Democrats wachimba ushindi wa Obama

MACHO na masikio ya wengi yako kwenye chama cha Republican ambacho, wanachama kadhaa wamejitokeza kuchuana ili mmoja wao ateuliwe kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba 2012.
Mchuano mkubwa ndani ya chama hicho kwa lengo la kusaka kura za kutosha uko kwa Michele Bachmann, Newt Gingrich, John Huntsman, Ron Paul, Rick Perry, Mitt Romney na Rick Santorum.
Mwanachama atakayepitishwa ndiye atapambana katika uchaguzi mkuu ujao na Rais Barack Obama wa chama cha Democratic anayewania kipindi cha pili.
Ingawa Obama anaonekana anafanya vizuri, mgogoro umeibuka ndani ya chama chake akilalamikiwa kwamba alitumia mlango wa nyuma kupata uungwaji mkubwa wa watu ili apate kura za kutosha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2008.
Mtikisiko ndani ya Democrats uko Jimbo la Indiana ambako mwenyekiti wa chama hicho, Dan Parker, hivi karibuni alitangaza kujiuzulu wadhifa huo.
Mwenyekiti huyo amefikia hatua hiyo wakati unafanyika uchunguzi kuhusu madai kuwa ulifanyika udanganyifu wa saini za wadhamini ili kumpata mgombea anayefaa kwa urais mwaka 2008.
Parker, ambaye amekuwa mwenyekiti wa Democratic kwa miaka saba, hakutaja sababu ya kujiuzulu kwake. Lakini malalamiko juu ya uwezekano wa udanganyifu katika mbio za kuelekea Ikulu ya White House ndiyo yatakuwa yamechangia mwenyekiti huyo kuachia ngazi.
Saini nyingi za wadhamini zilizoko kwenye fomu za maombi ya Obama na Hillary Clinton, kwa ajili ya kura za maoni inadaiwa zilighushiwa na zikaidhinishwa na Ofisi ya Usajili Wapigakura ya wilaya ya St. Joseph iliyoko South Bend.
Mwendesha mashitaka wa St. Joseph County, Mike Dvorak ameanzisha uchunguzi.
Parker, alisema katika taarifa yake kwamba “baada ya miaka saba ni wakati kwa kiongozi mpya kuchukua mazuri yetu ya zamani na kushughulikia changamoto mpya za baadaye.”
Kisha alisema, “Nakipenda chama cha Democratic Jimbo la Indiana na imekuwa heshima kubwa mimi kutumikia kama mwenyekiti wake."
Katibu wa masuala ya habari wa chama katika jimbo hilo, Benjamin Ray, aliliambia shirika la habari la Fox News kwamba madai ya kughushi yanayohusisha mbio za awali za urais hayakuwa sehemu ya sababu za msingi za kujiuzulu kwa Parker. “Hapana, nasisitiza hapana,” alisema Ray.
Madai hayo yalipoibuliwa kwa mara ya kwanza Oktoba, Parker alitoa taarifa ya maandishi akisema kwamba “tunaendelea kuunga mkono uchunguzi huo kwa lengo la kubaini tukio hili lisilo la kawaida kujua lilitokeaje na kumwajibisha yeyote aliyehusika."
Kuibuka kwa madai ya kughushiwa kwa saini kumeibua pia maswali kama kweli Obama katika kampeni zake alimudu kupata saini 500 kutoka nchi nzima ili aweze kuendelea kwenye kura za maoni.
Kwa mujibu wa maofisa wa uchaguzi, saini nyingi kati ya 534 ambazo ziliidhinishwa kumruhusu Obama kuingia katika kinyang’anyiro cha kura za maoni zilipingwa. Saini 704 zilithibitishwa kuwa halali kwa Clinton.
Inakadiriwa kuwa saini 150 katika karatasi za maombi yote mawili zilikuwa feki hivyo kuashiria kuwa, katika suala la Rais Obama, idadi ya kura halali zilizotakiwa katika fomu zake hazikufikiwa.
Wapigakura wengi waliiambia shirika la habari la Fox News kwamba hawatasaini wala kupeleka majina yao yaliyoonekana kwenye fomu za maombi ya Obama.
"Ni uzushi mtupu,” alisema Charity Rorie na kuongeza kwamba saini yake na jina pamoja na saini na jina la mumewe vyote vilighushiwa. "Inatisha ... kwa vyovyote vile ni kinyume cha sheria.”
Mwenyekiti wa chama pinzani cha Republican katika jimbo hilo, Eric Holcomb, alitoa taarifa ya maandishi kuhusu hatua ya kujiulu kwa Parker akiwashutumu Democrats.
Alisema, "Uoza mwingi wa chama cha Democratic katika jimbo la Indiana unaweza kutazamwa kwa namna walivyokosa mawazo na walivyopanua utamaduni wao wa ufisadi.”
Ripoti zinasema kwamba watu apatao saba wanadaiwa kuhusika kughushi saini, lakini hakuna mashtaka yoyote yaliyoandaliwa dhidi yao.