Eeh, hata mimi natishiwa kifo!


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MAWAKALA wa wakubwa wametuma ujumbe mzito: Wanataka roho yangu.

Ilikuwa saa 4.40 hivi asubuhi ya Jumamosi, Juni 4, 2011 wakati nakwenda kazini, nilipigiwa simu na mtu ambaye huchukizwa na makala zangu. Nilipopokea alinijulisha nijiandae kwa kifo.

“Haloo!, haloo!” niliitikia mara mbili ili kuvuta usikivu kwa vile sauti ya mpigaji ilikuwa chini. Naye aliitikia “Haloo!” Alipohisi tunasikilizana vizuri akauliza, “Wewe ndiye unajifanya mwandishi hodari?

Kwa vile sikujua alikusudia nini, nikamjibu, “Huo ni mtazamo wako.” Kana kwamba hilo ndilo jibu alilokuwa anasubiri, akasema, “Basi jiandae kwa kifo.” Akakata simu.

Awali nilichukulia huenda alikuwa ananifanyia mzaha. Niliendelea na safari yangu. Lakini saa 5.07 ziraili huyo alinitumia ujumbe mfupi kwenye simu ili kudhihirisha hafanyi mzaha.

Ujumbe huo uliotumwa kupitia simu Na. 0652316931, unasema:
Nipo Segera, hakikisha petroli ipo ya kutosha, bastola nakuja nayo wasiliana na Hangi kwa namba 0759221096 aandae ninja za kuficha uso.

Nilijitahidi kumpigia simu anieleze nitakutana na kifo hicho lini, lakini hakupokea. Niliwapa taarifa wakubwa wangu kazini kisha nikaripoti tukio hilo kituo kidogo cha polisi Chamazi na baadaye makao makuu ya kiwilaya, Mbagala, Temeke, Dar es Salaam.

Japokuwa simu niliyopigiwa iliniambia, moja kwa moja, kuwa nijiandae kwa kifo, ujumbe huo una tafsiri mbili. Kwanza, inawezekana mtumaji alikosea jina; lakini pili ujumbe unanifanya kuwa mshirika wa uhalifu. Tafsiri zote mbili zinathibitisha kuwa tukio la kifo lipo.

Wakikosa kuniua, basi akikamatwa mmoja wao, nitajwe kuwa mshirika wao. Uhalifu wa namna hii ulifanyika Januari mwaka 2006, wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge wilayani Ulanga, Morogoro na dereva teksi wa Dar es Salaam, walipokamatwa na polisi eneo la Sinza, wakidaiwa wezi.

Wakatiwa kwenye gari la doria, wakapokonywa mali waliyokuwa nayo, halafu wakapelekwa msitu wa Pande, Mbezi Beach walikouawa kwa risasi. Asubuhi polisi wakadai wameua majambazi wanne katika tukio la kurushiana risasi.

Polisi 13 waliohusika kuwakamata, kuwapeleka msitu wa Pande na kupeleka maiti zao ‘mochwari’, wakashitakiwa. Lakini eti mahakama haikumkuta hata polisi mmoja mwenye hatia wala kula njama za mauaji. Mahakama ni kama ilisema wafanyabiashara wale ‘walijifia’ tu.

Mimi sina hakika kama naweza kujiita mwandishi hodari. Wala siwezi kujinasibu kuwa nimefikia kuandika makala zinazotishia maslahi ya wakubwa serikalini au watu wasiojali maslahi ya taifa.

Mbona wanataka kuua nzi kwa bomu? Kila siku inayopita nazidi kuwa na hofu sasa. Sababu za hofu ni uzoefu wa wahariri wa MwanaHALISI katika matukio ya kushambuliwa.

Januari 5, 2008 majira ya saa 2 usiku, Mkurugenzi Mtendaji na mwandishi wa gazeti hili, Saed Kubenea, pamoja na Mshauri wa taaluma, Ndimara Tegambwage, peke yao waliokuwa ofisini muda huo, walivamiwa na watu wasiojulikana, wakashambuliwa na kujeruhiwa. Hata kesi iliyofunguliwa na jamhuri, ilitupwa. Uzembe mwingine.

Waswahili husema mwenzako akinyolewa wewe tia maji zako. Kwa kuwa sijui nimepangiwa kifo cha aina gani na lini, Mungu abariki njama zao za kutaka kuharakisha siku yangu ya kifo.

Jambo moja la msingi, hata nikifa leo, umma hautakaa kimya, utaandamana na kusema umechoshwa na uongo, dhuluma, uonevu, ukosefu wa haki, na demokrasia.

Umma utashutumu wizi unaofumbiwa macho na wakubwa, ubadhirifu, rushwa na ufisadi. Wakubwa wajue wanachama wa vyama vyote – CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP na wasio na vyama – wote wamechoka. Tofauti ni njia wanazotumia kupinga uchovu wa serikali.

Kwamba wakati wale wa CCM wananyukana vikali ndani, wapinzani wanaandamana kuilaani serikali ya CCM iache kulea ufisadi au kutania vita dhidi ya ufisadi, kwani wanachosema sicho wanachotenda.

Mathalani, CCM wameasisi mkakati wa kujivua gamba kwa lengo la kuwatosa watuhumiwa wote wa ufisadi na kamanda wake ni Rais Jakaya Kikwete. Ndani ya CCM, anataka watuhumiwa ufisadi Andrew Chenge, Rostam Aziz na Edward Lowassa wajivue gamba, akiwa serikalini anabariki miradi ya kifisadi iliyoasisiwa na watuhumiwa.

CCM inadai Rostam na Lowassa wanahusika katika kashfa ya kuingiza kifisadi kampuni ya kufua umeme ya Richmond ya Marekani na baadaye Dowans ya Oman. Lakini Rais ameikaribisha ikulu na kuipa dole kampuni ya Symbion Power ya Marekani iliyonunua mitambo ileile iliyoingizwa na watuhumiwa walewale.

CCM wanadai mitambo hiyo chini ya jina la Richmond au Dowans ni ufisadi, lakini ilipobatizwa kwa jina Shimbonyi, samahani, Symbion Power hakuna ufisadi na ikaruhusiwa kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa. Je, huu si unafiki?

Mbinu, mikakati, kampeni na mwelekeo huu wa CCM kujivua gamba ni sawa na mtu anayechakura chooni halafu akadai hali uchafu ila anakula wadudu tu. Kama mitambo ya Symbion ni halali, CCM hawawezi kudai walioingiza awali ni mafisadi, na wakisema hivyo, mkuu wa nchi haponi.

Tazama. Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu, alipata wakati mgumu alipowasilisha mwelekeo wa makadirio ya matumizi kwenye Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu wizara anayoongoza. Alishindwa kueleza mikakati ya kufufua shirika la ndege (ATCL), reli na usafiri wa baharini.

Kamati ya Bunge ilimrejesha akajipange upya. Lakini kumbe, Rais Jakaya Kikwete alikuwa na ahadi mfukoni. Akiwa ziarani mkoani Mwanza, alisema serikali yake imeanza kuandaa mkakati maalum wa kuifufua ATCL. Halafu akatia nakshi ahadi ya kununua meli kwa ajili ya usafiri katika Ziwa Victoria.

Je, wakati Waziri Nundu anaandaa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2011/2012, hakujua kama serikali ilikuwa na mikakati maalum ya kufufua ATCL kama alivyosema rais?

Hata maelezo ya awali ya Bajeti yaliyotolewa na Tume ya Mipango, mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, uchukuzi kwa njia ya ndege na meli haumo kwenye vipaumbele vya serikali.

Mwaka 2007 serikali iliahidi kuifufua ATCL, ikamteua David Mattaka kuwa mkurugenzi mkuu na ikatoa kiasi fulani cha fedha zilizoishia kulipa madeni. Ilichofanya kingine ni kueneza uvumi kwamba ilitaka kuingia ubia wa uendeshaji na kampuni moja ya China – basi.

Mattaka amestaafu akiacha shirika mahututi na yeye akasema anaondoka akijivunia kuanzisha nembo mpya ya shirika hilo.

Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, chini ya Dk. John Magufuli ilionekana kukuna wengi na kutajwa na wabunge kama inayoweza angalau kukidhi ujenzi wa miundombinu ya barabara nyingi. Lakini anayeshikilia Fuko la Fedha Tanzania, Waziri Mustafa Mkulo amesema bajeti ya Magufuli ni ndoto.

Mgongano huu unatokea siku chache baada ya semina elekezi kwa watendaji wakuu serikalini iliyofanyika mjini Dodoma. Huko Rais Kikwete, aliyeifungua na kuifunga, aliwaambia wateule wake hao wasitofautiane katika kauli zao. Vipi wamesahau? Naomba nisife mapema nishuhudie baada ya mwaka!

0789 3838 979, jmwangul@yahoo.co
0
No votes yet