Elimu bora haitafikiwa tusipobadilika


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

CHANGAMOTO katika uendeshaji na usimamizi wa elimu hapa nchini haziishi; inapotatuliwa moja, huzaliwa nyingine au wakuu wa shule wanapojitahidi kutafutia ufumbuzi mojawapo huibuka nyingine.

Mathalani, wakuu wa shule waliokutana chini ya mwavuli wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari (Tahossa) katika hoteli ya Savoy, Morogoro Februari mwaka huu, walijadili na kubainisha changamoto kadhaa zinazochangia na zilizochangia matokeo mabaya ya wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana.

Matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yalitangazwa katika kipindi ambacho yalifanyika mabadiliko ya uendeshaji wa shule za sekondari.

Awali shule za sekondari zilikuwa zikisimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Wemu). Kwa kila tatizo, Wemu ilikuwa inahusika moja kwa moja au mwalimu, mathalani kutoka Kibondo, Karagwe, Nkasi, Mvomero au hata Ilala alilazimika kwenda makao makuu, Dares Salaam kwa utatuzi.

Baada ya kuwepo ongezeko kubwa la shule za sekondari, na kwa misingi hiyo walimu na wanafunzi, matatizo yakaongezeka. Mwaka 2008 serikali ikaamua kugatua madaraka ya usimamizi wa shule hizo kutoka serikali kuu kwenda Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (Tamisemi).

Madhumuni ya ugatuaji madaraka ilikuwa kuipunguzia mzigo wa uendeshaji wizara mama kutokana na wingi wa shule ili wizara hiyo ijishughulishe zaidi na kutunga na kusimamia sera, kuwa washauri na kusimamia elimu ya juu.

Vilevile, ugatuaji madaraka ulilenga kuziweka shule zote yaani za sekondari na za msingi kuwa chini ya mwavuli mmoja au wizara moja. Julai 2009 shule hizo rasmi zikawa chini ya Tamisemi.

Huko zimezaliwa changamoto mpya katika usimamizi wa elimu ambazo wakuu wa shule wamebaini. Tamisemi imeongezewa mzigo, kwani kila linapoibuka tatizo inatumiwa Tamisemi, na kwa hapa ni halmashauri za wilaya, manispaa na majiji.

Wakati shule hizo zikiwa chini ya Wemu zilikuwa zikipata fedha za ruzuku ambazo ziligawanywa kulingana na idadi ya wanafunzi na kiwango kwa kila mwanafunzi kilieleweka.

Hivi sasa mambo ni tofauti. Huko Tamisemi kiasi cha fedha za ruzuku kinatofautiana kutoka halmashauri moja hadi nyingine kulingana na uwezo wa mapato. Halmashauri yenye vyanzo vingi vya mapato mgawo wa fedha kwa shule hizi huwa mkubwa kuliko isiyo na vyanzo vingi.

Katika kikao hicho cha Tahossa, ambacho mgeni rasmi alikuwa Afisa elimu mkoa wa Morogoro, Fatuma Kilimia, wakuu wa shule walijadili maboresho yaliyofanywa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem). Mmem ulichangia ongezeko la vyumba vya madarasa, upanuzi wa shule na ujenzi wa shule mpya.

Kadhalika walibainisha Mmem ulivyosaidia ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi na walimu. Vilevile walieleza jinsi Mmem ulivyosababisha kubuniwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (Mmes) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu (Mmeju).

Hata hivyo, wakuu wa shule, walibainisha wazi kuwa usimamizi usioridhisha katika Mmem na Mmes umechangia matokeo ya taifa ya kidato cha nne 2010 kuwa mabaya.

Mbali na wingi wa wanafunzi madarasani, uhaba wa vifaa na walimu, sababu nyingine za matokeo mabaya ya wanafunzi mwaka jana ni alama za chini zilizotumika kuchagua wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza katika shule za serikali.

Alama zinazomwezesha mwanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza zimeshushwa hadi 100 badala ya kati ya 250 na 300. Utafiti wa wakuu wa shule unaonyesha wanafunzi wengi waliojiunga na sekondari wakiwa na alama za chini ndio wengi wao walifeli.

Aidha, walikosoa utendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta). Katika ufundishaji, wanafunzi hupewa mazoezi kila wiki, majaribio kila mwezi na mitihani kila muhula. Matokeo hayo yote hujumlishwa ili kupata wastani wa ufaulu wa mwanafunzi kwa mwaka.

Matokeo haya na wastani kuanzia kidato cha pili, tatu na nne hutumwa Necta, ili pamoja na matokeo ya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne upatikane wastani wa ufaulu wa mwanafunzi.

Kazi hii imekuwa ikifanyika miaka yote, lakini ukweli kazi hii ni ya kuchosha tu walimu, Necta wanazingatia matokeo ya mwisho tu bila kujaza wastani wa matokeo ya darasani.

Wastani wa matokeo ya mwanafunzi darasani yasipopelekewa Necta hawatoi matokeo, lakini hata matokeo hayo yakipelekwa hayajumlishwi katika matokeo ya mwisho.

Necta, kwa mtindo huu inawakosesha haki watahiniwa kwani mwanafunzi anaweza awe alikuwa akifanya vema darasani, lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kisaikolojia, akafanya vibaya siku ya mtihani.

Sasa inakuwaje mtahiniwa huyu apate sifuri wakati ana alama za matokeo ya vidato vya pili, tatu na kidato cha nne kwa muhula wa kwanza?

Hapa kuna wanafunzi walio na uwezo wa wastani, hivyo waelezwe kuwa hakuna haja ya kuwa na alama hizo na ieleweke kuwa watahiniwa wazingatie mtihani wa mwisho tu. Mifumo mingi ya elimu inahusisha alama za mazoezi, majaribio na mtihani. Inakuwaje Necta hawatambui hizo alama?

Shutuma nyingine dhidi ya Necta ni mtindo mpya ulioanzishwa wa kutunga maswali kwa kuzingatia uwezo na ufahamu. Huu ni mtindo wa maswali unaomtaka mwanafunzi ajibu kwa kutumia uelewa wake na wala si kukariri.

Mfumo huu mpya ni mzuri, lakini walimu hawakuandaliwa. Walimu bado wanatumia mfumo wa kukaririsha wanafunzi wakati Necta wanawapima wanafunzi kwa uelewa. Kama walimu hawajapata semina juu ya utunzi huu mpya bila shaka watakanganyika jinsi ya kuandaa hayo maswali.

Jambo jingine geni masikioni mwa watu wengi ni mwingiliano wa kiutendaji kati ya ofisi ya mtendaji kata chini ya diwani kwa upande mmoja na mtendaji mkuu ambaye ni mkuu wa shule. Baadhi ya maeneo mkoani Morogoro, diwani anadiriki kufanya kazi za mkuu wa shule.

Mwingiliano wa majukumu unasababisha mvutano usio na msingi na unachangia kushusha ufanisi wa elimu. Mwingiliano uko katika ujenzi wa majengo ya shule na upokeaji michango ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza. Mkuu wa shule anapobaini kutokea kwa mapungufu, ofisi ya kata inakuja juu. Kila upande ufahamu majukumu yake.

Wazazi wengi wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa watoto wao. Wazazi hawa wanashindwa kuwalipia wanafunzi wao michango iliyoainishwa na Wemu. Michango hiyo ndiyo inayosaidia kuendesha shule.

Hivi karibuni Serikali imetoa maelekeozo ya kutowarudisha nyumbani wanafunzi kwa kukosa michango. Kutokana na agizo hilo michango haipelekwi shuleni. Mzazi hutimiza wajibu huo akijisikia. Serikali iainishe njia mbadala itakayowezesha wazazi kulipa michango kwa wakati.

Mwandishi wa makala haya ni mkuu wa shule moja ya kata katika mkoa wa Morogoro. 0714261361 song’orasm@yahoo.com
0
No votes yet