Dhambi ya ubaguzi yamtafuna Kikwete


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kilianzisha mradi mchafu kilipobaini uwezekano wa kusombwa na kimbunga cha mageuzi na kukataliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 1995.

Kilitafuta wataalam wa propaganda wabuni mahali pa kujishika. Wataalam hao wakabuni mradi wa hofu. Wakaeneza uzushi eti vyama vingi husababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

CCM ikjaza watu hofu ya kupoteza maisha, kukatwa viungo, kupoteza ndugu na jamaa kwa vita iwapo watachagua upinzani. Eti upinzani utaua watu kama ilivyotokea Rwanda, Burundi, Sudan na Somalia.

Vyombo vya habari, hasa vya elektroniki vikasambaza hofu hiyo kwa kuonyesha picha za mauaji ya Rwanda; vikahujumu ustawi wa mfumo wa vyama vingi.

Kwa kuwa, wakati vinaanzishwa vyama vingi, watu wengi hawakuwa na uelewa (wengine hadi leo) juu ya mfumo huo, wakalaani walioanzisha vyama vipya vya siasa badala ya CCM. Hawakujua vilianzishwa kikatiba.

Dhambi hii imewarudia wao. Wanatafuta pa kujishika, hawaoni. Sasa ni malumbano, chuki, minyukano. Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete amefungwa minyororo ya hofu. Kila analosema, hukosolewa vikali na kila analopendekeza, wenzake humbeza.

Rais Kikwete amebaki mpweke, ananyooshewa kidole, ananuniwa, anakasirikiwa, anakosolewa, analaumiwa, na anahofiwa ndani na nje ya CCM kama mwenyekiti na kama rais. Taifa zima lina hofu.

Kosa la Rais Kikwete ni kutaka kufurahisha kila kundi. Ilipoibuka kashfa ya ufisadi, Rais aliwatetea kwa nguvu watuhumiwa kwa kuwa walikuwa maswahiba na wasaidizi wake wakuu. Vilevile aliwasifu wapambanaji wa ufisadi.

Unafiki huu umekidharaulisha chama na umedhalilisha mamlaka ya urais kwa kudhoofisha vita dhidi ya ufisadi. Kitendo hicho ni sawa na kuwapa tuzo watuhumiwa ufisadi na zawadi wapambanaji.

Unafiki kama huu ulifanywa na lililokuwa Shirikisho la Soviet wakati wa vita vya kumng’oa nduli Iddi Amin wa Uganda. Soviet iliipa Uganda ndege za kivita, lakini shirikisho hilo, lililodaiwa kuwa na silaha kali hata kuzidi Marekani, liliiuzia Tanzania makombora ya kutungulia ndege za Uganda.

Inadaiwa (sina uhakika) baada ya vita kumalizika Soviet iliipa Tanzania tuzo ya dola milioni moja kwa matumizi mazuri ya makombora yake!

Nani atampa tuzo Rais kwa kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi na wapambanaji? Nani atamsifu Rais kwa kuacha kutumia taasisi za kiserikali kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) badala yake akamteua Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa kuwahoji watuhumiwa ufisadi?

Kama Rais Kikwete alipatanisha watuhumiwa ufisadi na wapambanaji kupitia kamati ya rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, anatakaje watuhumiwa wajivue magamba? Ni nini msingi wa kutaka watu waliopatanishwa wajivue magamba? Aliogopa nini kuwavua magamba wakati ule na kuwafungulia kesi?

Kwa uelewa wangu, ufisadi uliofanywa na Mapacha Watatu wa ufisadi ni uhujumu uchumi wa nchi, siyo CCM. Kwanini hataki kuruhusu mamlaka za kisheria – Polisi na TAKUKURU – ziwahoji na kuwashitaki?

Kwanini anabagua? Alibagua wezi wa EPA, baadhi yao walifunguliwa kesi na kufungwa huku akiacha wengine. Ni utawala bora gani huu wa ubaguzi? Kwanini sheria inabagua wananchi?

Mbona Basil Mramba, Gray Mgonja na Daniel Yona hawakuambiwa wajivue magamba kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka yaliyofisidi nchi sawa na yaliyofanywa na Mapacha Watatu?

Alipewa orodha ya wauzaji dawa za kulevya nchini, hakuitumia. Matokeo yake ameingia katika malumbano na maaskofu wakidai amewasingizia kwani hata ikulu wapo.

Kama kikosi cha kuzuia madawa ya kulevya kimenasa maaskofu wauza unga, amewaacha wa nini wahalifu hao wanaowapoteza kondoo wa Mungu? Anataka nao wakahojiwe na Msekwa?

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: