DPP aweza kupoteza heshima, kazi 


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
DPP Feleshi akiapishwa alipoajiriwa

UKITAKA kujua jinsi mwenye madaraka anavyoweza kupoteza heshima na hata kazi yake, msikilize Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi.

Feleshi anasema ofisi yake haina ushahidi kuhusu kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, inayodaiwa kukwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu (BoT).

Anataka mwananchi yeyote mwenye ushahidi huo, aupeleke ofisini kwake au polisi ili wautumie kwa uchunguzi.

Ofisi ya DPP ndiyo ofisi kuu nchini yenye mamlaka ya kuamua huyu ana kesi ya kujibu, hivyo ashitakiwe; au hana kesi ya kujibu, hivyo asishitakiwe. Mamlaka makubwa sana.

Kwa miaka sita sasa, hakuna taarifa za polisi kukamata yeyote kuhusiana na Kagoda. DPP hajakabidhiwa lolote la kufanyia kazi wala hajaonyesha juhudi za kutafuta mwenyewe.

Sasa DPP Feleshi ameamua “kuomba” mwenye ushahidi juu ya Kagoda ampelekee. Kama hii siyo dharau, basi ni uchovu; au ni dalili za Feleshi kutaka kufukuzwa kazi. Tujadili.

Kwanza, hapa kuna kampuni inaitwa Kagoda. Iliwasilisha BoT hati za kughushi na kujichotea zaidi ya Sh. 40 bilioni.

Waliosajili kampuni hii wapo. Ni John Kyomuhendo na Francis William – watu wawili wenye hali dhaifu zisizofanana na mabilioni ya shilingi yalizokwapuliwa.

Pili, hakuna ushahidi wa polisi kukamata watu hawa wasiofanana na mabilioni ya shilingi, kuwahoji na kupata fununu juu ya nani hasa alikwenda BoT kufanya “dili” na maofisa wa benki.

Tatu, hakuna ushahidi wa polisi kuwahoji Kyomuhendo na William kuhusu mabilioni  hayo ya shilingi kuwapita bila kubadili maisha yao.

Nne, hakuna ushahidi kwamba watu hawa waliishabanwa ili kutaja nani hasa walikwenda BoT kusaini nyaraka za kupokea fedha; na nani walihamisha fedha kutoka benki kuu hadi benki ya biashara?

Tano, kuna taarifa za kuhamisha fedha kutoka tawi moja hadi matawi matano ya benki moja. Vyombo vya habari viliishaorodhesha hata majina ya matawi na akaunti ambamo fedha ziliingizwa.

Nani alihamisha fedha hizo? Nani alipokea fedha hizo katika matawi mengine? Yako wapi majina ya waliokuwa wakisaini na nani walikuwa wakilipwa?

Sita, wako wapi mameneja wa matawi hayo ya benki waliosaidia uwekaji na uchukuaji ili waeleze nani hasa alikuwa anachota fedha hizo? Kweli ni Kyomuhendo na William au ni wengine? DPP Feleshi anataka msaada gani zaidi?

Saba, Waziri Mkuu mizengo Pinda aliishajichanganya. Mara ya kwanza aliwaambia wahariri ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam kuwa, serikali haiogopi mtu yeyote na kwamba wezi wote watawindwa bila kujali “nani ni nani” ikiwa ni pamoja na Kagoda.

Baada ya miezi sita hivi, akanukuliwa akisema ni vigumu kukamata na kushitaki Kagoda. Kama Feleshi hajaonana na Pinda kutaka kujua ugumu wa kukamata na kushitaki Kagoda, basi hataki kazi yake.

Nane, kuna ushahidi wa nyaraka. Huu umeandikwa mara nyingi magazetini. Unaitwa “ushahidi wa kiapo” wa wakili wa kujitegemea Biydinka Sanze.

Sanze ananukuliwa akieleza katika hati ya kiapo mbele ya chombo teule cha rais jinsi alivyoitwa, kutambulishwa kuhusu Kagoda na kuombwa kushuhudia hati za Kagoda zilizotumika kuchukua fedha benki.

Haya yameandikwa kwa muda mrefu. Ama DPP Feleshi ameyasoma na kuyadharau; au anadhani wananchi wana uelewa mdogo. Anakosea, hasa kuhusu Kagoda.

Tisa, Rais Jakaya Kikwete aliunda kile alichoita “Kikosi Kazi,” kuchunguza walioiba BoT. Jukumu la kikosi lilikuwa kujua nani alikuwa na kampuni ipi, alikwapua kiasi gani, akiwa na nani; na kufuatilia ziliko fedha hizo.

Kwa njia hii rais aliahidi watakaogundulika na kukubali kurudisha kiasi cha fedha walizoiba, hatawafikisha mahakamani.

Kagoda ni moja ya makampuni ambayo inasadikiwa kikosi cha rais kilihoji na kampuni hiyo ikakubali kurejesha fedha.

Kikosi kilikuwa cha watu watatu: aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali Johnson Mwanyika, Inspekta Jeneral wa Polisi (IJP) Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah.

Kama hajachoka kazi, Feleshi anashindwa vipi kuwauliza hao na badala yake anataka msaada wa wananchi mitaani ambao anajua hawajui?

Kumi, miezi mitatu iliyopita, ziliibuka taarifa kuwa Yusuf Manji ndiye mwenye Kagoda. Alikana haraka na kusema yeye alisaidia kulipa kiasi cha fedha ambacho Kagoda walitakiwa walipe ili kampuni hiyo iweze kumrudishia fedha zake hapo baadaye.

Kumi na moja, Manji baada ya kuonyesha kuwa anaifahamu Kagoda, sasa anadai kuwa ataipeleka mahakamani kwa kushindwa kumrejeshea fedha zake alizolipa serikalini kwa niaba yake.

Kumi na mbili, sasa tunajua kuwa Kagoda iliishalipa sehemu ya mabilioni ya shilingi iliyokwapua, hata kama hatujui yakowekwa mabilioni hayo.

Kwa kauli hiyo, serikali inajua Kagoda ni nani; kama anavyojua Manji ambaye anaidai. Wengine ni pamoja na Rais Kikwete na waziri mkuu Pinda. Kwa nini Feleshi hawaulizi ?

Wengine wanaoifahamu Kagoda ni John Kyomuhendo, Francis William, Johnson Mwanyika, Saidi Mwema na Dk. Edward Hoseah.

Kwenye orodha ya wanaoifahamu Kagoda, ongeza wakili Byidinka Sanze na Rostam Aziz ambaye wakili anamtaja kuwa ndiye alimwalika kushuhudia hati za Kagoda, akidai rais mstaafu Benjamin Mkapa ndiye aliruhusu uchotaji huo.

Wengine ni maofisa wa benki ambako fedha zilichukuliwa na kule zilikopelekwa, ambao wanajua waliokuwa wakichukua fedha na saini zao.

Bali yule ambaye hana mashaka hata kidogo kuhusu Kagoda, ni Rais Kikwete ambaye, kupitia kikosi kazi chake, anajua kampuni hiyo ilipaswa kurejesha kiasi gani cha fedha.

Rais anajua au anapaswa kujua Kagoda ililipiwa kiasi gani na Manji ndipo akaacha kuipeleka mahakamani.

Ni kweli ofisi ya DPP ina madaraka makubwa ya kuamua kushitaki au kutoshitaki. Inawezekana basi, katika mamlaka hayo, imekataa kushitaki Kagoda.

Inawezekana ndivyo, kwa vile DPP ana mamlaka yaliyopitiliza na ambayo yanaweza kutumika vibaya hadi ofisi yake ikatuhumiwa kula rushwa.

Tukienda kwa mfano huu wa fomula: Rushwa (R) ni sawasawa na mamlaka (M) jumlisha hiari ya maamuzi (H) toa uwajibikaji (U) au (R=M+H-U); basi utaona ofisi ya DPP ina uwezekano wa kutumbukia na kumezwa na ufisadi.

Ofisi hii inawajibika kwa rais ambaye anajua Kagoda ni nini, iko wapi; ilichukua kiasi gani, imerejesha kiasi gani na kwa nini haikushitakiwa.

Lakini mkurugenzi wake anasema anawataka wananchi kumpa ushahidi wa wizi wa Kagoda. DPP anafanya sarakasi. Anafanya masihara.

Nchini Uingereza ambako umechukuliwa mfumo huu, DPP anawajibika kwa bunge. Hili linapunguza mamlaka yaliyopitiliza na  maamuzi yasiyo kizuizi ambayo yaweza kuchumbia rushwa au udhaifu wa aina hiyo.

DPP Feleshi anafanya mzaha kuhusu Kagoda. Anatutania au ana kitu anaficha; au kuna kitu anaogopa kuweka wazi. Hili litamgharimu kazi na heshima.

0713 614872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: