Fedha za Manji zinapumbaza Yanga


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version

YUSSUF Mehboob Manji si wa kwanza kuifadhili Yanga, klabu kongwe nchini yenye utajiri wa mashabiki, rasilimali na mvuto mkubwa kwa wadau wa soka.

Kabla ya Manji anayezungumza kila wakati kwenye vyombo vya habari, walikuwako akina Mohammed Virani, Murtaza Dewji pia Abbas Gulamali. Hao wote ni Watanzania wenye asili ya Asia kama ilivyo kwa Manji.

Kila aliyefadhili kwa kipindi chake, alikuwa na dosari, hasa iliyolenga kukwaruzana na uongozi kiasi cha kuiathiri klabu hiyo kimaendeleo kwa miaka nenda-rudi.

Wakati kila mmoja alikuwa na mipango yake, Manji ana staili tofauti kidogo kwani anavaa kofia mbili kwa nguvu ya fedha.

Kofia ya kwanza ina baraka za uongozi uliopita wa Imani Mahugila Madega. Manji aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini wa klabu hiyo wakati ule ikiwa na wajumbe wawili; yeye na mama Fatma Karume.

Kwa nafasi hiyo alisumbua aligeuka kuwa msumari wa moto kwa uongozi. Aliwarushia tuhuma mbalimbali, lakini zilikosa mashiko kwa sababu malengo yake yaligundulika. Madega alisimama kidete. Ikashindikana.

Hakuna ubishi kwamba licha ya wanachama kuchagua uongozi mwingine Julai, mwaka jana, lakini ukweli unabaki kwamba Manji alikuwa na ‘mkono’ wake.

Manji ndiye aliyehakikisha wanachama wa mikoani wanafika kwenye uchaguzi. Alilipa gharama za nauli, chakula na aliwakatia tiketi kuingia kuoma pambano la kirafiki la kimataifa kati ya Taifa Stars na Brazil kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa aliyekuwa ndani ya viwanja vya biashara ya kimataifa Sabasaba, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam, ulikofanyika uchaguzi huo atakuwa alishuhudia namna alivyocheza karata apite yule badala ya huyu na ndiye alizima vurugu baada ya mmoja wa wagombea Francis Kifukwe kujitoa.

Akacheza karata yake. Akashinikiza kwamba mgombea yeyote atakayechaguliwa kuwa mwenyekiti, amteue Kifukwe kuwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini. Aliyechaguliwa ni Nchunga na akatekeleza agizo hilo kwa kumteua Kifukwe.

Hivi karibuni akajipa madaraka ya kuteua mjumbe wa nne, Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu kuingia kwenye Bodia ya Wadhamini.

Katika uhai wa miaka 70 ya klabu hiyo yenye masikani yake makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, madaraka haya ya Manji ni makubwa. Labda ka vile Yanga haina mfadhili mwingine wala miradi mizuri ya kuingiza fedha za kuendesha klabu, lakini madaraka haya ni makubwa mno.

Kwa mujibu wa katiba, wanahitajika wajumbe watano ambao wangekutana na kuteua mwenyekiti, lakini mara alipoteuliwa akajipa uenyekiti. Hata kama angekuwa amechaguliwa na wenzake, wajibu wa wadhamini wa labu si kupanga safu ya uongozi, bali kusimamia na kulinda mali za klabu pamoja na madeni.

Lakini, Manji amejiongezea kazi. Anatumia nafasi hiyo kuongoza klabu

Mwaka jana alipitisha karatasi kwa wachezaji wapige kura ni kiongozi gain alikuwa akimpinga klabuni. Akatangaza kutomlipa tena kocha na alikataa, kwa mujibu wa makubaliano na viongozi, kutoa fedha za nauli ya kwenda Lubumbashi kwa mechi ya marudiano dhidi ya St. Eloi Lupopo.

Madega alilazimika kuomba mkopo kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa makubaliano ya kulipa kidogokidogo na kulimalizia deni hilo kwa makato ya mechi dhidi ya Simba.

Manji alihakikisha Madega harudi (naye alielekeza nia yake kwenye ubunge kupitia CCM) na akahakikisha wagombea wenye mawazo ya kujitegemea hawapiti. Ikawa hivyo.

Hakuna ubishi, Manji ametoa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya maendeleo ya klabu hiyo. Lakini kwa nini hataki kuingia mkataba rasmi wa udhamini (sponsorship) ili ijulikane Yanga itarejesha kwa kutangaza bidhaa zake?

Kwa nini anang’ang’ania kumiliki nembo ya klabu na wanachama hawapewi maelezo ya kina kama huo ni mwelekeo wa kumiliki klabu?

Habari zinasema kwamba kila anachotoa, anakiandika katika rekodi zake, na wapo wanaohofia kwamba anataka kuimiliki klabu hiyo. Yakifanyika mahesabu, ikaonekana ameikopesha klabu mabilioni ya shilingi, klabu italipa vipi?

Inawezekana kwamba haya ni mawazo ya walalahoi tu, lakini kwa nini viongozi wafumbwe? Kwa nini viongozi wanaohoji wanatafutiwa njia ya kutoka?

Hakuna ubishi kwamba Yanga itashindwa kulipa deni hilo na Manji atatimiza malengo yake. Hizi fedha anazotoa kwa sasa kwa timu, matawi ya wanachama, ipo siku atazidai maana ana nyaraka zake. Hakika zitawatokea puani.

Nahisi kifo cha Yanga kwani inaelekea kupoteza hakimiliki zake zote ikiwa ni pamoja na nembo. Kuna taarifa kwamba tayari ana haki za kuanzisha kituo cha televisheni na redio huku akiwa ana gazeti ya ‘Yanga Imara’.

Kabla ya kuangalia matokeo ya huko tuendako, bila shaka kuna sababu. Wa kwanza kunyooshewa kidole hapa si idara nyingine bali ni viongozi.

Wanachama wanapaswa kukaa chini na kupata maelezo yanayotosheleza badala ya kumshabikia Manji akitimua viongozi wanaodaiwa ‘kupiga panga’ fedha anazotoa. Mwishowe watatimuliwa wanachama, na kwa kuwa viongozi wanabadilika kila uchao hatapatikana mtu wa uhakika wa kubisha kwamba klabu haijauzwa.

Walioshangilia Madega akidhibitiwa, wameshuhudia Katibu mtendaji Lawrence Mwalusako akiondoka, meneja Emmanuel Mpangala akitimuliwa na bila shaka watashangilia uongozi wa Nchunga ukifurushwa. Nini hatima ya klabu?

Katikati ya maandalizi ya mechi ya kimataifa dhidi ya Dedebit ya Ethiopia, Manji anafurusha, katibu meneja na anamkatia ‘laini’ kocha mkuu, ndiyo kazi aliyopewa? Mbona amevuka mipaka? Tusubiri matokeo ya kikao cha Bodi ya Wadhamini kinachofanyika leo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: