Dk. Shein ‘atakufa’ na wakubwa wanaotorosha karafuu?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SAFARI hii najadili masuala mawili ninayoamini ni muhimu sana kwa mustakbali wa taifa na uchumi wetu Zanzibar – ulinzi thabiti wa karafuu na dawa mjarab ya ufisadi.

Haya yote ni masuala nyeti. Karafuu ni nguzo ya uchumi kwetu hata katika hali yake ya sasa bei kutotabirika. Na ufisadi ambao ni tatizo lililoanza kimzaha tu, leo limekuwa kubwa isivyomithilika na linaumiza mno jamii.

Ninayatizama haya kwa mnasaba mmoja mkubwa: Yanawiana katika mantiki yake kwa dhana ya maendeleo.

Yanajenga taswira ya namna serikali inavyoonyesha bayana dhamira yake katika kutokomeza ufisadi ndani ya mfumo wa utumishi wa umma.

Ndiyo maana naona kila ninapoyatafakari haya, napata picha mbili zisizokubali kutengana. Ni picha zinazoshikana na kwa karibu sana zinashikamana. Fuatilia sababu.

Kwanza, katika kampeni ninayoiita mpya na kabambe aliyoianzisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wiki tatu zilizopita alipokuwa ziarani kisiwani Pemba, alitoa viapo.

Dk. Shein aliapa serikali kulinda karafuu yote dhidi ya uovu wa kununuliwa na wajanja na kuiuza nje kwa njia ya magendo. Anataka karafuu yote ikishakauka, iuzwe ZSTC, wakala anayesimamia kuiuza kimataifa.

Katika hilo, rais akasema hakuna hata mtu mmoja ataishinda serikali yake. Hata wale wanaoitorosha hawatashinda.

Dk. Shein, rais wa serikali ya umoja wa kitaifa inayoshirikisha vyama viwili tu vilivyopata haki ya kikatiba ya kujumuika serikalini, alisema hakuna mjanja wa kukiuka mkono wa sheria akishajiingiza katika biashara hiyo haramu.

“Hata wale waliotorosha magunia 170 ya karafuu juzi tutawapata na kuwa… hakuna tutakayemkubalia kutorosha karafuu yetu halafu tumuache hivihivi.

“Tunataka tuimiliki karafuu kwa ajili ya maendeleo yenu wananchi. Hawa wezi wanajali manufaa yao tu,” aliwaambia wanakijiji wa Sijeni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, alikozindua kampeni.

Hapa Dk. Shein alikuwa anataka wananchi, hususan wakulima wa karafuu, watambue kuwa karafuu ingali zao linalotegemewa na serikali kiuchumi. Serikali inataka wauze karafuu serikalini ili mapato yasaidie kujenga nchi.

“Tunaihitaji karafuu yote (itakayovunwa) maana yake hatujaiachia huria. Hii ni dhahabu kwa nchi yetu lazima tuendelee kuitunza na kuiandalia mfumo mzuri wa uzalishaji na soko ili nanyi mpate manufaa nayo,” alisema.

Hiyo ina maana kubwa. Serikali haijaiachia karafuu kuuzwa popote na hatua hiyo ni pigo kwa wananchi waliotumaini kuruhusiwa kuuza watakako.

Ahadi hiyo ilitolewa na mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad wakati wa kampeni ya uchaguzi uliopita. Alisema akiongoza serikali, wataruhusu wakulima wauze karafuu wanakotaka.

Dk. Shein alikuwa ameshajulishwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui kuwa maguni 170 ya karafuu kavu yametoroshwa na kupelekwa nje ya nchi.

Lililo jema ni Dk. Shein kusema wazi serikali inawajua watu waliohusika na “tutahakikisha wanakamatwa na kushitakiwa.”

Karafuu zilizotoroshwa alisema kwa bei ya soko wakati huo, zina thamani ya Sh. 36 bilioni.

“Ati wanajigamba wataendelea, mawee… hawawezi. Sisi tuna nguvu kubwa, hii ni serikali. Na tunawaambia nanyi wapelekeeni salamu huko waliko, tutawashinda wote hawana pa kukimbilia.

“Ndugu wananchi, nataka muwaambie  kwamba wanachokifanya si halali kwenu na si halali pia kwa serikali yenu,” Dk. Shein alisema katika lugha ya kuthibitisha mamlaka yake.

Waziri Mazrui hivi karibuni aliniambia kwamba uchunguzi madhubuti umeanza kujua wahusika katika mpango mzima walivyonunua karafuu hadi kuzitoroshwa na kwamba tayari boti iliyotumika kusafirisha pamoja na mmiliki wake wamejulikana.

Karafuu hizo zilitoroshewa mkoani Tanga kabla ya kupakiwa kwa chombo kingine na kupelekwa nchini Kenya ambako mawakala wa serikali huko huharakia kuzinunua.

Zanzibar imekuwa ikilaumu hatua ya Kenya kununua karafuu wasiyoizalisha katika ardhi yao. Zanzibar ndiyo mzalishaji pekee wa karafuu kwa ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika.

Mazrui anasema msimu huu kiasi cha tani 3,000 za karafuu zinatarajiwa kupatikana. Serikali imetenga kiasi cha Sh. 60 bilioni (dola 20 milioni) kwa ajili ya Mpango wa kufufua karafuu.

Pamoja na mambo mengine, fedha hizo zinatumika kuzalishia miche, kununulia vifaa vya uchumaji na hifadhi ya karafuu kavu na komesha magendo.

Lakini, serikali inapoapa kukomesha magendo ya karafuu huku ikihusisha wakuu wa mikoa na vikosi vya ulinzi na usalama katika kampeni, imesahau baadhi yao ni wanufaikaji wa magendo?

Taarifa hizi zipo kwenye kumbukumbu za Baraza la Wawakilishi tangu mwaka 203 pale lilipounda kamati teule kuchunguza tuhuma zilizoenea kuwa viongozi wa serikali wanauza karafuu kwa magendo.

Kamati hiyo iliongozwa na mheshimiwa Ali Juma Shamhuna, mwakilishi wa Donge wakati huo akiwa nje ya serikali. Taarifa ya uchunguzi wake ilisomwa barazani.

Hakutaja jina la kiongozi yeyote lakini habari za ndani ya kamati ile zilitaja majina ya viongozi kadhaa waliokuwa Pemba wakiwemo wakuu wa mikoa.

Baadhi ya viongozi hao wangalipo kwenye viti. Walichukuliwa hatua gani wakati ule? Wanapewaje dhamana nzito leo?

Wakati utaamua mbivu na mbichi. Ila wachunguzi wa kiraia, wakiwemo waandishi wachokonozi, wataifanya kazi ya kufuatilia kampeni na watafichua kila watachokibaini.

Ndipo unapokuja mshikamano wa kampeni ya kuilinda karafuu na ukomeshaji wa ufisadi kupitia sheria mpya ya kupambana na rushwa ambayo muswada wake umeidhinishwa wiki iliyopita na baraza.

Wajumbe wa baraza walishiriki semina ya kujadili muswada wa sheria ya kupambana na rushwa na ufisadi iliyowasilishwa katika semina hiyo na serikali.

Kokote kule itakoanzia kubana mafisadi, ukweli unabaki kuwa baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu serikalini lazima washughulikiwe kwani wamekuwa wakinenepa na kutajirika kwa mgongo wa utumishi wa umma.

Wanachuma mali binafsi kwa kutumia nafasi walizopewa na rais ili wawatumikie wananchi. Mtindo huo unakua sana kiasi cha wengi wao kuonekana wenye mali nyingi sasa isiyostahili kwa mapato yao.

Kwa muda mrefu, viongozi kama hawa wamekuwa wakilindwa na utawala hadi wengine kufikia kustaafu utumishi. Mfumo wa kulindana miongoni mwa viongozi wa serikali umeimarika.

Unaimarika hakika. Kwanini waliopora kituo cha watoto Forodhani hawajashikwa? Waliotajirika kupitia mikataba ovyo ya kuendesha ukumbi wa disko wa Hoteli ya Bwawani hawajashikwa?

Waliotwaa viwanja viwili hata vitatu vilivyopimwa Tunguu na kwingineko; walionunua gari kuukuu kwa gharama ya gari mpya katika mradi wa MACEMP je?

Waliojenga ukuta ‘mshenzi’ makao makuu ya Ghuba ya Menai kwa kutumia mafundi uchwara je? Waliofanikisha wizi wa dola za wananchi benki yao ya PBZ je?

Walionufaika na mpango wa kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa je? Waliohujumu karakana ya serikali Chumbuni; wanaohujumu mitambo ya Idara ya Ujenzi wa Barabara je?

Kweli, wenye dhamana wanakodisha mitambo/magari ya kubeba kokoto kwa ajili ya miradi ya barabara halafu mapato yanaingia mifukoni mwao? Kweli?

Itaendelea…

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: