EAC: Vipusa tu taabu, Shirikisho je?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 07 April 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Waraka wa Wiki

BAADA ya kufufuliwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 1997, jambo moja lilitarajiwa miongoni mwa nchi wanachama.

Kwamba nchi wanachama zinapokwenda kwenye mikutano ya kimataifa, kama kuna upigaji kura au lolote lingine—wana EAC watakuwa na kura moja. Kwamba watasimama pamoja kwa kila jambo.

Kama kuna tofauti yoyote, ilidhaniwa kwamba ingeweza kutafutiwa suluhu kabla ya kufanyika kwa mkutano unaotarajiwa.

Lakini kwa kile kilichotokea hivi karibuni kule Doha, Qatar, inaonekana nchi wanachama wa EAC hawakubaliani katika baadhi ya mambo; mengine yakiwa mambo ya msingi kabisa.

Katika mkutano huo wa Doha, serikali ya Tanzania na Zambia walikuwa wakiomba wapewe ruhusa ya kuuza shehena yake ya pembe za ndovu ilijazana hapa nchini.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), uuzaji wa pembe za ndovu ni jambo lililopigwa marufuku duniani kote. Hii ni kwa sababu idadi kubwa ya tembo imekuwa ikiuawa kwa sababu ya biashara hii haramu.

Ili nchi iweze kuruhusiwa kuuza pembe za ndovu (na bidhaa nyingine yoyote inayotokana na viumbe vilivyo hatarini kutoweka) ni lazima ruhusa itolewe na taasisi inayojulikana kama CITES.

CITES (Contention on International Trade in Endangered Species) ni taasisi inayotambuliwa na UN iliyowekwa kwa ajili ya kuzuia viumbe vilivyo hataraini.

Katika mkutano huo wa Doha, Tanzania na Zambia zilikuwa zimejipanga kwa ajili ya kwenda kuomba kibali ili ziruhusiwe kuuza shehena zake.

Mkutano huo wa Doha ulikuwa ukijulikana kufanyika kwake tangu katikati ya mwaka jana. Na tangu wakati huo, msimamo wa wanachama wawili wa EAC, Tanzania na Kenya, ulikuwa ukijulikana.

Tanzania ikitaka iruhusiwe kuuza pembe za ndovu huku Kenya ikipinga suala hilo. Kenya inadai kwamba ruhusa hiyo itaongeza biashara ya vipusa.

Msimamo wa Tanzania kwenye mkutano huo ulikuwa kwamba shehena iliyopo nchini ni kubwa kiasi cha kufanya uhifadhi wake uwe mgumu kwa serikali.

Pia, Tanzania ilikuwa na mpango wa kutumia fedha zitakazopatikana katika uuzaji huo (zaidi ya Sh 20 bilioni) kwa ajili ya kufanya shughuli za uhifadhi wa tembo.

Na serikali ilikuwa na matumaini kwa vile katika miaka ya nyuma, Afrika Kusini iliwahi kuruhusiwa kuuza vipusa vyake.

Lakini mkutano wa Doha ukaikatalia Tanzania ruhusa ya kuuza vipusa vyake. Sababu kubwa zilikuwa tatu.

Kwanza Tanzania ilikuwa na shehena kubwa ya pembe za ndovu ambazo hazikujulikana asili yake. Maana ya ugunduzi huo ni kwamba pembe za ndovu zilizotoka nje ya nchi zimeingizwa nchini na kuhifadhiwa katika maghala yetu.

Pili, ilikuwapo ripoti ya utafiti iliyoonyesha kwamba asilimia kubwa ya pembe za ndovu zinazokamatwa duniani hutoka Tanzania.

Ripoti hiyo haikusema kwamba pembe zote hizo zina asili ya Tanzania, lakini hutoka maeneo mbalimbali na kupitia nchini kabla ya kusafirishwa kwenda ughaibuni.

Tatu, Kenya ilifanya kazi kubwa kuhakikisha Tanzania haipati ruhusa iliyotaka ya kuuza pembe hizo za ndovu.

Kwa hiyo, ndani ya mkutano huo wa kimataifa, ndugu wa familia moja (Kenya na Tanzania) walikuwa wakizunguka huku na kule kusambaza ‘fitna’ dhidi ya mwenzake.

Kuna maswali mengi kutoka Doha. Mtu anaweza kuamua kuzungumzia kuhusu ni kwa vipi imekuwa rahisi sana kusafirisha vipusa hivi kutoka Tanzania kuliko kutoka katika nchi nyingine yeyote duniani.

Kwamba inakuaje pembe za ndovu waliouawa nje ya Tanzania zinaingizwa na kupata nafasi kwenye maghala yetu ya kuhifadhia. Nani anayeziingiza na kwa faida ya nani.

Lakini leo sitaki kuzungumzia hayo mawili. Ninachotaka kuzungumzia leo ni kwa vipi Tanzania na Kenya zimeshindwa kuwa na msimamo mmoja katika hili.

Ndani ya EAC, kumeundwa vyombo mbalimbali ikiwamo mikutano ya wataalamu na mawaziri kuhusu mambo yanayohusiana na jumuiya.

Ilikuaje jambo hilo likashindwa kufikiwa mwafaka ndani ya vikao hivi? Ilikuaje mawaziri wa utalii wa nchi hizi mbili na pengine wa nchi nyingine wanachama wakashindwa kufikia mwafaka.

Na tangu tangazo la kufanyika kwa mkutano huo wa CITES litolewe, kumekuwapo na mikutano ya wakuu wa nchi hizo walau miwili ambayo jambo hili lingeweza kuzungumzwa na kufikiwa ufumbuzi.

Inaonekana ama jambo hilo halikuzungumzwa au mwafaka haukupitiwa. Lolote kati ya hayo mawili, basi hiyo itakuwa ishara mbaya sana kwa EAC.

Kama wakuu wa nchi za EAC wanaweza kukutana na wasizungumzie kabisa jambo kubwa ambalo lilikuwa na hatari ya kuwagawanya katika mafungu hilo ni jambo la hatari kwangu.

Lakini, kama wakuu hawa walikutana na kufikia uamuzi wa kutokubaliana kufikia kiasi cha kupambana mbele ya watu ughaibuni, hili nalo ni jambo la hatari.

Kama Tanzania itakuwa na kinyongo na Kenya kutokana na kilichotokea Doha, sidhani kama Watanzania watakubali kuwaunga mkono Wakenya katika jambo lolote kubwa katika anga za kimataifa.

Na kama Kenya imeshindwa kuiunga mkono Tanzania Doha, Rwanda inaweza kuhisi ina haki ya kupingana na Uganda au Burundi katika jambo lolote linalozihusu nchi zao katika medani ya kimataifa.

Ikishafikia hapo, sioni ni namna gani EAC inaweza kusonga mbele. Ninafahamu kwamba hata nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU) huwa na tofauti katika baadhi ya mambo.

Lakini tofauti hizo huishia ndani ya Bunge la EU au kupitia vikao mbalimbali vilivyoundiwa mfumo ndani ya jumuiya hiyo. Siku zote, nje ya Ulaya, wanachama huwa kitu kimoja.

Na, kwa maoni yangu, dhana ya kuwa na vitu kama EU au EAC ni kuwa na msimamo mmoja katika masuala makubwa na si kinyume cha hapo.

Kama kuna siri kubwa ambayo imefichuka baada ya mkutano wa Doha ni kwamba hata viongozi wenyewe wa EAC hawako pamoja.

Kama wangekuwa pamoja, aibu hii ya Tanzania kurudi kichwa chini isingejitokeza. Kama tatizo ni fedha za hifadhi ya tembo, nchi wanachama zingeweza kuibuka na dai la kutaka fedha za uhifadhi kwa sababu ya kazi kubwa ya kuhifadhi pembe hizo.

Kama wana EAC wangekuwa na mawasiliano mazuri, ni lazima wangetoka Arusha wakiwa na msimamo mmoja ambao ungewezesha umoja wao au Tanzania, walau kwa kipindi hiki, kunufaika kutokana na kuhifadhi mzigo mkubwa wa vipusa.

Ninahofu kwamba huko tuendako, si ajabu tukaanza tena kusikia matamshi ya ajabu kutoka kwa viongozi wa nchi wanachama.

Katika mazingira haya, ninaweza kumcheka mtu yeyote atakayekuja kwangu na kudai kwamba katika kizazi hiki, kuna siku tutakuja kuwa na kitu kinaitwa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Kwa kifupi, hilo haliwezekani.

0
No votes yet