Dk. Kiula apania kumng’oa Chiligati

KATIKA himaya yoyote, hakuna ambapo mfalme, kwa mila na desturi, anaweza kurithisha vijana wake ufalme wakati yeye bado yu hai.
Bali ikitokea hivyo, inawezekana basi mfalme aliyepo amezeeka sana na anashindwa kutekeleza majukumu yake; au ana hofu kwamba asipofanya hivyo, watoto wake wanaweza kupigana na hata kuuana; kila mmoja akitaka kurithi.
Hata hivyo, katika enzi hizi za demokrasia, vijana wanaweza kuonyesha nia ya kutaka kurithi ufalme wakati mfalme bado yupo.
Hivyo ndivyo inatokea katika majimbo mengi ya ubunge, ambapo vijana hutangaza nia ya kuwania ubunge wakati ‘wenye majimbo’ hayo bado wapo na wanataka kuendelea.
Mbunge (mfalme) wa Jimbo la Manyoni Mashariki ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, John Chiligati anataka kuendelea kuwa mwakilishi wa eneo hilo, lakini “vijana” wanane wameamua kupandisha joto lake.
Sababu kubwa ni uwakilishi usioridhisha. Katika vikao vichache kabisa alivyowahi kufanya katika eneo lake la uwakilishi, Chiligati amekuwa akikiri, “Jamani naomba mnisamehe nina ndoa ya wake wawili.”
Ndoa anazozungumzia ni madaraka aliyopewa ndani ya serikali na chama kwa upande mmoja na uwakilishi wa wananchi, kwa upande mwingine.
Anawataka wananchi wasilalamike au wasinung’unike pale anaposhindwa kufika kusikiliza shida zao kwa kuwa majukumu ya kiserikali yanamlia muda mwingi kuliko uwakilishi.
Majukumu mengi ya kiserikali yanayomkabili; na ukweli kwamba mbunge huyo hapati muda wa kutosha wa kufanya mikutano ya hadhara na wananchi hadi wakati wa kuomba kura tena, Manyoni Mashariki wanaandaa watu wengine wa kuwakilisha jimbo hilo.
Presha itakuwa kwa Waziri Chiligati kupanga mikakati ya ushindi. Waliotangaza nia ya kumg’oa hawana cha kupoteza ikiwa watashindwa.
Na kutokana na upinzani kuchechemea katika jimbo hilo, ni wazi atakayepitishwa na vikao vya CCM, ndiye atakuwa mbunge. Lakini chama hicho kikikataa chaguo la wananchi, huo waweza kuwa mwanzo wa kujengeka upinzani katika jimbo hilo.
Miongoni mwa watu wanane waliotangaza nia ya kumwondoa au kupambana na Chiligati katika nafasi hiyo kupitia CCM, yumo Dk. Edwin Joseph Kiula aliyeko makao makuu ya Dayosisi ya Bonde la Ufa, Kanisa Anglikana, Manyoni.
Wengine ni Edwin Pius ambaye ni mwalimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Salesi Mahula anayefanya kazi katika shirika la kidini.
Wengine ambao hadi tunakwenda mitamboni walikuwa wakitajwa kwa jina mojamoja, ni Agaitani ambaye ni mwalimu wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Nyambwa ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Dk. Kiula ambaye amefanya kazi ya kutibu watu kwa takriban miaka 30 sasa, anasema anataka kutoa mchango wake kwa maendeleo ya wananchi kiafya, kielimu na kiuchumi.
“Nimezaliwa Manyoni, nimekulia Manyoni, nimeishi tarafa zote kama mwanafunzi na kama mfanyakazi nikitoa huduma ya tiba kwa takriban miaka 30 sasa; hivyo nazijua shida za wananchi,” anasema Dk. Kiula.
Dk. Kiula anadhani anaweza kuwa mbadala wa Chiligati ambaye amebanwa na majukumu ya kiserikali na chama kiasi cha kushindwa kukutana na wananchi wake.
Jimboni kwake wapigakura wanamuona Chiligati kuwa amezidiwa na vyeo ndiyo maana hawafikii kutatua kero zao na kupata mawazo mapya ya kupeleka bungeni au serikalini.
Japokuwa kuna raslimali kadha wa kadhaa, wilaya ya Manyoni imekuwa masikini zaidi kimkoa na mkoa wa Singida ndio masikini zaidi nchini.
Singida kwa ujumla imeshindwa kutumia raslimali zilizopo na maeneo tengefu ya wanyama kama vile Rungwa, Muhesi na Kizigo ili kuwaendeleza wananchi.
Tatizo kubwa ni barabara za kufika kwenye maeneo hayo na wawindaji wanaofika ni wale wanaotumia usafiri wa anga. Hawa hutua porini, huwinda na kuondoka bila hata kulipa kitu kwenye vijiji vya jirani na maeneo hayo.
Katika Manyoni yenye ardhi inayofaa kwa kilimo, ina matrekta yasiyozidi 10 na wakulima wengi bado wanategemea jembe la mkono.
Raslimali nyingine ambayo ni hazina kwa wananchi wa Manyoni na taifa kwa jumla ni hazina ya madini katika maeneo ya Londoni, Mafurungu na Sasilo.
Vilevile Manyoni kuna madini ya uranium kwa ajili ya nishati na kutengenezea mabomu ya nyukilia.
Dk. Kiula anasema kuna mambo mengi zaidi ambayo atashughulikia. “Kwanza ni ajira kwa vijana wengi wasio na kazi. Nitajitahidi kuwahamasisha wajiajiri.,” anasema.
Anasema, “Vijana waliambiwa wajiunge kwenye vikundi ili wapate mikopo kutokana na mabilioni ya shilingi yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete. Vijana kweli walijiunga, lakini kutokana na kuachwa bila kupewa mbinu za kupata mikopo ile, walikosa,” anasisitiza.
Changamoto nyingine ambazo amesema atasimamia kikamilifu ni upatikanaji wa maji safi na ya uhakika; ujenzi wa shule na kwa ufanisi mkubwa upatikanaji wa huduma za afya.
“Kwa mfano kijiji cha Senza; mgonjwa anayehitaji huduma za hospitali baada ya zahanati kushindwa, inampasa atembee umbali wa kilomita 70 kwenda ama Manyoni au Kilimatinde au Dodoma mjini,” anasema.
Kwa watu wasiomfahamu, Dk. Kiula ndiye aliyefufua utoaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto kwa kutumia gari na ndege – huduma ya dharura ya gari na ndege iliyoitwa Mission Aviation Fellowship-MAF.
Kadhalika, baada ya kuguswa na matokeo mabaya ya mitihani ya darasa la saba katika vipindi viwili tofauti – mwaka 2006 na 2008 – kwenye kata za Solya, Sukamahela na Kilimatindi, aliandaa kambi ya maandalizi na matokeo yakawa mazuri.
Kuhusu mchango wake katika CCM, anasema, “…Viongozi wangu wanaujua.”
Pengine suala tete ambalo linaweza kuwa kete ya Dk. Kiula ni kuhusu hatima ya wakazi wanaoishi kwenye maeneo ambayo yamepatikana na machimbo ya madini ya uranium.
Ukanda mzima wa Bonde la Ufa unaounganisha vijiji hadi Bonde la Bahi wilaya ya Bahi mkoani Dodoma umegundulika kuwa na hazina ya madini hayo.
Tayari kampuni ya Uranex kutoka Australia imepewa kazi ya kuchimba wakati wowote kuanzia mwaka ujao. Serikali imekamilisha mkataba na kampuni hiyo wakati wananchi hawajui hatima yao.
Dk. Kiula anasema akichaguliwa atahakikisha wananchi wanalipwa fidia halali kwa makazi na mali zao kama vile mifugo, viwanja na mashamba.
“Vilevile nitapigania wananchi wanufaike na madini hayo yakianza kuchimbwa,” anasema.