Dhahabu yaleta balaa kwa wananchi Geita

KUISHI karibu na mgodi wa dhahabu siyo lazima iwe baraka. Kwa wananchi wengi wanaoishi maeneo kuzunguka Geita Gold Mine (GGM), dhahabu imekuwa balaa.
Wanaona wenye magari madogo kwa makubwa wakiingia na kutoka mgodini. Wanaona baadhi ya wafanyakazi na vibarua wa mgodini wakienda na kurudi. Ni kama kanda ya sinema isiyobadilika.
Hiyo ndiyo hali ya maisha katika kitongoji cha Katoma kilichopo kilometa tatu kutoka mgodi wa dhahabu wa GGM.
Wakazi wake ni watifuaji ardhi wasiostahili hata kuitwa wakulima. Hawana mashamba. Wana bustani za migomba iliyonyauka, magimbi, karanga na miti mithili ya mihogo inayowapa kisamvu.
Unaridhika mara moja kuwa umefika makao makuu ya ufukara – kilometa tatu kutoka mgodi wa dhahabu –inayiongizia taifa zaidi ya nusu ya mapato yake ya fedha za kigeni na kufanya Tanzania kuwa nchi ya tatu katika Afrika kwa kuzalisha dhahabu nyingi.
Ardhi ya Katoma ni kame kwa kipindi kirefu cha mwaka. Kitongoji kizima kina kisima kimoja cha maji.
Maji ya kisima yanafanana yaliyotumika kufulia nguo au yaliyotibuliwa na mifugo na juu yamejaa ukungu wenye chembechembe za vipande mbalimbali vinavyoelea. Anayechota sharti apembue kwa kata ukungu uende pembeni.
Kilometa tatu kutoka kwenye mgodi wa dhahabu – ambamo kuna maji ya bomba, chakula kingi na safi na maji ya kuoshea magari na kunyweshea bustani – wananchi wanakunywa maji ambayo utasita hata kunywesha mifugo.
Thamani ya dhahabu inajulikana kwa waliombali – nchi za nje – ambako inauzwa na kulinda thamani ya fedha za mataifa yao; na kwa serikali ambayo inalipwa mrabaha kutoka kwa wachimbaji wa kigeni.
Milipuko mikubwa ya baruti wakati wa kupasua mawe mgodini, hutengeneza wingu la moshi na vumbi na vyote hutua kwenye maji ya Katoma na vitongoji vingine vya karibu vya Nyakabale na Mgusu, ambayo wananchi wanategemea kwa matumizi yote – kunywa, kupikia, kuoga, kufua na matumizi mengine.
Kwa suala hili la maji, dhahabu ya Geita haijawahi kuwa baraka kwa wakazi wa vitongoji vilivyoko karibu na mgodi. Uchafuzi wa maji ambayo ni muhimu kwa maisha yao, ni balaa tupu.
Katika kijiji cha Nyakabale, Mzee Kasoboke Maselle (70) anatoa ushahidi wa alivyohamishwa na wachimbaji wa GGM ili kupisha ujenzi wa bwawa la majitaka ya mgodini ambayo yana sumu.
Bwawa hilo lililopo eneo la Nyamonge, Mashariki mwa kijiji cha Nyakabale na linatiririsha maji yenye sumu katika mto Mtakuja unaoingia moja kwa moja ziwa Viktoria.
Mwenyekiti wa Nyakabale, Stephano Minzimanunu Lufungulo, anasema kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu mgodi wa GGM na kwamba wananchi wameacha kuwaamini viongozi wao kwa madai kuwa wanashirikiana na wenye mgodi.
Anatoa mfano wa GGM walipofunga njia waliyokuwa wanapita wananchi kwenda mjini Geita na kuwaelekeza njia mpya wanakotumia kati ya saa tano na saa sita kufika mjini badala ya saa moja ya awali.
“Hapa kijijini tunaishi kwa mashaka, nyumba zetu zimepasuka kutokana na milipuko ya baruti. Mimi mwenywe ng’ombe wangu 19 wamekufa baada ya kunywa maji ya mto ambamo yaliingia maji yenye sumu iliyotiririka kutoka mgodini,” anaeleza mzee Lufungulo.
Anasema wakati wa kiangazi bwawa lenye maji ya sumu hufuka moshi ambao hutanda kijijini na wananchi kuvuta hewa chafu.
Kwa mujibu wa mtaalam wa mambo ya madini na miamba mjini Geita, sumu inayotiririkia kwenye mito na visima inaitwa Cyanide iliyosheheni kemikali mchanganyiko.
Anasema kemikali hizo zinafanana na acid kwani zinaunguza hadi kwenye mfupa, pale tone hai linapoangukia mwilini.
Akionyesha ukali na ubaya wa kemikali hiyo, mtaalam huyo amesema hata wamiliki wa GGM wanalinda bwawa la majitaka hayo ili hata ndege wasinywe maji hapo ingawa imethibitika kuwa yanatiririkia mtoni.
Amesema ndege akinywa maji kwenye bwawa atakufa na ndege mwingiune au mnyama atakayekula mzoga wake atakufa.
“Hii ndiyo balaa inayotukumba kwa kuishi karibu na mgodi. Wageni wanachuma mali sisi tunachuma maradhi na vifo,” anasema mzee Kasoboke Maselle.
Wakazi wapatao 270 ni miongoni mwa walioswagwa kutoka maeneo yao ya asili ili kupisha eneo la mgodi. Kuna waliolipwa na ambao hawakulipwa. Malalamiko yanaendelea lakini ufumbuzi hauonekani.
Mwandishi: Lakini huoni sababu nzuri ya kuishi karibu na mgodi?
Maselle: Nimefaidika na ninaendelea kufaidika. Huoni miguu yangu ilivyo? Ni mafanikio ya kuwepo kwenye maeneo haya.
Mwandishi: Faida ipi?
Maselle: Angalia miguu yangu…
Binti Ashura Maselle: Anakuonyesha miguu iliyoharibika kutokana na kukanyaga maji ya sumu yanayotiririka kutoka kwenye bwawa la mgodi.
Wasiofaidika na dhahabu iliyo karibu na makazi yao ni pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi ya Mgusu. Mwandishi alikuta darasa la nne wakisomea mchangani chini ya mti.
Siyo rahisi kuamini kuwa shule ya msingi ya Mgusu iko chini ya milima inayotoa dhahabu. Shule yenye wanafunzi 1,204 katika madarasa saba, ina vyumba vinne tu vya kusomea.
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Selelii Magida anasema shule yao inatakiwa kuwa na mikondo 30 kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo; lakini kutokana na uhaba wa madarasa, watoto wanakaa mpaka 200 kwenye darasa moja.
Hata vyumba vinne vinavyoitwa madarasa havina madawati. Wanafunzi wanakaa kwenye sakafu iliyopasuka. Moja ya madarasa hayo linatumika kama chumba cha walimu ambamo wanakalia madawati badala ya viti na meza.
Shule iliyopo barazani mwa mgodi wa dhahabu na walimu na wanafunzi, wakati wote wananusa harufu ya dhahabu, haina chaki, vitabu vya kiada na ziada wala mbao za kuandikia.
Shule ya Mgusu ina walimu 11 na nyumba moja ya walimu ambayo kuta zake zimejaa nyufa. Walimu wengi wamepanga nyumba mjini Geita, umbali wa kilometa 28. Wanafika shule kwa kutumia usafiri wa baiskeli za kukodi.
Pamoja na mazingira magumu ya kusoma na kufundisha yanayowapata walimu na wanafunzi wa shule hiyo, lakini imepeleka kidato cha kwanza wanafunzi 72 kati ya wanafunzi 114 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana.
Hata hivyo, diwani wa kata ya Mtakuja, Suzana Mashala anasema GGM hawana msaada kwa vijiji. Amesema vikiomba msaada wenye mgodi wanasema siyo kazi yao kusaidia vijiji. Wanadai wanatoa msaada kwa halmashauri tu.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Geita, Elias Chasama, anasema wanachopata kutoka GGM ni Sh. 250 milioni tu kwa mwaka zinazotokana na kodi ya halmashauri.
Tangu mgodi huo uanze kufanya kazi zaidi ya miaka kumi iliyopita, umejenga wodi ya wazazi na visima viwili kwa wanakijiji cha Mpovu ambao waliathirika kutokana na maji ya sumu yanayotoka mgodini.
Chasama amesema halmashauri waliiomba GGM kujenga shule ya sekondari ya wasichana, lakini tangu ianze kujengwa ni miaka saba sasa na haijakamilika.
Kwa ujumla, mazingira na maisha kwa wakazi wa maeneo kuzunguka GGM, ni magumu, ya hatari na yanayoweza kuelezwa kuwa balaa kubwa kuliko baraka.
Kaimu mtendaji wa kijiji cha Mgusu, Diackar Balele, anasema kuishi kwenye maeneo ya dhahabu ni “nuksi na hakuna faida yoyote. Huu mgodi tumeomba utujengee zahanati haukujenga. Tumeomba utuchimbie kisima haukuchimba.”
Anasema hata walipowaomba wasaidie kufunika kisima wanachochota maji kutokana na athari za baruti wanazolipua, “hakuna majibu tuliyoyapata. Sasa kuna faida gani kuwa majirani wa wasioitika matakwa yetu.”