Dua la kuku la CCM laishindwa CHADEMA


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

KATIKA mchezo wa soka kuna mambo mengi yanayovutia mashabiki. Pale ligi inapokaribia mwisho, utasikia mengi zaidi, hasa kutokana na nafasi ya kila timu kunyakua ubingwa.

Wakati baadhi ya timu zinakuwa zimekata tamaa, nyingine zinakuwa zinaomba dua kuchukua ubingwa. Katika ligi hiyo zitakuwamo pia zile zinazoomba dua mbili — ushindi wa michezo yao, na kushindwa kwa wapinzani wao ili zenyewe ziwe kwenye nafasi nzuri.

Mazingira haya ya kuomba dua mbili, ndiyo yanayokikumba Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kinazidi kuomba kiimarike na kukubalika tena kwa jamii, na wakati huo huo, kinaomba wapinzani wao, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wapate migogoro isiyoisha na kusambaratika.

Ndiyo kisa, utasikia wale wanachama wa CHADEMA wanaoanzisha chokochoko ndani ya chama wanakuwa ndio marafiki wa CCM na serikali yake. Ndio wanaoonekana wazuri na mabingwa wa demokrasia.

Rafiki yangu mmoja mwenye mapenzi na ushawishi ndani ya CCM, alinidokeza baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010, kuwa pamoja na chama chake kupata ushindi kwa mbinde, “kazi yao dhidi ya CHADEMA ilikuwa imemalizika.”

Kada huyo wa CCM alisema, “Subiri uone jinsi CHADEMA itakavyosambaratika kama ilivyokuwa NCCR-Mageuzi baada ya uchaguzi wa mwaka 1995.”

Kwa kuwa sikuwa nafahamu vizuri CHADEMA wamejipanga vipi kukabiliana na migogoro, nilimsikiliza na kumwamini kwa kiwango fulani. Lakini hadi leo nimesubiri sijaona majibu.

Kauli kama hizi zimekuwa zikitolewa na wanachama na hata viongozi wengi wa CCM. Imani yao ambayo ndiyo dua yao ni kwamba CHADEMA isambaratike na kuishiwa nguvu.

Watetezi wa hoja hii wanatoa mifano ya NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) ambayo kura za wagombea wake zinazidi kupungua, hasa upande wa bara.

Kimsingi hakuna chama kisichokuwa na migogoro, lakini kinachotakiwa ni umahiri wa viongozi wa chama hicho kutatua migogoro husika kabla haijaleta madhara na kusababisha kisambaratike.

CHADEMA kama vyama vingine, kina migogoro mingi ya ndani yake — baadhi ya migogoro ni wanachama wenyewe, mingine ya mapandikizi ya watawala, lakini viongozi wake wamekuwa wajanja na wepesi wa kuitatua na kuimaliza ndani ya vikao.

Uwezo huu wa viongozi umegeuka msumari wa moto kwa CCM, maana dua lake limekuwa kama la kuku lisilompata mwewe. Wameshindwa kupenya na kukisambaratisha.

Kushindwa kwa mkakati wa kuisambaratisha CHADEMA ndiyo hofu kuu iliyobaki kwa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wanachama na viongozi wa chama hiki wanajua fika kwamba ushawishi na mvuto wake kwa jamii umepungua. Wanafahamu kuwa kundi la Watanzania walio wengi, la vijana, halina mapenzi na chama chao.

Viongozi hawa wa CCM ni mashuhuda kwamba hata makada wao wa siku nyingi wanaanza kuachia ngazi. Na zipo taarifa kwamba hata waliokuwa wajumbe wao wa nyumba 10 waliokuwa mtaji wa chama, wamekataa kuwania nafasi hizo.

Kinachoshangaza sasa ni jinsi chama kinavyoendelea kufanya au kukumbatia mambo yanayokishusha badala ya kukipandisha hadhi.

Mojawapo ya mambo hayo, ni jinsi CCM inavyoendelea kuwakumbatia wanachama wake wenye tuhuma za ufisadi na wizi wa fedha za umma, na kuwabembeleza baadhi yao wajiondoe kwa utaratibu unaotajwa kama “kujivua gamba” huku wengine wakilindwa.

Tatu, ni jinsi chama hiki kikongwe kinavyoshindwa kuiwajibisha serikali yake kwa kushindwa kulinda rasilimali za umma na badala yake mawaziri na watendaji wake wakaishia kujinufaisha wenyewe.

Nne, namna chama hicho kilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake lukuki kwa wananchi, hasa ahadi mama ya kuleta “Maisha bora kwa kila Mtanzania”.

Kasoro hizi zote kwa chama kinachotawala, zinaonekana na kuathiri moja kwa moja maisha ya Watanzania. Miradi ya maendeleo inasimama, shule hazina walimu, vijana wanakosa ajira, mikopo ya elimu ya juu ni taabu na mbaya zaidi umaskini umekithiri kila kona ya nchi.

Ajabu, hata pale inapotokea fursa ya kisiasa ya chama hicho kuonyesha kuwa kinaweza kuwakomboa Watanzania kinarudi nyuma na kuwaacha watani wao wa jadi sasa, CHADEMA, watambe.

Mathalan, bungeni wakati wa muswada wa mabadiliko ya katiba, wabunge wa CCM walipigania mambo ambayo ni ya maslahi kwa chama zaidi badala ya taifa.

Mfano mwingine, ni pale ilipotokea fursa, ya kuorodhesha wabunge 70 ili kuwasilisha hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu au mawaziri wenye tuhuma za ubadhirifu na wizi wa fedha za umma wajiuzulu, chama hicho hakikuonyesha makeke yake.

Kati ya wabunge 258 wa CCM watano tu ndio waliounga mkono. Wengine wote, kama alivyosema mwenzao, Deo Filikunjombe wa Ludewa, ni “waoga na wanafiki.”

Wabunge wa upinzani, isipokuwa John Cheyo wa UDP, waliweka saini zao. Shinikizo la wabunge hao, ndiyo matarajio tuliyonayo sasa Rais Kikwete akubali kuwa huu si upepo tena, bali ni kimbunga, na hivyo kukubali shingo upande “kusuka upya” baraza lake la mawaziri.

Kinachonishangaza zaidi hata wale waliojibatiza kuwa ni ‘mitume 12” au wapambanaji wa ufisadi ndani ya CCM, hawakuweka saini zao.

Kwa mazingira haya, hivi CCM itakwepaje mtego wa kuomba “dua la kuku” dhidi ya CHADEMA wakati haina uwezo wa kuondoa kasoro nilizotaja hapo juu?

Kama wabunge wake wamekumbatia chama badala ya kuinyoosha serikali inayoshindwa kutumia vizuri fedha zao, chama kinataka wananchi wafanyeje, kama si kukiadhibu?

Kwa takwimu za mfumuko wa bei uliopanda kutoka asilimia 4 mwaka 2005 hadi asilimia 19.8 mwaka huu, chama hicho kitaachaje kuomba CHADEMA ife, na haifi?

Kwa wananchi, ukieleza takwimu za mfumuko wa bei hawana habari nazo, lakini ukieleza bei ya sukari ambayo kilo moja inakwenda hadi Sh. 3,000 au sukari ya kupima ya Sh 200 kwenye vifuko vilivyochomelewa kwa mshumaa wanapata somo lenyewe.

Ukiwaeleza jinsi baadhi ya wananchi wanavyokwenda na mswaki dukani kuwekewa dawa ya meno ya Sh. 10 au Sh. 20 wanaelewa vizuri.

Hawa wanaozidi kuelewa somo siku wakitoa uamuzi wa kuhamishia mapenzi yao kwa chama kingine, au kuhamisha kura zao kwenye sanduku, itakuwa balaa.

Lakini hata hayo yakifanyika, hawatakosekana watu wa kuwabeza kwa kuwabatiza majina wakitaka tuamini kwamba ilikuwa lazima wawapende hata kama hawatimizi wajibu wao.

Bila kuwapo mabadiliko ya kweli ndani ya chama na viongozi kuanza kuwajali wananchi badala ya wao binafsi, CCM itazidi kuomba dua la kuku, huku wapinzani wao wakizidi kupaa.

0788 346175
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: