Dk. Shein hamjui Francis Cornish


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 29 June 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Francis Evans Cornish

RAIS Dk. Ali Mohamed Shein, pengine kwa alichojifunza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikokuwa makamu wa rais kwa miaka minane, amehamishia semina elekezi Zanzibar.

Ameshaitisha semina kwa mawaziri na manaibu wao. Ameitisha semina kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu wakuu na manaibu wao, pamoja na wakuu wa taasisi za serikali.

Semina ya pili ilikuwa wiki iliyopita. Hii ilishirikisha makatibu wakuu, manaibu wao, na wakuu wa taasisi za serikali na kaulimbiu yake ilikuwa: “Utendaji ni wa kuwatumikia wananchi.”

Dk. Shein alibainisha nguzo kuu za utumishi wa umma katika awamu yake na kuhimiza ziwe ndio muongozo kwa watumishi wote. Baadhi ya nguzo hizi ni kutenda kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za fedha; na uwajibikaji.

Lakini wakati ametimiza miezi minane tangu awe Rais wa Zanzibar, ndani ya Baraza la Wawakilishi, chombo cha kutunga sheria za kutawala watu na kazi za serikali, mawaziri alowateua wanalaumiwa kwa utoro wakati wa vikao.

Kwa sasa, serikali inawasilisha bajeti – makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2011/12. Baada ya bajeti kuu kupitishwa, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, ameanza kulalamika “mawaziri wanatoroka vikao.”

Tena anatoa lawama hizi wakati mezani kwake kunaendelea mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais iliyoko chini ya Balozi Seif Ali Iddi, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyeteuliwa na rais na pia mbunge wa Kitope kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ofisi yake ndiyo inayosimamia utendaji wa serikali. Kiongozi wake, kwa hivyo yeye Balozi Iddi, kikatiba, ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi ambalo pia lina jukumu la kuisimamia na kuishauri serikali namna nzuri ya kutumikia wananchi.

Spika Kificho, ambaye ameamua kutoficha ukweli, amesema kati ya mawaziri wote 19, wakiwemo watatu wasiokuwa na wizara maalum, mawaziri wawili tu ndio walimuaga kwamba hawatakuwepo barazani siku hiyo.

Wakati anatamka hayo – bila ya shaka akionyesha kuchoka kuvumilia utoro wa mawaziri wa Dk. Shein – mawaziri saba hawakuwepo ukumbini. Hapo ilikuwa mapema asubuhi baada tu ya spika kuongoza dua ya kuombea siku njema ya shughuli za baraza.

Akawataja mawaziri hao wawili waliompa taarifa rasmi kama utaratibu unavyotaka, kuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Haji Omar Kheri na wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Zainab Mohamed Omar.

Kumbe mawaziri wanadharau wajibu wao. Hawaheshimu sheria na kanuni au nguzo kuu ya utumishi – uwajibikaji.

Kama mawaziri wanakuwa mfano wa kutowajibika na ikabainika na wananchi, ni tatizo kubwa. Wanachokifanya ni kuiba muda wa serikali. Wanaiba fedha za serikali. Nasisitiza hizi ni fedha za wananchi wanazolipa kupitia kodi mbalimbali.

Unapokuwa na mawaziri watoro wa kutumikia wananchi, hapo unajua kabisa dhana ya uwajibikaji, imepigwa kumbo, imebezwa na kudharauliwa. Matokeo ya dharau hiyo, ni kutotumainia maendeleo. Mahali pasipokuwa na uwajibikaji, huwezi kutarajia pakapatikana maendeleo.

Mawaziri wakidharau uwajibikaji, makatibu wakuu, manaibu wao na wakuu wa taasisi zilizo chini yao wafanyeje? Katika hali kama hii, wafanyakazi wa chini yao watafanyaje? Hawatawajibika. Watalala. Nani atawawajibisha? Hayupo maana walio juu yao wamelala. Huko ni kulewa madaraka.

Hee, mawaziri wanalewa madaraka mapema hivi! Miezi minane tu ya uongozi, wanachagua kazi. Na siyo kuchagua kazi, bali kupuuza kazi walizopewa na kula kiapo kuzitekeleza baada ya kuteuliwa.

Lakini, yote hayo tisa. Twende mbele.

Wakati Dk. Shein anahimiza uwajibikaji na nidhamu kwa utumishi wa umma, wakiwemo wateule wake, mwenyewe yupo kwenye rekodi ya kukwepa wajibu wake.

Wiki tatu zilizopita, alipokutana na viongozi wa wilaya na mikoa katika kuhitimisha ziara zake kiserikali, na baada ya kulalamikiwa kushamiri kwa tatizo la wananchi kuporwa ardhi, aliwageukia viongozi, akasema:

“Mtajuana wenyewe... aliyesababisha (tatizo) atatatua. Viongozi waliopora ardhi za wananchi na kuziuza watajua wenyewe namna ya kurudisha fedha za watu ili wananchi wabaki na ardhi yao.”

Ni kauli inayovunja moyo wananchi na inachoma moyo wale walioathirika na uporaji huo wa ardhi ambayo wamekuwa wakitumia tangu enzi na dahari.

Kauli hii inapotolewa na kiongozi mkuu wa nchi inachukuliwa sawa na yule baba aliyemwambia mwanawe alipojikata kisu wakati akikichezea; “Utajijua mwenyewe.” Hivi ni kweli mtoto atajua mwenyewe la kufanya?

Kukomesha uovu huo kwa wale ambao Dk. Shein anaamini ama wameshiriki kuidhinisha au walinyamazia wasaidizi wao walipokuwa wanaidhinisha, kilichotakiwa wakati ule, na kinachotakiwa sasa ni kuchukua hatua kutatua. Utatuzi waweza kuwa kushitaki wale waliouza ardhi ya wananchi. Ni mafisadi kama wanaoiba fedha za serikali.

Tatizo la wananchi kuporwa ardhi linakua Zanzibar. Ardhi kubwa imetwaliwa kinyemela na viongozi na wapo waliouza kwa bei mbaya kwa wageni. Malalamiko yapo ukanda wa mashariki na kusini mwa kisiwa cha Unguja.

Uporaji wa ardhi ya wananchi kama huo umefanywa pia maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Pemba. Mapande ya ardhi yameuziwa wageni, wakiwemo waliojipachika jina la wawekezaji na kuyatumia kuombea mikopo kisha kukimbia nchi.

Sasa wananchi wanataka utumishi uliotukuka, utumishi uliojaa utu, nidhamu na uadilifu – yote haya ni yaleyale ambayo Dk. Shein anayahimiza anapofungua semina zake elekezi.

Picha hiyo inasumbua sana. Yapasa rais, wasaidizi wake na washauri wake, warudi kwenye mstari na kutambua wajibu wao. Wafahamu kuwa wananchi wanamatumaini makubwa nao.

Katika serikali yetu, lipo tatizo kubwa la ukosefu wa uwajibikaji. Kuanzia juu ya uongozi mpaka chini. Viongozi wanapaswa kuwa mfano kukomesha udhaifu huu.

Tuangalie funzo liliopo katika simulizi zinazomtaja mwanasheria aliyewahi kuwa hakimu nchini Canada enzi za karne ya 18.

Akiwa hakimu wa mahakama ya Winnipeg mwaka 1874, Francis Evans Cornish, alijiadhibu faini ya dola 5 au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kufika kazini amelewa.

Alipofika, aliingia mahakamani na kuketi kitini kwake. Akasema, “Kesi ya kwanza leo ni inayonihusu mimi mwenyewe. Nimefika kazini nimelewa kwa hivyo nitakuwa mshitakiwa wa kwanza. Kosa hili ni dharau ya mahakama ambayo hukumu yake ni faini ya dola tano au kifungo cha miezi mitatu jela.” Alifika na fedha zake mfukoni, akalipa faini. Ametimiza dhana ya uwajibikaji mbele ya kadamnasi ya watu.

Viongozi wetu wajipime. Wakitenda kosa, wajiadhibu kabla ya kuadhibiwia. Ndipo watathibitisha kutenda haki kwa watumishi walio chini yao. Wajipige faini na wanaposhindwa kulipa, watinge jela. Hapo wananchi wataamini wamepata viongozi watendaji na siyo watamkaji tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: