Duniani hakuna chama pendwa milele


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

NILIWAHI kuandika kwamba zinakuja siku ambazo watatokea waandishi mahiri watakaoandika hayahaya tunayoandika sisi, lakini wao watatuzwa tuzo na nchi yao hiihii!

Hii ndiyo mipango ya Mwenyezi Mungu, mitume na manabii wake kukataliwa au kutotambuliwa na watu wa wakati wao! Wataandika hivihivi kuwa kilichoingia kwa hila kitaondolewa kwa hila kwa maana walioishi kabla yetu walisema, Lila na Fila havitengamani.

Huja tumepungukiwa busara na kwakuwa hatukujaliwa hekima tunawaongoza waja wa Mwenyezi Mungu kwa kubangaiza.

Nimekuwa nikipokea ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa wasomaji wengi wa gazeti hili zikinitaka nichapishe makala hizi katika kitabu kwa faida ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Naomba niwajibu wote hao kwa kusema nimekubali ombi lao na wanaotaka kuchangia uchapishaji wanaweza kufanya hivyo kwa kutumia simu na 0713334239 au 0754334239.

Sasa naomba niingie kwenye mada yangu ya leo. Vyama vingi vya siasa huanza kama vyama vya wananchi. Vingine hujiita ‘chama cha wananchi’. Hujiwekea sura ya ukombozi. Viongozi husema lazima wawakomboe wananchi. Unaweza ukadhani wao siyo wananchi.

Chama chochote cha siasa huanzishwa kwa lengo kuu moja, kushika dola yaani kutawala. Kumtawala nani? Jibu ni kumtawala mwananchi! Hivyo kumkomboa mwananchi ni kumtoa kwa mtawala yule kumweka kwa mtawala mwingine. Huo ndio utaratibu ambao mataifa ya dunia yamejiwekea.

Utaratibu kwamba watu wachache waanzishe vyama vya kisiasa na kitakachoungwa mkono na wananchi wengi ndicho kipewe ridhaa ya kuwaongoza. Uzoefu umeonyesha kuwa viongozi wa vyama vya kisiasa huanza kama watumishi wa wananchi. Kadri wanavyozidi kupata umaarufu hubadilika na kuwa watawala.

Chama cha Mapinduzi (CCM), hiki ambacho leo wafuasi wake wanapiga watu mapanga na kumwagia tindikali wengine, kilianza kama chama cha wakulima na wafanyakazi.

Leo ukikitazama hakina sura ya mkulima wala ya mfanyakazi. Viongozi wake wanaitwa waheshimiwa. Toka lini mtumishi akawa mheshimiwa? Huku ni kuvimbiwa madaraka. 

Viongozi wanapofikia hali hiyo huwa kero kwa wananchi. Kadri wanavyojidhania kuwa ni maarufu ndivyo masikio yao huzidi kuziba na macho yao huzidi kupoteza nuru.

Wanapochokwa hawaoni na wanapokebehiwa hawasikii tena. Inapolazimika kuwaondoa huwa hakuna njia nyingine ila mapambano. Tunaoandika huwa tunaandika kwa lengo moja kuu, kuepusha mapambano.

Tunaonya na kutoa tahadhari ili kudumisha amani. Hakuna walioumbwa na Mungu ili wapigane. Hali inapolazimu wanadamu hupigana. Tunaandika haya ili kuepusha tusifike huko.

Vyama vya upinzani ni muhimu kwa kuwa vinafanya vyama vilivyo madarakani viwajibike. Vinalinda haki za raia na raslimali za nchi visihujumiwe na walioko madarakani.

Ndiyo maana viongozi wa chama cha upinzani wanapoungana na viongozi walioko madarakani huwasaliti wanachama wao. Msaliti ni mtu hatari sana katika jamii.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni chama cha upinzani ambacho kimejipatia umaarufu mkubwa hasa kutokana na ubovu na udhaifu wa CCM. Wanachama wake wengi walitoka vyama vingine wakitafuta matumaini.

Mshikamano wa viongozi ndio hutengeneza uimara wa chama na hivyo kuleta matumaini. Hakuna chama-pendwa! Watu wanataka mabadiliko bila kujali yataletwa na nani.

Viongozi wanapoanza kuonyesha mfarakano hadharani hufifisha matumaini ya wanachama wao. Kuanzisha mjadala wa urais sasa kwa CHADEMA, ni kuanzisha fujo. Matamshi yaliyotolewa na kiongozi wa CHADEMA katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kuwa, “mwaka 2015 nitakuja tena hapa kuomba kura zenu, lakini si za ubunge bali za urais,” ni fujo.

Kugombea urais ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa. Lakini si kila chama kina utaratibu wake wa kumpata mgombea urais? Kila mtu akisimama na kujibwatukia tu, itakuwa ni kukivuruga chama. Na katika CHADEMA kama imani na mapenzi makubwa yaliyoonyeshwa na Watanzania wengi (siyo wanachadema peke yao)  kwa Dk. Willibrod Slaa yataendelea hadi 2015, itakuwaje? 

Ni  ukweli kuwa Dk. Slaa  bado yungali katika vichwa na vinywa vya Watanzania walio wengi. Sisisitizi hapa kuwa fulani awe au fulani asiwe, nasisisitiza taratibu walizojiwekea wenyewe zizingatiwe.

Wakati Zitto Kabwe anatangaza kwamba anutaka urais, Arumeru Mashariki kulikuwa kunawaka moto. Wafuasi wa CHADEMA na Watanzania wanaoipenda nchi yao waliochoshwa na CCM, walitarajia kauli na mawazo ya viongozi wa CHADEMA yangekuwa kuhakikisha ushindi katika ubunge wa Arumeru Mashariki na chaguzi ndogo za udiwani.

Badala yake wakasikia maneno ya ovyo ovyo. Je, yawezekana ilikuwa mbinu ya kudhoofisha kampeni za CHADEMA?

Wakati wengine wanasema CHADEMA wakishindwa Arumeru Mashariki viongozi wote wakitaifa wajiuzulu, kwa maoni yangu wahuni wote waliomo katika vyama vya siasa wadhibitiwe.  Siyo katika CHADEMA tu, bali na katika vyama vingine vyote.

Watanzania hivi sasa wanateswa kutokana na wahuni wachache tu. Kazi za kihuni ziko tele! Waende wakafanye uhuni wao kule!

Tuliwahi kuwasikia viongozi hawahawa wakishawishi iundwe serikali ya kisaliti. Wakatengeneza neno la kihuni eti serikali ya umoja wa kitaifa. Umoja wa viongozi kugawana ulaji, wao wanaita umoja wa kitaifa.

Nani kawaambia kuwa taifa ni viongozi? Uroho wa vyote, mali na madaraka humfanya hata mtu mzima kuwaza sawa na mtoto mdogo.

Ukimsikia mtu anakwambia yeye ni mzalendo jua huyo siyo mzalendo. Mzalendo au mtu mwema hutambuliwa na wengine. Mlevi halisi huwa hajitambui! Mnafiki ndiye hujisifia mwenyewe kama yule Mfarisayo aliyeingia Hekaluni na kusali kwa sauti kuwa, “Nakushukuru Mwenyezi Mungu kwakuwa mimi si kama watu wengine. Mimi nafunga, nalipa zaka na kuwasaidia maskini” Dua yake haikupokelewa!

Kuna mdahalo ulioendeshwa na Startv katika hoteli ambayo zamani iliitwa Movenpick kati ya kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni wa sasa Freeman Mbowe na aliyemtangulia, Hamad Rashid.

Ilitamkwa mbele ya kipaza sauti na mmoja wa wahojiwa kuwa ana rafiki yake mbunge wa CHADEMA aliyemwambia kuwa wakati wa kampeni sehemu fulani ya jimbo lake ilibidi asitaje jina lake kwa kuogopa kunyimwa kura na wasio wa dini yake. Anayetuletea udini hatufai.

Sitashangaa kusikia CCM iko tayari kumsaidia kiongozi wa CHADEMA anayetaka kukisambaratisha chama hicho. Ni kweli watu wanataka mabadiliko lakini CHADEMA watambue hapa hakuna chama-pendwa!

 

0713334239 
0
No votes yet