Dk. Ndugulile: Serikali yetu itajuta

MAMBO mawili yanamkereketa Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile. La kwanza ni kupandishwa kwa nauli za kivuko cha Kigamboni; na pili ni mradi wa mji mpya wa Kigamboni.
Akiwa na mwaka mmoja tu bungeni, Dk. Ndugulile anasema anaumizwa roho kuona wananchi wanazidishiwa mzigo wa gharama za maisha bila ya serikali kuwa wazi katika namna inavyoendesha mambo.
Anasema tatizo ni kuwa serikali inajenga utamaduni wa kutoa majibu mepesi na wakati mwingine ya kejeli na kiburi dhidi ya mambo yanayogusa maisha ya watu.
Dk. Ndugulile anatahadharisha serikali: “Kama serikali haitakuwa makini kushirikisha wananchi katika mipango yake ijue ni sawa na kujichimbia kaburi. Ipo siku itajuta.”
Anapotoa hoja ya “majibu mepesi, ya kejeli na kiburi” analenga kauli iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwamba nauli mpya za kivuko cha Kigamboni zitaendelea na wasioweza wapige mbizi.”
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wabunge wa Dar es Salaam kulalamika kuwa hawakushirikishwa katika upandishaji nauli za kivuko hicho.
Mbunge wa Kigamboni anasema amefuatilia tatizo la kivuko kwa mara tu alipochaguliwa mbunge Oktoba 2010.
“Barua yangu ya kwanza kuiandikia serikali baada ya kuchaguliwa ilikuwa ya 19 Januari, 2011 niliyopeleka Wizara ya Ujenzi. Nilitoa taarifa za ongezeko la watu Kigamboni, nikatoa malalamiko yetu ya foleni pale kivukoni na mfumo wa uendeshaji kivuko,” anasema.
Anasema hajajibiwa barua zake. Sasa anasikitika kuwa hata yeye mbunge anashtukia nauli mpya kupitia tangazo la serikali kwenye vyombo vya habari.
Dk. Ndugulile anahoji mbona hesabu za mapato ya kivuko hazijawahi kuwekwa wazi ili “gharama za uendeshaji zijulikane. Kwamba nauli zilizopo ni za muda mrefu ni kisingizio dhaifu… tunasema kabla ya kupandisha wangeeleza wanadhibiti vipi mapato.”
“Tunaamini kuna mapato mengi yanavuja. Zipo taarifa za wafanyakazi kutumia vitabu tofauti katika kutoa stakabadhi. Unapandishaje nauli bila ya kuangalia matatizo haya,” anashangaa.
“Taarifa zetu za uchunguzi zinasema wakifanya vizuri wanakusanya hadi (Sh.) 13 milioni kutoka 8 milioni hadi 9 milioni. Lakini mapato yanavuja hapa,” anasema.
Anasema “Tumeelezwa kuwa mfanyakazi huondoka na hadi Sh. 500,000 kwa siku na zikipungua basi anapata Sh. 300,000… ni fedha nyingi.”
“Haya hawataki tuyaeleze bayana. Hata barua yangu ya Ijumaa tarehe 6 Januari, 2012) sijajibiwa. Naona watendaji wa serikali wamelala,” anasema Dk. Ndugulile.
Barua nyingine anasema ni ya 3 Januari 2012 aliyomtumia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Unajua wakazi wa Kigamboni si wote wanatoka maeneo ya karibu. Kuna wanaotoka Kimbiji, Kisarawe2, Kibada, Mji Mwema na kwengineko. Kabla ya kufika kivukoni, huwa wamelipa nauli kwenye magari au kutumia mafuta kwa kiasi kikubwa kwa wale wenye usafiri,” anasema.
Dk. Ndugulile anasema kwamba pamoja na serikali kutamba kuongeza makusanyo ya kivuko baada ya kupandisha nauli, “idadi ya wasafiri na magari vimepungua.”
Anakiri amewasihi wananchi kutulia. Lakini, anaiona aibu ya wazi inayomkumba pamoja na wabunge wenzake wa Dar es Salaam katika suala hilo.
“Namna tunavyotofautiana na serikali ya chama chetu CCM inasikitisha. Hali hii haileti sura nzuri lakini ndio ukweli wa mambo,” anasema huku akihofia hali kama hiyo inawapa nguvu wapinzani wao kisiasa.
Kuhusu mpango wa mji mpya wa Kigamboni, Dk. Ndugulile anasema wazo la serikali ni zuri lakini mradi huo umechukua muda mrefu mno wakati shughuli za wananchi zimesimama.
Anasema serikali baada ya kutangaza mpango huo tarehe 4 Oktoba 2008, iliagiza wakazi wa kata sita kati ya 17 zilizoko Kigamboni, wasitishe uendelezaji wa maeneo yao.
Kata zilizojumuishwa katika mpango huo ni Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Kibada, Mji Mwema na Somangila.
Anasema kusitisha mipango ya wakazi wa kata hizo kwa muda wote huo ni kuwadhoofisha kiuchumi.
Hata wakati huu ambapo serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango huo, anasema utakwama kwa sababu kuna upungufu mkubwa katika usimamizi wa sheria za mipango miji na hakuna uwazi.
“Nakwambia wananchi wamekubali kwa shingo upande amri ya serikali. Hawajui mradi unaanza lini na unaanzia wapi? Haieleweki hasa stahili za Wanakigamboni ni zipi? Watazipataje stahili hizo. Haya ni mambo hayajaelezwa vizuri na wananchi hawajashirikishwa ipasavyo,” anasema.
Anaitaja sababu ya pili ya uwezekano wa mradi huo kukwama kuwa ni bajeti. Mradi umepangwa kugharimu Sh. 15 trilioni wakati bajeti ya serikali kwa mwaka ni 13.5 trilioni.
Serikali haijaeleza wapi itapata fedha za kutekeleza mradi huo, anasema.
Dk. Ndugulile anasema kwa sasa amakabiliwa na kazi ngumu ya kutuliza wananchi ambao wanalalamika kutoshirikishwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande mwingine, anasema amepiga hatua katika kuimarisha miundombinu katika huduma ya elimu na maji, ikiwemo kujenga madarasa katika shule za msingi zilizoko kata za Mianzini na Kiponda.
Pia anasema amenunua madawati 550 na amechimba visima vitatu vya maji eneo la Kisarawe2.
Dk. Ndugulile (43) ni tabibu mwenye shahada tatu za taaluma hiyo. Shahada mbili, ya kwanza alipohitimu mwaka 1997 na ya pili (Uzamili) aliyohitimu mwaka 2000 katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS).
Shahada ya tatu (Uzamivu) aliipatia Chuo Kikuu cha West Cape, Afrika Kusini. Amebobea fani ya magonjwa ya kuambukiza.
Amewahi kufanya kazi kama mshauri katika wizara za afya za Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Burundi, Rwanda na Msumbiji.
Kadhalika ni mwakilishi wa Bara la Afrika katika masuala ya UKIMWI ambako makao makuu ya Geneva, Uswisi, lakini kwa nini aligeukia siasa na kuwa mbunge huko Kigamboni, anasema:
“Nilipenda siasa na nimesukumwa na uzalendo tu kwa nchi yangu. Ndio maana utaona siasa zangu hazitofautiani na zile za wanasiasa vijana tunaohubiri jimbo, taifa, chama na mwisho ndio masuala binafsi.”
Dk. Ndugulile ni mtoto wa ofisa ubalozi mstaafu, Gabriel Sengo na mama Martha Sengo. Alizaliwa Zimbabwe ambako baba yake alikuwa anafanya kazi katika ofisi ya ubalozi.
Faustine alipata elimu ya awali, msingi na sekondari akiwa huko Zimbabwe. Baadaye familia yake iliporejea nchini, alijiunga na sekondari ya Tambaza kukamilisha kidato cha sita alikohitimu mwaka 1988.