Fatuma Mikidadi: Mimi si fisadi

"NIMEHANGAIKA sana. Nimelazimika kuja hadi hapa ili niweze kuweka jambo hili sawa. Kwamba mmenitaja kuwa mkurugenzi wa bodi wa kampuni ya Biashara Consumer Services Company Limited (BCS).
"Ni kweli nilikuwa huko, lakini sifahamu hicho kinachotajwa. Sijui kwamba kampuni ilichota mamilioni ya fedha. Kwa kweli hilo silijui."
Ni kauli ya mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano (Viti Maalum), Fatuma Bashehe Mikidadi, katika mahojiano yake na gazeti hili, ambapo anakana kuhusika na utafunaji wa mabilioni ya shilingi za umma.
Kampuni ya BCS ni miongoni mwa makampuni kadhaa nchini, ambayo yalichotewa mabilioni hayo kutoka katika Mfuko wa Chakula (Food Aid Counterpart Fund – FACF) unaofadhiliwa na Serikali ya Japan.
Baada ya kampuni hizo kupatiwa fedha ili kutekeleza miradi ya maendeleo iliyochaguliwa, baadhi hawakufanya hivyo na wala hadi sasa hawajarejesha fedha hizo.
Mbali na Fatuma, wakurugenzi wengine wa kampuni hiyo ni Jackson Kaale, Kandanga Muhangwa, Edmund Mkwawa, Flavian Gowele, Judith Juma, Abdul Nur Suleiman na Salome Mbatia.
Fatuma anasema mara baada ya kuona habari hiyo, aliamua kutafuta ofisi za gazeti kwa lengo la kuweka mambo sawa.
"Nilipoona habari hii, niliona hapakaliki. Nikasema lazima niwatafute ili nami nipate fursa ya kutoa maelezo yangu," anasema Fatuma kwa taratibu.
Anasema, "nimekuja hapa ili kuwaeleza kwamba mimi si fisadi. Simo humo hata kidogo. Sihusiki na kadhia hiyo. Jamani mimi simo."
Anasema awali alijulishwa jambo hilo na ndugu zake ambao walikuwa wa kwanza kupata gazeti.
"Nimekuja kuweka sawa jambo hili ili nieleweke vizuri, maana siku hizi ukihusishwa na ufisadi, jamii inakuwa ni muovu," anasema.
Anasema, "mimi nimeteuliwa tu kuingia katika Bodi hii, sikuomba? Unajua hili ni shirika la serikali. Mambo ya serikali unayajua," anasema kwa taratibu.
Je, ilikuwaje hadi wakafanikiwa kuchota mabilioni yote hayo ya shilingi bila bodi kujulishwa?
Anajibu: "Yaliokuwa yanafanyika humo, mimi binafsi sikuyajua. Tulikuwa tunasomewa tu taarifa ya mapato na matumizi. Hata mara moja, hatukuwahi kuelezwa fedha zilitoka wapi. Hawakuwahi kutukuambiwa kama walizipa kwa mkopa au vipi."
Fatuma anatoa barua inayoonyesha kwamba wakati sakata hilo linatokea tayari alikuwa amemaliza kipindi chake cha uongozi.
Inasema, "Menejimenti imepokea nakala ya barua kutoka Wizara yetu kuhusu mabadiliko haya ya Bodi kwa masikitiko.
"Hata hivyo, kwa kuwa suala hili liko nje ya mamlaka yetu, tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwako kwa mchango ulioutoa wa kuongoza Kampuni hii kwa kipindi kirefu tangu mwaka 1993," inasema sehemu ya barua hiyo 5 Juni, 2000, ambayo imesainiwa na Katibu wa Kampuni, Salome Mbatia.
Anasema, "Mipango ya kuwaaga rasmi itafanywa, baada ya kushauriana na Bodi mpya na tutawajulisheni. Kwa niaba ya Menejimenti ninaomba kuwashukuru tena, na kuwatakia kheri katika shughuli zenu."
Mbatia, tayari ametangulia mbele ya haki. Alifariki dunia kwa ajali ya gari Oktoba mwaka jana, akiwa njiani kuelekea Njombe, Iringa, kusaka kura za kumuwezesha kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Huyo ndiye aliyekuwa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo kwa mujibu wa barua ya Fatuma. Kabla ya kufikwa na mauti, Mbatia alikuwa Naibu Waziri katika wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Hakuna ajuae mchango mkubwa aliutoa Fatuma ni upi, lakini salamu hizo walipewa pia wajumbe wengine wa Bodi ya BCS.
Kumbukumbu za utoaji wa fedha za FACF, zinaonyesha kampuni za serikali zilizojulikana kama RTC (Regional Trading Company), nazo zilichotewa fedha nyingi kutoka mfuko huu. Nyingi ya makampuni haya hazikuweza kuzirejesha.
Fatuma Mwishehe Mikidadi, alizaliwa mwaka 1946 katika kijiji cha Mingoyo, Wilaya ya Lindi Vijijini, mkoani Lindi.
Alisoma shule ya Mtwara Girls alikomaliza mwaka 1967 na baadaye Chuo cha Ualimu Tabora (TTC). Hiyo ilikuwa kutoka mwaka 1968 hadi 1969.
Alianza kazi serikalini mwaka 1970 katika shule ya msingi Mingoyo, kabla ya kwenda shule ya Dodoma, Rahaleo na Pilipili, zote za mkoani Lindi.
Mwaka 1995 alijiunga na Chuo cha Ualimu Chang'ombe, Dar es Salaam, kwa ajili ya Stashahada ya uwalimu.
Mwaka 1981 Fatuma alisoma masuala ya ukaguzi wa shule mjini Bagamoyo. Wakati huo tayari alikuwa Afisa Mkaguzi wa Shule.
Mwaka 1989 Fatuma alijiunga na chuo cha CCM, Kivukoni, kabla ya kwenda nchini Szechoslovakia kwa ajili ya masomo ya siasa na uchumi.
Anasema akiwa Kivukoni, ndipo alipojitumbukiza katika siasa baada ya kuvutiwa na mijadala mbalimbali, lakini kubwa alivutiwa na sera ya CCM.
Mwaka 1993, alikwenda Harare, nchini Zimbabwe kwa kozi ya Uwezeshaji Wanawake katika uongozi. Kozi kama hiyo alichukua pia nchini Ubelgiji.
Ameshika nafasi mbalimbali za uongozi na utawala. Mwaka 1970-1981 alikuwa mwalimu, mkaguzi wa Shule (1981-1992); Afisa Elimu Vielelezo Mkoa Lindi (1992-1993); Afisa Elimu Watu Wazima Mkoa Lindi (1993-1994) na Mkuu wa Wilaya Mtwara na Lindi (1994-2006).
Amechukua pia mafunzo ya kompyuta na uongozi mkoani Morogoro mwaka 2003 na mafunzo ya wanawake na maendeleo mwaka 2004.
Hivi sasa Fatuma ni miongoni mwa wanafunzi katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) akichukua masomo ya shahada ya kwanza (Bachelor of Arts Science - BSc). Alijiunga na chuo hicho mwaka 1998.
Uzoefu wake katika siasa, umeanzia mbali: Amekuwa katibu Idara ya Huduma za Umma Mkoa (1987); Mjumbe wa NEC-CCM (1987-1994); Mwenyekiti UWT Mkoa wa Lindi (2004); Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa UWT (2004).
Mwaka 2005 aliwania ubunge kupitia Viti Maalum na kufanikiwa kuchaguliwa.
Anasema anatumia nafasi yake hiyo kuhamasisha wananchi, hasa wanawake na vijana katika vikundi kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.
Anakaribia kwenda mkoani Lindi kukabidhi baiskeli kwa walemavu baada ya kuwahakikishia kupitia ziara alizozifanya kwa pikipiki.
Anasema, "Nimepata idadi ya 200 watu wenye ulemavu ambao ni wanawake na wanaume wakiwemo watoto. Pia nina majina ya watoto 200 yatima katika mkoa wa Lindi. Hawa nimepanga kuwasaidia kwa njia mbalimbali," anasema.
Baiskeli 50 amesaidiwa na kanisa la Christian Mission Fellowship na kumi zimetolewa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) wa Mama Anna Mkapa.
Amegharamia sare za shule kwa wanafunzi 40 wilayani Ruangwa kwa Sh. 720,000 na kupitia msaada wa Shirika la SUNY of US (Marekani) amewapatia madiwani 60 wanawake mafunzo ya uongozi na utawala bora.
Pia amesadia wanawake wa wilaya ya Ruangwa wamepata mafunzo ya masuala ya ndoa na talaka, mirathi pamoja na kuandika wosia na ukimwi.
Anasema, "Nimechagua kusaidia zaidi makundi haya maana ndiyo yaliyoachwa kimaendeleo. Wanahitaji msaada kujikwamua na umasikini."
Pia amesaidia vifaa vya michezo kwa timu kumi za soka, ikiwemo inayojumuisha wanawake iitwayo Rahaleo Women FC.