Fisadi kuwa rais mwaka 2015


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version
Mtazamo

WAZAZI wapendwa salaam sana.

Lengo la barua hii ni kuwaarifu kwamba mimi, mke wangu na watoto, sote ni wazima wa afya.

Pia tumefurahi kwamba tumekuwa wateule wa kuingia mwaka mpya wa 2012. Hofu na shaka yetu ni kwenu.

Lengo jingine la barua hii ni kutaka ufafanuzi wa habari nilizosikia kutoka huko nyumbani. Baba, eti ni kweli mmewapokea makada wa mtandao wa kifisadi uliotafuna uchumi wetu na kutusababisha ugumu wa maisha?

Kama ninyi wazazi na wanakijiji wote hapo Tanzania bado mnalaani mafisadi yalivyokula kodi zenu kupitia  Meremeta, Kagoda, DeepGreen Finance, EPA, migodi, umeme hadi shule kubaki kijiwe cha uhuni na kutoa elimu duni kwa watoto, imekuwaje mmewachinjia kuku kwa furaha?

Nasikia hata walioondolewa kwenye pepo ya uwaziri wanaingia kanisani ! Je, wanaungama makosa? Kama ni urais wa mwaka 2015, waambieni watubu kwanza.

Baba, yule Kuhani Mkuu alifundisha, mtu akitenda dhambi inampasa afanye kitubio, akiri makosa, aombe msamaha kwa Mungu ndipo arudishwe kundini.

Sasa hao wanaopita huko nyumbani, waliungama wapi? Kwanini waje huko na siasa za ghiliba wakati wanajua kwamba hawajasamehewa dhambi kwa kuasisi ufisadi uliosababisha watoto kufa kwa utapiamlo, akinamama kukosa huduma za afya ya mama na mwana, shule kukosa vitabu na vifaa vya kufundishia?

Baba, waambie wanakijiji wenzako; walionyang’anywa mashamba ya mpunga, kule walikopokonywa migodi na wale wazee wastaafu walionyimwa mafao yao, kwamba wakikubali ghiliba hizi wajue kwamba wanaandaa fisadi kuwa rais mwaka 2015.

Inauma, tena inauma sana kusikia mnapumbazwa kwa michango ya ujenzi wa kanisa wakati mnajua hao wanaojipitisha ndio baadhi yao wanalindwa kwa nguvu za mkubwa wao wasishtakiwe kwa ufisadi kupitia kampuni chuma ulete ya umeme! Sababu za kuwakana ziko wazi.

Kwanza, hao wanaojipitisha wanatoka Chama Cha Mafisadi (CCM) kilichowatelekeza ninyi wenye chama – wakulima na wafanyakazi. Wabunge na makada maarufu wanafisidi nchi; wanauza nyara za taifa, wanajilipa mishahara posho kubwa na kujilimbikizia mali huku madaktari na walimu wanalia njaa.

Pili, baadhi yao ndio tuliwazomea na kuwashtaki kijijini kwa kufadhili, kuunga mkono na kushiriki kulea ufisadi.

Tatu, wengine ni wale waliopambana na ufisadi lakini walipoteuliwa kwenye pepo ya uwaziri waliacha hata kuzomea mafisadi; wakaungana na waasisi wa ufisadi.

Nne, wapo wale walionyamaza kimya tusiwajue kama walikuwa wanaunga mkono au wanapinga ufisadi. Hawa hawajulikani msimamo wao.

Baba unawezaje kumwanini mtu ambaye alikataa kabisa kuonyesha msimamo wake dhidi ya ufisadi? Mtu yeyote aliyeshiriki kutengeneza mtandao wa kifisadi hataweza kuuzuia akiwa rais? Marafiki zake wote ni mafisadi atawatema vipi akiwa rais?

Kwahiyo, kama baba na wanakijiji wenzako mmezama kufikiria rais wa mwaka 2015 kutoka ndani ya CCM mjue mapema, hakuna mgombea kutoka chama hicho aliye tayari kufumua mfumo fisadi uliomlea.

Mwisho, nadhani baba ulimsikia yule Bosi Mdogo wa Bunge. Alisema ni kweli wao wamejirundikia miposho lakini akauliza, “Mnajua miposho wanayozoa sirikalini na jamaa wanaosamehe wenye hatia na kufunga wasio na hatia?” Balaa.

Maana yake ni nini? Hakuna mbunge au mwanachama anayetokana na CCM mwenye dhamiri safi ya kuondoa ufisadi kwa sababu umeanzishwa na makada wa chama hicho. CCM haifai kuaminiwa tena kutoa rais mwingine kwa sababu ni zao lilelile la kifisadi.

Wasalimie wote. Mwambie babu nitamletea ugoro.

0
Your rating: None Average: 2.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: