Fikra za Makinda na jaribio la kamati teule


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

KUNA usemi maarufu wa wahenga kwamba kila zama ina kitabu chake. Kauli hii imetumiwa kueleza sababu za watu wa vipindi tofauti kutumia mbinu na mikakati tofauti katika kutekeleza majukumu yao.

Watawala wengi wanapoingia madarakani, iwe kwa njia ya sanduku la kura au hata kwa mapinduzi ya kijeshi, au kama wimbi la nguvu ya umma ambayo imepamba moto katika miaka ya hivi karibuni, wana kawaida ya kufanya mambo kwa mikakati na hata sera tofauti na watangulizi wao.

Inaelekea Spika wa Bunge, Anne Makinda, ni mfuasi wa dhana hii ya kila zama na kitabu chake. Amesoma busara za watangulizi wake katika kujipanga na kuacha historia yake katika utawala wake.

Wiki iliyopita Makinda alitangaza Kamati Teule ya Bunge kumchunguza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo. Hii itakuwa kamati teule ya kwanza kuundwa tangu Makinda awe Spika wa Bunge.

Makinda inaonesha amepania kuacha kielelezo katika kipindi chake cha uspika. Katika mazingira ya kawaida Makinda ameonesha kukataa kuwagusa wabunge wa aina mbili; mosi, wale wote waliojijengea umaarufu, kwa kuwajibika na kuchangamsha Bunge. Hawa ni wale waliojijengea umaarufu katika Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Samwel Sitta. Makinda ameamua kuwachunia.

Kundi la pili ambalo Makinda amaeamua kuwakimbia ni wale waliohusika moja kwa moja na hoja husika kwa kuibua mjadala wenyewe kama alivyofanya Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Nishati na Madini. Shellukindo alimlipua Jairo kuwa alikuwa amechangisha fedha kutoka kwa taasisi zilizochini ya wizara yake ili kufanilisha kupitishwa kwa makadirio ya wizara yake.

Hoja ya Shellukindo ndiyo chimbuko la kadhia yote inayomwandama Jairo na hata Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ambaye amezoea mno madaraka kiasi cha kujikuta akiingiza mikono hata katika mambo asiyokuwa na nguvu nayo, na sasa naye anachunguzwa na Kamati Teule ya Bunge.

Mwingine ambaye anaingia katika kundi hili ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ambaye kimsingi ndiye alianzisha hoja ya kutaka kuwajibishwa kwa Jairo na hata Luhanjo kwa jinsi walivyofanya ‘usanii’ wa kuua hoja ya Shellukindo.

Zitto alijenga hoja kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo iliombwa na Luhanjo na kuitumia kumsafisha Jairo, ilitakiwa kujadiliwa bungeni na wabunge kwa sababu suala zima la Jairo lilikuwa la Bunge na si la utawala kama ambavyo alijaribu kuonesha Luhanjo.

Yumo pia Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, ambaye alibadilisha kidogo hoja ya Zitto kwa kupendekeza kuundwa kamati teule ili kuchunguza suala lote hilo. Kama ilivyokuwa kwa Shellukindo na Zitto, Spika Makinda pia hakumteua Sendeka kuwa mjumbe kwenye kamati teule.

Hata Zainab Vullu (Viti Maalum – CCM), ambaye alichangia mjadala wa kuundwa kamati teule, hakika naye jicho la Makinda halikumwona ili awe mjumbe wa kamati hiyo.

Makinda akiwa na nia ya kujijenga nje ya viwango na alama zilizoachwa na Sitta, aliwateua Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes; Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Mchungaji Israel Natse; Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Ramo Makani; Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Umbulla.

Katika timu hii, Khalifa ndiye mbunge pekee mkongwe, akiwa ameingia bungeni mwaka 1995 na Blandes ambaye aliingia kwa mara ya kwanza mwaka 2000, wengine wote ndiyo kwanza wanaingia bungeni.

Jambo ambalo limekuwa likisumbua vichwa vya wengi ni uamuzi wa Spika Makinda kuwachagua wabunge wengi wapya katika kamati hii. Lakini si upya tu bali pia ambao hawana makeke, hawana uzoefu wa muda mrefu wa harakati hizo. Ni vigumu kuingia katika kichwa cha Makinda kujua hasa alilenga nini.

Ni kweli Makinda anataka kujijenga kwa kutazama dhana ya kila nyakati na kitabu chake, kwa hiyo kama walivyojengwa au kujijenga akina Zitto, Sendeka na Shellukindo, angependa pia kuona wengine wakijijenga kwa fursa na nyakati zao.

Hata hivyo, pamoja na dhana ya kutaka kuandika historia yake mwenyewe kwa viwango vyake, pia yapo mambo mengine mawili hivi yanayoweza kuwa nyuma yake.

Hapa zinaibuka hoja mbili; mosi ni heshima ya Bunge kama taasisi kwa sababu kuna suala la kuingiliwa kwa madaraka yake kwa uamuzi wa Luhanjo. Kwa sura yake halisi, hili ni jambo gumu na tete kwa taasisi hii kuchunguza kesi inayoihusu na haki ionekane ikitendeka kwa uhakika.

Ndiyo maana Makinda anaamini kuwa na watu wapya, ambao hawakufungwa na hisia kali, hawana historia na ambao wanaonekana kutofungamana na upande wowote, inaweza kuwa na faida kubwa wakati wa kujadili hoja husika, hivyo kumsaidia kufikia mwisho mwema, likifanikiwa hili atajenga historia pia.

Hoja ya pili nje ya dhana ya vitabu na nyakati, ni juu ya matarajio ya umma kwa wanaochunguza na wanaochunguzwa. Hili linaathiriwa sana na historia ya kamati teule.

Mara nyingi kamati teule zimekuwa na kishindo kama kamati za Edward Oyombe Ayila, Arcado Ntagazwa, Philip Marmo, Idd Simba na Dk. Harrison Mwakyembe. Kamati teule hizi kila mmoja iliondoka na waziri kama si mawaziri pamoja na watendaji wa serikali.

Makinda ni mbunge mzoefu, ni mkongwe na aliona kamati zote hizi zikifanya kazi; alikuwako bungeni  kama mbunge au waziri, anajua moto na makali ya Kamati Teule. Haya yamo kichwani mwake na anajua matarajio ya umma juu ya maamuzi ya Bunge kuundwa kamati teule hasa katika kipindi kama cha sasa ambacho kukamiana kisiasa kumekuwa jadi ya siasa za taifa hili.

La mwisho ambalo haliwezi kukwepwa katika uamuzi wa Spika Makinda ni mtafaruku ambao chama chake kilipitia juu ya siasa za kukamiana wakati wa Bunge chini ya Sitta lilipoamua kuwasulubu watu ambao nao walijibu mapigo kupitia kwenye vikao vya chama.

Mfano mmojawapo ni pale Sitta alipoandamwa ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akidaiwa kuwa ndiye kiini cha mpasuko wa kisiasa ndani ya chama chake, kiasi cha baadhi ya wajumbe kutaka apokwe kadi. Makinda anajua vizuri madhara ya kujeruhiana kisiasa, ni kwa maana hiyo anajaribu kuratibu shughuli zake asije kujikuta katika njia ya mtangulizi wake, Sitta.

Pamoja na Spika Makinda kuyakimbia majina makubwa katika kamati teule aliyoteua, bado kuna kila uwezekano uamuzi wake ukawa mkali kama kamati zilizotangulia, hapa ndipo utakapokuwa mwanzo wa ngoma nyingine ambayo haijulikani mwelekeo wake. Tuvute subira kidogo hadi hapo Novemba 2011.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: