Daladala Sumatra, Majembe wastukia

WAMILIKI na wafanyakazi wa mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam, wamestukia mradi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na Majembe Auction Mart wa kutoza faini holela barabarani.
Wakiongea katika mahojiano na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema mradi wa kukamata magari ya abiria jijijini kwa kutumia Majembe Auction Mart, utakuwa umebuniwa kwa ajili ya “manufaa binafsi.”
“Naamini Majembe haikuwahi kuwa na wafanyakazi wengi kama hawa, hivyo wameajiri watu baada ya kupewa tenda. Sasa wamepata wapi mafunzo ya Usalama Barabarani kama sio ubabaishaji,” anasema Juma Ally mmiliki wa gari Na. T 909 ABS Toyota DCM linalofanya safari zake kati ya Tabata na Mnazi Mmoja.
Amesema kazi inayofanywa na kampuni ya Majembe haifanywi kitaalam na kwamba huenda huo ni mradi binafsi kwa wahusika. Anasema Majembe ni mawakala, hivyo wanafanya kazi na kulipwa kutokana na jinsi wanavyokusanya mapato. Hapa lazima watakuwa wakitubambikia makosa ili kuweza kuingiza fedha nyingi.
Jumatatu ya wiki iliyopita, ilikuwa kero tupu kwa wakazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam kutokana na mgomo wa wenye mabasi na madreva wa daladala kupinga kile walichosema “kunyanyswa na Majembe Auction Mart.”
Madreva waliegesha magari vituoni. Wengine wakakaa ndani ya mabasi na wengine wakatoka, alimradi hayaondoki, wakipinga hatua ya kampuni ya madalali ya Majembe ya kuwakamata na kuwatoza faini kwa kile kilichoitwa “kutofuata taratibu za usafirishaji.”
Pamoja na mgomo huo kuhusisha mkoa mzima wa Dar es Salaam, lakini vilio na masikitiko vilitokea kwa wakazi wa Tabata, ambao hawakupata usafiri wa kwenda kokote nje ya maeneo yao.
Watu wengi walitembea kwa miguu kwa umbali wa kilometa 15 kwenda kazini na makazini. Hata hivyo, mgomo huo ulisitishwa baada ya siku mbili ukifuatiwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi na Sumatra kuwa utaratibu wa kukamata magari “uangaliwe upya.”
Mwenyekiti wa madereva wa daladala Tabata, Hassan Kurwa, anasema waliamua kufanya mgomo kutokana na kutozwa faini kubwa na kampuni ya Majembe.
Kulwa anasema kilichowauma hadi kufikia kufanya mgomo ni kampuni ya Majembe kuwatoza faini kubwa za papo kwa papo kuanzia Sh.100,000 hadi 250,000 kwa kile walichoona ni kosa.
Anasema waliamua kuweka magari yao nyumbani au kutembea usiku ili kuepuka kupigwa faini zingine ambazo amedai ni za kulazimishwa na Majembe ili kuongeza kipato kwa kampuni hiyo.
“Hawa jamaa ni zaidi ya askari wa Usalama Barabarani kwani wamekuwa wakitoza faini kubwa hata kwa kosa la kutovaa viatu wakati umevaa sare nzuri,” anasema Kulwa.
Kwa mujibu wa Majembe, zoezi la kukamata magari “yanayokiuka taratibu na sheria barabarani” liliandaliwa kwa pamoja na Majembe, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kwa kushrikiana na jeshi la polisi kitengo cha Usalama Barabarani.
Majembe Action Mart, ambao pia wanatumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatilia wadeni sugu, ndio walipewa jukumu la kufuatilia na kukamata madreva wa magari ya daladala ambao wanadaiwa kutofuata sheria.
Ofisa mafunzo na Usalama wa Sumatra, Aaron Kisaka amesema Majembe wamepewa mkataba wa mwaka mmoja kwa kushirikiana na jeshi la polisi katika kukamata na kutoza faini ya papo kwa papo madreva wa magari watakaopatikana na makosa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kisaka amesema Majembe imepewa jukumu la kuendesha operesheni ya kukamata magari kwa kutumia sheria Na. 9 ya mwaka 2001 na kwamba kabla ya hapo madereva walikuwa wakiwakwepa maofisa wa mamlaka hiyo.
Edson Mwaijande mmoja wa wakazi wa Tabata ambao walipata adha kubwa ya usafiri siku hiyo anasema, serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo kwa umakini kwani wanachi ndio wamekuwa wakipata shida kutokana na mgomo huo.
“Kweli mgomo umetuathiri sana. Ilifikia wakati mimi na mke wangu tukapanda Pick Up (gari isiyo ya abiria) ili tuwahi kazini. Hili mara nyingi linatukumba sisi watu wa Tabata pekee; “sijui tumekosa nini?” anasema Mwaijande.
Lakini Kisaka amewataka wafanyakazi wa Majembe nao kufanya kazi kwa kufuata sheria na sio kwenda kinyume na taratibu za mkataba. Amesema, “Madareva nao wana haki ya kulalamika kwetu kama hawatendewi haki na Majembe; na ikibainika kwa wanakamatwa kinyume cha sheria mamlaka iko tayari kuvunja mkataba na kampuni hiyo.”
Afisa uhusiano wa kampuni ya Majembe, George Kyatika amesema ana imani na vijana wake na kwamba wamepewa maelekezo na mafunzo ya usalama barabani.
Alisema amekuwa akipata malalamiko kutoka kwa wamiliki wa daladala lakini wao wamekuwa wakifanya kazi kwa misingi na taratibu waliozopewa na SUMATRA; hivyo wanaokwenda kinyume wanatakiwa kwenda kulalamika katika Mamlaka hiyo.
Naye Kamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani, James Kombe anasema zoezi hilo ni la kudumu na lina lengo la kutoa usafiri wa uhakika kwa wakazi wa jiji.
“Lengo ni kutoa utaratibu mzuri kwa madereva ikiwa ni pamoja na kuepuka ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikitokea barabarani na hasa kwa mabasi ya daladala,” anasema Kombe.
Hata hivyo, Kombe hakusita kuwalaumu wamiliki wa vyombo hivyo kutotoa maelekezo mazuri kwa madareva na makondakta wao namna wanavyofanya safari zao kinyume na taratibu za usalama barabani.