Dola inadhalilisha Bunge


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Imefilisika kifedha na kwa hoja

JUMA lililopita nilijadili tukio la jaji mkuu tuliyenaye kuonekana katika mazingira yanayoshawishi kuwa yeye ni sehemu ya mhimili wa utawala.

Kitendo chake cha kukaa katika semina elekezi ya watendaji wakuu wa serikali, akishuhudia rais akitoa maelekezo kwa watendaji, kinaweza kumfanya afikiri kuwa naye anaelekezwa na rais katika kazi zake.

Aidha, kitendo cha yeye kutumika kutoa maelekezo kwa watendaji wakuu wa serikali, kinajenga hisia kuwa hata yeye anaweza kutoa maelekezo ya namna hiyo kwa majaji na mahakimu.

Hilo likitokea, utakuwa ni mwiba mkali katika mhimili wa mahakama zetu.

Hisia zangu zaweza kuwa zinapotosha ukweli, lakini yeye jaji mkuu na majaji wenzake wachache wenye tabia ya kujipendekeza kwa wakuu wa serikali, wanajua ninachokisema.

Punde si punde yaweza kuibuka mawasiliano machafu baina ya jaji mkuu, majaji na mahakimu yatakayothibitisha kuwa mahakama yetu haiko huru hata kidogo.

Ukiacha mbali utata wa uteuzi wa jaji mkuu, liko pia suala la hekima iliyotumika, siyo tu kumwalika katika semina ile “elekezi,” bali hata uhusiano wa kinasaba na wakuu wengine wa vyombo vya dola.

Cheche hizi katika taifa ambalo linalazimisha watu waende kulala bila kula, siku moja zaweza kuzusha moto mkali katika vyombo vyetu nyeti na ambavyo vinapaswa kuishi mbali na tuhuma kama hizi.

Dola yetu na mihimili yake mitatu – bunge, mahakama na utawala/serikali – inapaswa kuwa na haki sawa katika maongozi ya nchi. Kiongozi wa bunge ni spika, Anne Makinda.

Hata kama katika ujumla wake unaounda dola, mkuu wa nchi ambaye ndiye mkuu wa mhimili mmojawapo anakuwa ndiye “mwenyekiti” wa umoja wa dola yetu, bado katiba yetu, pamoja na ubovu wake, inatamka uhuru wa kila mhimili katika utendaji wake wa kazi kila siku.

Yako maeneo ambako mihimili hii inategemeana, bali si kwa kulazimishana ila kwa kushauriana na kushawishiana.

Hivyo basi, mkuu wa dola hana budi daima kuonekana anasahau kuwa yeye ni “mwenyekiti” wa wenzake wawili ili kustawisha uhuru wa utendaji wa wakuu wawili waliobaki katika mihimili yao.

Kumbe ndiyo sababu tunatakiwa kuwa makini katika kuchagua mtu anayeitwa rais na mkuu wa nchi.

Kwani rais na mkuu wa nchi asiye na akili sawasawa, anaweza kuvuruga nchi na kusababisha maafa makubwa kwa taifa na ustawi wake.

Ni mkuu huyuhuyu ambaye anaweza kuamua mtu afe akafa; nchi iende vitani ikaenda, bunge livunjwe likavunjwa, na maamuzi mengine makubwa chini ya katiba yetu ya sasa.

Baada ya makala ile, yametokea mambo kadhaa yanayoashiria ama kupungua kwa umakini katika kuongoza dola, au uzembe wa wazi wa kuingiliana kwa mihimili.

Yote mawili hayana ushahidi, lakini kukosekana kwa ushahidi peke yake katika taifa letu, si uthibitisho wa uhakika kuwa jambo fulani halikutendeka.

Kwa maoni yangu, muingiliano wa mamlaka za mihimili yetu, siku za karibuni umelidhalilisha na kulifedhehesha bunge letu pale wabunge wake wa upinzani walipoanza kukamatwa na polisi na kuwekwa rumande kwa sababu za kisiasa.

Bunge limedhalilishwa na mhimili wa serikali pale vyombo vyake vya dola vilipojipa jukumu la kuamua ikiwa matamshi fulani ya wanasiasa kama ni “siasa safi” au “siasa mbaya.”

Uelewa huu mpya wa siasa miongoni mwa polisi umetoka wapi kama si shinikizo la wanasiasa kwa jeshi la polisi?

Serikali imekabidhi masuala ya kisiasa mikononi mwa polisi na kuwanyang’anya wabunge haki ya kukutana na wapigakura wao mpaka wapate ruhusa ya polisi na mazungumzo hayo yasimamiwe na polisi kwa muda uliowekwa na polisi.

Imekuwa kana kwamba wapigakura ni wafungwa na wabunge ni jamaa zao wanaofika kuwatembelea gerezani; na wakati wa mazungumzo sharti askari magereza awepo kusikiliza mazungumzo hayo.

Wakati haya yanafanyika, wabunge wa chama tawala wanashangilia kwa kuwa wao hawahitaji kibali wala kusimamiwa na polisi katika mikutano yao. Hili lina gharama kubwa tuendako.

Bunge limedhalilishwa na mhimili wa mahakama pale mahakimu walipoamua kupeleka akili zao likizo na kuazima za wanasiasa katika kufanya kazi zao zinazowahusu wanasiasa.

Tumeshuhudia mahakimu Tarime na Urambo, kwanza wakigoma kutoa dhamana kwa kosa linaloruhusu dhamana, na pale walipoikubali, wakaweka dhamana ngumu sana kana kwamba wanafurahia wabunge wabaki mahabusu.

Tumeshuhudia kosa la kibinadamu la hakimu wa Arusha kubatilisha hati ya kukamatwa na baadaye kuisaini ikimdhalilisha kiongozi wa upinzani bungeni.

Serikali hiihii ambayo inakaribia kuzimia kwa kukosa fedha ikapata fedha za kujaza mafuta magari ya polisi ili kutetea kosa la hakimu mjini Arusha.

Serikali hiihii na vyombo vyake, ina kipimo cha ajabu cha kuisaidia kuamua mbunge gani imwombee ruhusa kwa spika ili ahojiwe au kukamatwa; na ni yupi polisi wanaidhini ya kumhoji au kumkamata bila kwanza kuwasiliana na spika.

Udhalilishwaji wa bunge mikononi mwa mahakama na serikali umeshangiliwa sana na wabunge wa chama tawala kwa upofu unaoweza kukigharimu chama chenyewe siku za karibuni.

Hii ni kwa sababu, misingi mibovu ya kutafsiri sheria na katiba ikiachwa ifanye kazi na kuzoeleka, baadaye misingi hiyohiyo huota usugu unaoweza kukidhalilisha chama tawala chenyewe kikibahatika kubaki madarakani.

Au hata kikiondoka madarakani, misingi ileile mibovu ya kutafsiri sheria hutumika kukikandamiza kinapokuwa chama cha upinzani.

Sheria kandamizi na za kudhalilisha bunge zisiachwe kuendelea eti kwa sababu zinakikandamiza chama cha upinzani.

Ubovu wa sheria haubagui chama wala mtawala pale hali ya kutotawalika itakapokuwa imeruhusiwa na watawala vipofu na walevi wa madaraka.

Dola yetu imefilisika kwa kukosa fedha na hoja. Kilichobakia ni ubabe wa polisi na mahakama katika kunyamazisha hoja zisizojibika.

Taarifa zilizozagaa katika mitandao hivi sasa zinasema chama tawala na mtawala wake walipata kura chache sana katika vituo na makambi ya polisi.

Ukiwauliza polisi wenyewe wanasema wazi kuwa wamepigika na ndiyo maana wao na rushwa ni kama chanda na pete.

Ugumu wa maisha unaowakabili polisi hauwezi kuondolewa kwa kuwafanya polisi watumike kama chombo cha kukandamiza demokrasia nchini.

Tayari mbegu imepandwa ndani ya polisi mmojammoja na imemea. Nani anabisha kuwa ikikua yaweza kukataa kutekeleza amri haramu kutoka kwa watawala waliofilisika?

0
No votes yet