Danny Mrwanda 'amefulia'?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 07 July 2009

Printer-friendly versionSend to friend

TIMU ya soka ya Simba, kama zilivyo klabu nyingine zenye misuli ya kifedha, imefanya kufuru katika usajili, kwa kujaza nyota wa ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa waliotua katika kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Bara na michuano ya kimataifa ni nyota wa Kitanzania aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa katika klabu ya Al Tadhamon ya Kuiwat, Danny Mrwanda.

Mrwanda amerejea Simba baada ya kucheza ughaibuni kwa takribani miaka miwili. Alikwenda huko na Nizar Khalfan ambaye baada ya mwaka mmoja alirudi nyumbani kuichezea Moro United.

Tofauti na Nizar, Mrwanda aliripotiwa kuwa juu zaidi kimafanikio huko ugenini, hali iliyozidisha raha katika nafsi za Watanzania waliokuwa na matumaini makubwa ya kusikia nyota yake ikipaa zaidi na zaidi, hasa kufungua milango ya kucheza Ulaya.

Naye, mara kadhaa alikaririwa akisema hatarudi nyuma, bali kuhakikisha anacheza soka Ulaya.

Kinyume chake, naye amefuata mkumbo wa nyota wengi wa Kitanzania wanaokwenda nje ya nchi na kurejea baada ya muda mfupi. Amerejea katika ligi ya nyumbani ambako ukiondoa nyota wa kigeni, wazalendo hawalipwi vizuri.

Na sababu kubwa inayotajwa kuwa inawarudisha nyumbani nyota wetu ni uvivu, kiasi cha kushindwa kuvumilia mazoezi makali, mazingira magumu ya `kuchungwa’ ugenini na ulimbukeni.

Siwezi kumweka Mrwanda katika kundi hilo, lakini ninachoweza kueleza ni kwamba, tabia hii ya nyota wa taifa kubahatika kwenda nje, na kisha kurudi nyumbani baada ya muda mfupi, kamwe haitoi picha nzuri.

Hali hii, naweza kusema inajenga taswira mbaya, hasa ya kuwaonyesha chipukizi wanaochipukia kwamba, ni ngumu kwa nyota wa Kitanzania kucheza soka ya kulipwa Ulaya.

Na kama dhana hii inajengeka kichwani mwa mchezaji wa Kitanzania, kinachofuatia ni kulewa sifa haraka, akijiona aliyefika kilele cha mafanikio, hasa kama amebahatika kucheza Simba au Yanga.

Si vibaya tukaziongeza Azam FC na African Lyon zilizoibuka kwa kasi katika kupapatikiwa na nyota wa soka wa kigeni na hata wa Kitanzania kutokana na klabu hizo kuingia katika kundi la `Malisho Bora’.

Hapa ndipo tunapojiuliza, inakuwaje kwa mchezaji mwenye umri mdogo, lakini mwenye uwezo mkubwa kisoka kama Mrwanda akate tamaa mapema na kuamua kurudi kucheza ligi ya nyumbani?

Iko wapi ahadi yake ya kuhakikisha anaitumia Tadhamon kama njia ya kwenda Ulaya na kwingineko kwenye maendeleo ya kweli ya soka?

Maswali ni mengi, lakini itoshe tu kusema kwamba, Watanzania wasiwe wepesi wa kuridhika na mafanikio ya mwaka mmoja au miwili nje ya nchi, na kisha kutamani kurejea kuwakoga wenzao waliowaacha nyumbani, badala ya kufikiria kufika mbali zaidi.

Gazeti hili lilishawahi kutoa mifano ya nyota kama Nonda Shabani aliyetoka Yanga na kufika Vaal Professionals ya Afrika Kusini alikokumbana na mazingira magumu kwa upande wake, akakimbia, lakini baada ya kutafakari akarejea na kupata mafanikio yaliyompeleka hadi Ulaya alikogeuka mmoja wa washambuliaji nyota kabisa duniani.

Kama Nonda aliyesugulishwa benchi na akina Mohammed Hussein Daima `Mmachinga’ alijiuliza mara mbili na kuamua kwenda `Mbele kwa Mbele’ na hatimaye sasa kuwa miongozi mwa watu wanaoogelea katika lindi la utajiri, inashindikanaje kwa nyota wetu wa Kitanzania?

Kwamba, faraja yao ni kuona wakishangiliwa `kinafiki’ pale Uwanja wa Uhuru, wakiandikwa kila kukicha na vyombo vya habari, au wakihongwa `mabibi’ na pombe’ kama fadhila ya unyota wao Simba na Yanga?

Ifike mahala tuseme hapana. Nyota wetu wawe na kiu ya kweli ya kimaendeleo, badala ya kusubiri kila kitu kiwafikie mezani.

Hawawaoni wenzao wa nchi za Magharibi mwa Afrika kama Nigeria, Ivory Coast na Cameroon waliojileta Yanga wakitaka angalau wajaribiwe?

Wamekuja kwa gharama zao, wakiamini baada ya kupata nafasi wataongeza sifa katika wasifu wao, na hata watakapoondoka Yanga na kwenda kujiuza kwingine, watakuwa na uzoefu wa kutosha wa kupambana ugenini.

Ndiyo maana najiaminisha kwamba, ujasiri wa Mrwanda wa kurejea haraka nyumbani badala ya kupaa kimafanikio, ni sawa na kufulia.

Alipaswa kujifunza kwa wenzao kama Mohammed Abdallah `Athuman Machuppa’ waliotua kwa mbwembwe Msimbazi, lakini mwisho wa siku wakaonekana wasaliti, angalau kwa kujaribu kuhoji maslahi yao.

Tujiulize, kama si ung’ang’anizi wa Machuppa, leo hii kwa soka yetu si angeitwa Veterani!?

Lakini angalia, ni miongoni mwa chipukizi wapya wa kisoka huko Sweden, akitajwa kuwa tishio katika siku za usoni.

Staili hii ya Machuppa ya kupambana mpaka `damu ya mwisho’ ndiyo iliyopaswa kuigwa na nyota wengine kama Mrwanda, badala ya kurejea kiholela ili kuja kuishia kushangiliwa na watu wanaowafahamu pale Uwanja wa Uhuru.

Kwangu mimi, Mrwanda `amefulia’, labda atuthibitishie kwamba uwezo wake katika soka ya ushindani umefikia kikomo, hafundishiki na hana jipya la kujifunza, ndiyo maana ameamua kurudi nyumbani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: