kutafuta namba ya waziri na kumpigia baada ya wahusika wengine wanaowaeleza shida wanazozipata barabarani kutochukua hatua.

Kwanini apigiwe waziri wakati namba ya kupiga bure (0732 928 723) ya traffiki imetolewa?

Kwanini apigiwe waziri wakati Sumatra wapo na polisi wa barabarani wanaonekana kila sehemu? Inawezekana wameelezwa lakini hawachukui hatua? Je, kuna maslahi wanayoyapata katika kimya chao?

Tangu kuvunjwa kwa Mamlaka ya Usafiri na Leseni Mkoa wa Dar es Salaam (DLTRA), ambayo iliongozwa na David Mwaibula, madereva wa daladala hawakuwa na mtu au ofisa wa kuogopa na kuheshimu.

Bali sheria zipo. Wasimamizi wa sheria za barabarani Sumatra; na trafiki nao wapo. Kwa nini hakuna woga katika kutenda makosa barabarani?

Wakati wa uongozi wa Mwaibula, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mamlaka hiyo, haikuwa rahisi kuona daladala zinakatisha njia kama sasa.

Hii ni kwa kuwa Mwaibula hakuwa bosi wa kukaa ofisini kusubiri ripoti kutoka kwa wasaidizi wake. Alinyanyuka kitini na kuingia barabarani kuhakikisha anaitumikia dhamana yake.

Waziri Dk. Mwakyembe anasema watawasaka wamiliki na madereva wanaovunja sheria kwa kuwatoza nauli kubwa kuliko kiwango na wanaokatisha njia.

Dk. Mwakyembe anasema “kuwasaka.” Hakuna haja ya kuwasaka watu hao. Wamejaa tele.

Kwa mfano, asilimia 90 ya daladala zinazokwenda Gongolamboto, Pugu na Chanika, hukatisha njia.

Polisi vituo vya Buguruni, Tazara, Stakishari Ukonga na kile cha Gongolamboto, wanalijua vizuri hili; wala halina haja ya uchunguzi.

Huo ni mfano wa njia moja tu, barabara ya Nyerere, ingawa ziko nyingi. Hata Sumatra wanalijua vizuri hili. Kama hawalijui, basi hawawezi kusimamia utekelezaji wa kile anachosema waziri.

Dk. Mwakyembe aende Buguruni nyakati za jioni aone wananchi masikini wanavyokamuliwa na waendesha daladala. Nauli halali ya Buguruni mpaka Gongolamboto, Sh. 300, haifuatwi. Badala yake abiria wanatozwa Sh. 900 mpaka 1,000 – ziada ya asilimia 200.

Daladala za Gongolamboto, Pugu na Chanika haziendi moja kwa moja kama zilivyosajiliwa. Zinatoka Buguruni na kwenda Lumo, Yombo kwa Limboa au Mwisho wa Lami.

Madereva wakishashusha abiria huko ambako si ruti yao, hwenda Vingunguti au Jeti, kupakia abiria na kuwashusha Banana.

Wakitoka Banana wanakwenda Gongolamboto. Wakitoka Gongolamboto ndio wanapakia abiria wa kwenda Pugu kwa Sh. 300 na Chanika kwa Sh. 500.

Kwa maana hiyo, abiria wa Gongolamboto, Pugu na Chanika wanapanda na kushuka daladala nne badala ya moja.

Sumatra na trafiki wanalifahamu hili. Tunapanda daladala na kushuka nao; wao wenyewe, wake zao na watoto wao. Wanashuhudia.

Abiria wanalazimika kupanda basi kutoka Buguruni mpaka Vingunguti au Jeti kwa kulipa Sh. 300. Hapo, wanapanda daladala nyingine mpaka Banana kwa kulipa Sh. 300 nyingine.

Wakishushwa Banana wanapanda daladala nyingine au hiyohiyo iliyowashusha, mpaka Gongolamboto kwa bei mpya ya Sh. 300.

Abiria aliyepaswa kwenda Gongolamboto kwa Sh. 300 analipishwa Sh. 900; aliyepaswa kwenda Pugu kwa Sh. 400 analipishwa Sh. 1,200 na yule wa Chanika ambaye alipaswa kulipa nauli halali ya Sh. 700 anakwapuliwa Sh. 1,400. Ni dhulma mtindo mmoja!

Askari trafiki wanajua yote haya. Utawaona wamekusanyika Buguruni na daladala zinatangaza mbele yao kwenda njia zisizosajiliwa. Hakuna hatua wanazochukua.

Nenda Banana na Gongolamboto nyakati za jioni. Magari yanayotakiwa kutoka Buguruni kwenda Gongolamboto, Pugu, Chanika, Mvuti na Dondwe, utakuta yameegeshwa.

Sasa badala ya kutoka Buguruni, yanapakia abiria Banana kwenda Gongolamtoto, Pugu na Chanika. Yote yanafanyika mbele ya macho ya trafiki.

Maana yake ni nini? Kwamba gari limetoka Buguruni dereva akitangaza kwenda Banana. Hapo, abiria wa mbali wanaachwa. Wengi wanaopanda ni wale wanaokwenda Banana.

Lakini dereva akishateremsha abiria wote, hutangaza kuendelea mbele zaidi; kwa nauli tofauti. Wanaokwenda wanapanda tena basi lilelile kwa nauli nyingine. Dhuluma kubwa.

Kutoka Buguruni, ikitokea daladala kwenda moja kwa moja Banana au Gongolamboto nyakati za jioni, abiria hutozwa Sh. 500 mpaka Sh. 1,000.

Lakini daladala hizi zinapotoka Chanika, Pugu na Gongolamboto hwenda moja kwa moja Kariakoo na Buguruni kwa nauli halali.

Kwa mfano, Sh. 500 kutoka Pugu hadi Kariakoo; Sh. 700 kutoka Chanika hadi Buguruni; Sh. 400 kutoka Pugu hadi Buguruni na Sh. 300 kutoka Gongolamboto hadi Kariakoo au Buguruni.

Ni bahati mbaya kwamba polisi wapo, Sumatra wapo, lakini hakuna aliyejitokeza kusaidiana na wananchi kupambana na mtandao huu wa kudhulumu wananchi masikini.

Itakuwa faraja kubwa kwa wananchi hawa iwapo Dk. Mwakyembe atafanikiwa kudhibiti makondakta na madereva wa daladala.

Bali najenga shaka iwapo Sumatra, ambao wamekuwa wakiona yote haya yakitendeka, wataweza kutekeleza kauli au amri ya waziri.

0784 447 077 babujongo@yahoo.com
0
No votes yet