Dk. Kitine: Mtandao wa JK umeivuruga nchi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
DK. Hassy Kitine, mkurugenzi mstaafu wa usalama wa taifa

DK. Hassy Kitine, kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibuka na kutema nyongo. Anasema kuzorota kwa chama chake kisiasa hadi kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita, kumesababishwa na viongozi wake kuacha misingi yake ya asili.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki iliyopita nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Dk. Kitine anasema kudhoofika kwa CCM kumeletwa na kushindwa kusimamia maadili.

Amesema, “Kudhoofika kwa CCM kisiasa; kupotea kwa mwelekeo wake na kupotea kasi na umaarufu wa chama hiki, kwa kiwango kikubwa kumechangiwa na hatua ya baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia miiko ya uongozi na maadili ya chama chetu.”

Anasema kama chama chake kinataka kurejesha heshima yake kiliyokuwanayo huko nyuma, sharti kijitazame upya na kijirerejeshe kwa wanachama wake. Viongozi wake ni lazima waachane na tabia ya kukumbatia wenye fedha, jambo linalokidhalilisha chama kwa kuonekana mbele ya umma kuwa ni chama cha wenye fedha.

Anasema viongozi waliopewa dhamana waangalie sana uteuzi wa viongozi katika nafasi za ubunge na udiwani, ambako ndiko malalamiko yanaanzia.

“Leo ndani ya CCM, uongozi unanunuliwa…Rushwa ndiyo msingi wa mtu kuchaguliwa. Tukitoe chama chetu huko,” anaeleza kwa sauti ya unyonge.

Kingine ambacho Dk. Kitine anasema kimechangia kuzorota kwa chama chake, ni kile alichoita, “Mbegu chafu ya wanamtandao.”

Kundi hilo lililoundwa mara baada ya kumalizika kinyang’anyoro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, lilifanya kazi kubwa ya kuchafua wanachama na viongozi wa chama hicho waliojitokeza kusaka urais.

Anasema kundi la mtandao lililoundwa maalum kwa ajili ya kumuingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete, nalo lazima libebe lawama kwa kuchangia kukivuruga chama chake.

Kwanza, kwa hatua yake ya kumchafua kila aliyeonekana tishio katika kinyanganyiro cha urais mwaka 2005. Lakini pili ni kutokuwapo mipango thabiti ya kutekeleza pindi mpango wa kuingia ikulu utakapofanikiwa.

Dk. Kitine ambaye aliwahi kuwa waziri wa utawala bora wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, mkurugenzi wa usalama wa taifa, mbunge na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, anasema viongozi wa mtandao waliaminisha kila mmoja kuwa Kikwete ndiyo mwisho wa matatizo ya wananchi, jambo ambalo lilisababisha wananchi wengi kumuamini.

Anasema, “Mtandao uliofanya kazi ya kumuingiza Rais Kikwete madarakani hauwezi kuachwa katika hili la kudhoofika kwa chama chetu. Ni kwa kuwa mtandao ulifanya kazi ya kutafuta ikulu kwa udi na uvumba, lakini ukiwa haujui ukifika ikulu utafanyia nini wananchi.”

Dk. Kitine anataja waliochafuliwa kwa kutaka urais kuwa ni pamoja na mwanadiplomasia anayeheshimika duniani, Dk. Salim Ahmed Salim ambaye wanamtandao walimzushia kuhusika na mauaji ya rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume na ujio wa chama cha Hizbu.

Anasema, “Haya yote yamejenga ufa mkubwa ndani ya chama na yamechangia kukidhoofisha chama chetu. Si jambo jema kumtungia mtu tuhuma za uwongo kwa sababu ya urais.”

Anasema hata tuhuma dhidi yake kuhusiana na matibabu ya mkewe nje ya nchi, zililenga mbio za urais mwaka 2005.

“Hata mimi nilichafuliwa katika mazingira hayohayo. Nikiwa waziri wa kwanza wa utawala bora nchini baada ya kuundwa kwa wizara hiyo mwaka 1997, nilidhaniwa nitagombea urais au nitakuwa na ushawishi kwa mmoja wa wagombea. Wakaamua kunisakama hadi nikaondoka,” anasema Dk. Kitine huku akishusha pumzi.

Akiongea kwa kujiamini, Dk. Kitine anasema alipokuwa ikulu aliweka utaratibu wa watu wachafu kutomkaribia rais au ikulu kugeuzwa kijiwe cha soga, jambo ambalo liliwaudhi wengi.

Anasema, “Sasa kuona hivyo, wale waliokuwa wanataka kugeuza ikulu kijiwe cha soga wakaungana na wale waliokuwa wanatafuta urais na kuanza kunisakama; katika mambo yanayohusu nchi, hakuna anayemuogopa.”

Alipoulizwa kwa nini anadhani hatua yake ilimsababishia kusakamwa na wetu wengi, wakiwamo hasa wale aliodai kuwa walikuwa wanautafuta urais, Dk Kitine aliishia kujibu, “…Inatosha kusema yale yamepita na nimeshasamehe.”

Mwaka 1997 mara baada ya kushinda kiti cha ubunge katika jimbo la Makete, rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa alimteua Dk. Kitine kuwa waziri wa utawala bora, jambo ambalo lilizusha minong’ono mingi kuwa anaweza kuwa miongoni mwa watakagombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Wizara hii iliundwa mara baada ya rais Mkapa kupokea ripoti ya tume ya Jaji Joseph Warioba ambayo sehemu kubwa ya mapendekezo yake yalilenga udhibiti wa mianya ya rushwa serikalini.

Uchaguzi mdogo wa Makete ulikuja kufuatia kifo cha Tumtemeke Sanga ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo. Wakati Dk. Kitine anagombea ubunge wa Makete alikuwa mkuu wa mkoa wa Tanga.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Dk. Kitine alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Iringa Mjini. Ingawa alipenya katika kinyang’anyiro cha kura za maoni kwa kuwamwaga washindani wenzake zaidi ya 10, lakini alipoingia katika ushindani na wagombea wa vyama vingine vya siasa, Dk. Kitine alishindwa na mgombea wa chama cha NCCR-Mageuzi, Kibaasa.

Hata hivyo, mwenyewe anasema kushindwa kwake katika kiti cha ubunge Iringa Mjini kulitokana na anachokiita “fitina za kisiasa.” Anasema fitina hizo zilijikita katika ukabila na udini. Ziliibuliwa na washindani wake ndani ya chama chake.

Kitine alizungumzia pia hatua ya CCM kutaka kuwachukulia hatua watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini – Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Anasema chama chake kitafute ushahidi wa kutosha na kisha kiwape nafasi wanaotuhumiwa kujitetea, kisha ikithibitika kuwa wametenda makosa wanayotuhumiwa waondolewe moja kwa moja kwenye chama.

Hatua kama hizo zichukuliwe pia kwa wale wanaotuhimiwa kuanzisha Chama cha Jamii (CCJ) wakati wakiwa bado wanachama wa CCM.

Wanaotuhumiwa kuanzisha chama ndani ya chama, ni pamoja na Samwel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Nape Nnauye na Victor Mwambalaswa.

“Hili la hawa walioanzisha chama ndani ya chama na wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ni lazima chama chetu kitafute ushahidi wa kutosha na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika kufuatana na katiba na taratibu za chama,” ameeleza.

Anasema kuanzisha chama ukiwa bado ndani ya chama ni kosa ambalo haliwezi kuachwa bila kutolewa maelezo.

“CCM kisifanye parapara. Pamoja na kwamba kumfukuza mtu ndani ya chama ni hatua kubwa, lakini utafutwe ushahidi; ikithibitika kwamba hawa watu walishiriki katika kuazishwa kwa chama wakiwa bado ndani ya CCM, basi wawajibishwe,” ameeleza.

Anasema, “Ushahidi huu lazima ueleze ushiriki wa kila mmoja. Ukipatikana wote wafukuzwe.”

Akizungumzia matatizo yaliyopo katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dk. Kitine anasema wakati umefika wa mataifa hayo mawili kila mmoja kujiamulia mambo yake.

“Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliniambia muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda Uingereza, ‘…nadhani sasa wakati umefika kwa Zanzibar kuachwa kujiamulia mambo yake,’” anaeleza Dk. Kitine akimnukuu Nyerere.

Anasema, “Mwalimu alifikia hatua hiyo baada ya kuona Zanzibar kila siku hawaishi malalamiko. Nami naona sasa wakati umefika wa Zanzibar kutengana na Bara. Tufungue mjadala, wananchi wajadili suala hili na wakiona kuwa Muungano uvunjike, basi tufanye hivyo kwa amani na utulivu.”

Anasema hilo ni muhimu kuliko kusubiri nchi kuingia katika machafuko. “Tujadili kwa uwazi jambo hili. Kama tutavunjika tuwe na utaratibu wa undugu kushirikiana. Kuogopa tatizo hili, kunaweza kutuingiza katika matatizo mengi makubwa huko mbele.”

Anasema, “Tufike mahali tuamue kama tunataka Muungano, basi uwepo. Kama hatuutaki, basi tuachane nao kwa salama na kisha tutafute njia ya kuishi kwa umoja na amani kama ndugu,” anaeleza.

Anasema katika kufikia suluhu ya malalamiko ya Muungano, serikali iruhusu kuitishwa kwa kura ya maoni na kila upande wa Muungano uruhusiwe kupiga kura yake.

0
Your rating: None Average: 4.5 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: