Dk. Ng'wandu: Utumishi uliotukuka


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 19 March 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

NANI mwalimu kuliko yule aliyefundisha Shule ya Msingi, Sekondari na Chuo Kikuu kwa nyakati tofauti?

Nani mwakilishi wa wananchi kuliko yule aliyewakilisha jimbo la uchaguzi kama mbunge na jumuia ya kimataifa kama mtaalam?

Kwa miaka 35 Dk. Pius Yasebasi Ng'wandu amekuwa yote hayo na bado anaonekana kuwa na nguvu ya kuendelea kutumika kama kibarua wa umma ngazi ya kimataifa.

Hapendi kutamba, lakini ndio ukweli, viongozi wengi waliopo katika siasa na utawala, wamepitia mikononi mwake.

Ana rekodi ya miaka 10 ya kufundisha na miaka 25 ya kutumikia serikali. Katika miaka hii 25, amekuwa mkuu wa mkoa, balozi, na waziri. Aidha, amekuwa mbunge wa jimbo la Maswa, mkoani Shinyanga tangu 1980 hadi 2005 alipoamua kuacha uwakilishi.

Dk. Ng'wandu anaharakisha kukueleza mambo mawili makubwa katika maisha yake yote ya utumishi. Kwanza, utumishi wa umma ni uadilifu na utii. Pili, mtumishi wa umma lazima aamue kuachia ofisi akingali na nguvu na wakati anaowatumikia bado wanampenda.
 
Anasema, mtumishi anatakiwa kutumikia watu kwa namna ambayo hao anaowatumikia watamlipa wema.

Akiongea kama anayefundisha, Ng'wandu anasema mtumishi anatakiwa kuhakikisha kuwa haki inatolewa kwa yule anayestahili.

Hili, anasema linatokea pale mtumishi anapokuwa anaamini na kusimama katika sheria na taratibu, pamoja na desturi; hasa pale inapokuwa sheria haisemi wazi nini cha kufanywa katika jambo fulani linalohitaji kuamuliwa.

Ni kwa kuzingatia hayo, anasema wananchi wa jimbo la Maswa walitaka aendelee kuwa mbunge wao, lakini aliwajibu, "?Hapana. Haiwezekani. Mtanichoka na kunichukia. Uwakilishi si ajira ya milele."

Anasema hakutaka kuondoka kwa kupigwa mawe na kwamba kiongozi, mwakilishi wa watu, anatakiwa aondoke kwa furaha, siyo kwa watu kufurahi anaondoka kwa kuwa wamemchoka.

Mwalimu huyu anaamini kwamba siasa siyo njia pekee ya mtu kuishi. Kutumikia watu kupo kwa namna nyingi; si siasa peke yake.

Dk. Ng'wandu anasema kwamba tatizo kubwa lililokwishaota ndani ya vichwa vya Watanzania wengi wanaokusudia kuwa viongozi, ni kuamini kwamba mlango wa mtu kupata maisha mazuri ni siasa tu.

"Sivyo hata kidogo. Lazima tufike mahali kama taifa, tutafute njia nyingine mbadala, tusibanane tu katika mlango wa siasa peke yake. Ipo milango mingine tunayopaswa kuitumia kujitafutia maisha mazuri," anasema.

Ana mengi ya kujenga hoja yake hii. "Kama wewe ni fundi mchundo au fundi katikaeneo jingine lolote; ukiwa mwalimu, ukiwa mtawala, utaweza kuishi vizuri iwapo taifa litakuwa linaheshimu taaluma, serikali inaheshimu uzoefu na hazina ya maarifa.

"Hapo hatutakimbilia mlango mmoja tu wa siasa kama ajira ya pekee. Ukitumia vizuri madaraka, heshima (sifa njema au hadhi) na utaalam wako, utapata heshima tu, anasema.

Anasema kwa kutumia usanii, watu wanapata heshima. "Muigizaji tu anapata heshima na umaarufu. Mchezaji mpira anapata heshima," anasema akitolea mfano kama ilivyo nchini Marekani na kwingineko.

Dk. Ng'wandu anasema mwalimu, hata mwanasiasa, anaweza kupata "utukufu" lakini hiyo ni kwa muhusika kutumia vizuri fursa zake.

"Ukitumia vibaya fursa yako, heshima yako na umaarufu wako, basi utaleta rushwa na ufisadi. Hapa ndipo baadhi yetu tunapokosea. Unapewa heshima na jamii kama kiongozi, halafu unaichezea kwa kutafuta kujinufaisha. Huwezi kufika mbali; utakwama tu maana watu watakuchoka," anasema Dk. Ng'wandu.

Kwani Dk. Ng'wandu anafahamu nini kuhusu neno hili, "ufisadi?" Anasema ni tabia ya mtu kujipatia kipato asichostahili. Na tabia hii inawapata watu wanaodhani uadilifu ni tabia inayomtia mtu ufukara.

"Ukitumikia watu kwa uadilifu, ukiwa na upendo kwa wale unaowatumikia na ukiwaona wote wanaokuja kwako na kuwahudumia kwa usawa mbele ya sheria, hupati shida. Hutampendelea mtu wala hutamnyima anayestahili haki yake."

Anasema katika utumishi wake hakudhalilisha mtu. "Sijamtendea udhalimu mtu yeyote. Sitendi ufisadi; siwezi kuitwa fisadi. Watu wanafahamu nilivyotumikia nchi na wanajua staili yangu ya kufanya kazi. Daima nimekuwa nikiitambua haki kwa anayestahili."

Baada ya kutumikia wananchi wa Maswa kwa miaka 25, Dk. N'gwandu aliamua kuacha kugombea ili aangalie maisha yake binafsi. Anashangaza kila mmoja anaposema kuwa hakujiandaa kustaafu kustaafu.

"Unajua, mtumishi hujiandai kustaafu. Hivi ndivyo ninavyoamini. Unapokuwa mtumishi unatakiwa kujishughulisha tu na kazi yako. Ukisema ah, sasa maisha yangu yatakuaje nishastaafu, ndio unapoanza kutafuta kipato kwa njia chafu. Utaishia kuwa mla rushwa na hatimaye fisadi wa hali ya juu," anasema.

Kwa hiyo ni kweli yeye hakujiandaa? Anasema hakujiandaa, bali baada ya kustaafu siasa, ndipo alipoketi na kutafakari cha kufanya.

"Tazama, nimesoma vizuri, nilifundisha ngazi zote za elimu; sikupata shida kuamua njia ya kuchukua kujenga maisha yangu. Si nina fani niliyoisomea? Unatumia hiyo kutafuta kuishi vizuri," anasema.

Dk. Ng'wandu alipata shahada ya kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki (Dar es Salaam).

Alipata Shahada ya Uzamili katika Sosholojia mwaka 1973 kutoka Chuo Kikuu cha Alberta, Canada na baadaye Shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika Elimu kwenye Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani.

Akiwa mbunge, Dk. Ng'wandu aliamua kusomea sheria na kufaulu kujinyakulia shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT).

Dk. Ng'wandu, alizaliwa 15 Julai 1943 katika kijiji cha Budekwa wilayani Maswa. Alisoma Shule ya Msingi ya Bura wilayani humo na baadaye Seminari ya Nyegezi, nje ya jiji la Mwanza kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu, Morogoro ambako alirudi kufundisha.

Pamoja na shule nyingine, alifundisha sekondari ya Tosamaganga, Chuo cha Ualimu Kleruu, Iringa; Mwalimu Mkuu Sekondari ya Mpwapwa, Dodoma, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Butimba, Mwanza na kiongozi wa elimu wizarani kwa miaka kadhaa hadi kufikia kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu.

Dk. Ng'wandu anasema amestaafu kuwakilisha jamii finyu na kwamba sasa anawakilisha jamii pana; jamii ya kimataifa.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)