DIWANI YUSUPH: Napigania elimu, afya na ulinzi


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

KUTANA na Yusuph Fungameza (44), diwani wa kata ya Uyovu, wilaya ya Bukombe mkoani Shinyanga.

Kata yake ndiyo inatajwa kuongoza katika maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na katika ujambazi wa kutumia silaha.

“Nimeamua kupigania mabadiliko katika mambo matatu makuu: Elimu, Afya na Ulinzi,” anasema Fungazeza ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la kwanza, Yusuph.

Anasema mapema, katika mahojiano yake na MwanaHALISI, “Elimu itaongeza uelewa na maarifa na wananchi watatumia elimu hiyo katika kupambana na VVU na ujambazi.”

Yusuph ni diwani kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Diwani aliulizwa amefanya nini katika siku 100 za uongozi wake na nini anatarajia kufanya baadaye.

“Tumeanza kwa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa ulinzi. Wameelewa haraka. Sasa ndio tumeanza kukabiliana na suala la usalama. Unajua, kuna vitendo vingi vya ujambazi na mauaji,” anaeleza Yusuph.

Anasema, “Kituo chetu cha polisi hakina hata baiskeli. Nimeomba gari kwa RPC (mkuu wa polisi wa mkoa). Amekubali lakini amesema ni bovu; mpaka alitengeneze. Zinahitajika Sh. 3,000,000 (milioni tatu tu).”

Yusuph anasema, “Aliponieleza hivyo, niliona tunaweza kuchelewa kulipata. Nikawaita wakazi na wafanyabiashara wa eneo langu. Nikawaeleza. Wakakubali kuchanga fedha kwa ajili ya matengenezo yote.”

Anasema wananchi wameahidi pia kuchangia lita mia nne (400) za petroli kwa ajili ya kuanzia kazi.

Kwa mujibu wa Yusuph, RPC ameonyesha ushirikiano katika kuimarisha ulinzi na kwamba tayari uongozi wake wa kata, kwa kushirikiana na wananchi na polisi, wameweka mikakati ya kudhibiti uhalifu.

Kijiji cha Runzewe ambacho ndiko yaliko makao makuu ya kata ya Uyovu ndicho kinachoongoza kwa uhalifu wa kutumia silaha.

Diwani Yusuph anasema silaha nyingi zinazokamatwa katika eneo lake, kwa mujibu wa jeshi la polisi, ni za kivita na nyingi zinatoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Burundi na Rwanda.

Runzewe ndio kituo kikuu cha magari yaendayo Burundi, Rwanda, Congo, Kigoma, Ngara na sehemu nyingine. Hapa pia kuna mkusanyiko mkubwa wa wachimba madini wadogo na wanunuzi.

Yusuph anataja mwingiliano usioratibiwa rasmi wa raia wa nchi jirani – Burundi, Rwanda, Congo na Uganda, kuwa moja ya vyanzo vya uhalifu.

Hata hivyo, anasema kwa juhudi za sasa za ulinzi shirikishi, ujambazi unaweza kukabiliwa.

Kuhusu afya, diwani Yusuph anasema  Runzewe ndipo panaongoza kwa kasi ya maambuzi ya VVU mkoani Shinyanga. Kijijini hapo, maambukizi yanatajwa kuwa juu kwa asilimia saba (7%).

Katika kijiji cha Runzewe kuna wasichana wengi waliochini ya miaka 20 waliotoka mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Tabora, Mwanza, Kagera pamoja na mikoa na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Congo.

Wengi wao “wanafanya kazi” katika migahawa na maduka ya kuuza bia na bidhaa nyingine (grocery).

Msichana mmoja kutoka Rwanda, aliyesema ana umri wa miaka 26, alimwambia mwandishi wa makala hii kuwa yeye na wenzake wengi, “tumefuata wauza madini wenye fedha nyingi.”

Binti huyu alikutana na mwandishi katika duka la pombe maarufu kwa jina la Stop Over.

Ni Runzewe ambako kuna mashindano ya ngono kati ya wasichana wadogo waliopachikwa jina la “sungura wachafu,” na wale wa umri wa zaidi ya miaka 20.

Diwani Yusuph anakiri eneo lake kukumbwa na biashara ya ngono na isiyo salama. Anasema njia kuu wanayotaka kutumia ili kupunguza maambukizi ya VVU ni kutoa elimu ya afya kwa jumla; na kusisitiza kinga katika mahusiano ya ngono.

Njia nyingine ni kuzuia kupeleka kijijini pale wasichana wa umri mdogo kwa nia ya kuwatumikisha katika ngono za kulipwa.

Aidha, anasema kutakuwa na utaratibu wa kutambua wakazi halali wa kijiji, wageni wanaoingia, kule watokako na shughuli zao kijijini.

Mikakati ya diwani huyu ni pamoja na kufuatilia kupatikana kwa walimu wa kutosha, madawati, vitabu na vifaa vingine vya kufundishia mashuleni.

Yusuph, mwenye elimu ya sekondari, ana mke na watoto watano.

0784 447077 unclejay_jongo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: