Fitina katika kampeni za kulinda karafuu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inayoendeshwa kwa mfumo unaoitwa wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK), inafurahia mafanikio ya kampeni yake ya kuilinda karafuu dhidi ya hujuma.

Ukimsikia waziri anayehusika na biashara, Nassor Ahmed Mazrui kwenye vyombo vya habari vya serikali, utasema kila kitu kinakwenda vizuri.

Kwamba kampeni yenyewe inapata maendeleo ya kupigiwa mfano tena kwa kasi ya mwendo wa swala wala si konokono.

Hapo nyuma katika safu hii, nilihoji mambo kadha wa kadha kuhusu kampeni hii. Niliuliza kama sasa serikali ipo tayari kuilinda karafuu?

Nikauliza pia Dk. Ali Mohamed Shein, huyu rais wa Zanzibar, ameamua kufa na wakubwa wenzake wanaotuhumiwa kuwahi kuihujumu karafuu kwa kuiuza kwa magendo?

Inajulikana wazi katika kile alichokiita “Task Force ya Taifa” baadhi ya wajumbe wake hawajasafika na tuhuma hizo. Lakini pia nilijua kama ni mtego utateguka tu.

Leo, tayari zimefika taarifa kuwa idadi ya viongozi wa ngazi ya chini wa serikali, masheha, waliotimuliwa kwa sababu ya kuhisiwa, kuwa wanahujumu kampeni ya kuilinda karafuu, imeongezeka.

Masheha wengine wawili, mbali na yule wa Mgogoni, jimbo la Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, wametimuliwa kazi.

Hiyo labda ni tisa maana masheha na viongozi wa serikali, lao ni moja, angalau mpaka ulipofanyika uchaguzi mkuu 31 Oktoba 2011. Masheha ndio waliokuwa wakitekeleza maagizo ya viongozi wa juu ambayo mara nyingi yalikuwa ya haramu kisheria.

Kubwa ni taarifa mpya kwamba Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dadi Faki Dadi kufanikiwa kuondoa askari polisi kadhaa mkoani kwake kwa kuwatuhumu kuzorotesha kampeni ya serikali.

Dadi anatajwa kuwa amewachongea askari polisi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad.

Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa kutoka ndani ya serikali na Jeshi la Polisi, Dadi amefikisha orodha ya askari na kuwataja kuwa wanakorofisha kasi ya kampeni ya kuilinda karafuu.

Taarifa ilipofikishwa Ikulu ikafuatiliwa hadi kutoa tamko la kuhamishwa kwa askari waliotajwa.

Japokuwa zipo taarifa Dadi amerudishiwa mzigo wa kutoa maelezo ya kina ya namna askari walivyohusika katika wanachotuhumiwa, tayari Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, ameamuru askari hao wahamishwe.

Harakati za askari hao kuondoka Pemba zimeshamiri. Angalau kufikia hatua hii, naambiwa tuhuma dhidi yao zaweza kuwa ni fitina tupu na matokeo ya staili ya uongozi wa RC Dadi Faki Dadi.

Hata yeye hajasafishwa tuhuma za kuhusika na biashara tata ya karafuu kama ilivyotajwa na kamati ya Ali Juma Shamhuna, ambaye mwaka huo wa 2003 alikuwa nje ya baraza la mawaziri. Hivi sasa yu ndani ya SUK.

Shamhuna, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Donge, jimbo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ambalo sehemu yake lina mikarafuu mingi vilevile, aliongoza kamati iliyotumwa na Baraza hilo kwenda Pemba kuchunguza tuhuma kuwa baadhi ya viongozi waandamizi serikalini wananunua karafuu na kuziuza Kenya kwa magendo.

Kitendo hicho ni kuvunja sheria ya serikali na adhabu yake ni kifungo cha miaka kadhaa jela pamoja na mhusika kufilisiwa karafuu alizokamatwa nazo na chombo kilichokutwa kinasafirisha.

Dadi yumo katika kikosi kabambe cha Dk. Shein kilichokabidhiwa dhamana ya kusimamia kazi ya uchumaji, uhifadhi na ulinzi wa karafuu mpaka hatua ya mwisho ya kuuzwa kwenye vituo vya Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC), wakala pekee wa serikali katika kuishughulikia karafuu.

Kwa kuwa karafuu imekuwa ikiuzwa kwa magendo hasahasa nchini Kenya, na kwa kuwa mkoa anaouongoza, Kaskazini una milango isiyohesabika ya kuingia Kenya, ana nafasi nzuri ya kusimamia yote hayo matatu – uchumaji, uhifadhi na ulinzi.

Ila milango hiyohiyo imekuwa ikitumika kufanikisha utoroshaji wa karafuu zilizokamatwa na kufilisiwa kutoka wafanyabiashara wanaosakwa kwa nguvu nyingi leo.

Karafuu nyingi zilizopata kukamatwa na polisi au askari wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) zilitajwa kuwa hazikurudishwa serikalini. Baadhi ya waliokamatwa nazo waliachiwa bila ya kushitakiwa mahakamani.

Zipo taarifa ndani ya Jeshi la Polisi kuwa wapo watu waliokamatwa katika misako wakituhumiwa kuwa katika maandalizi ya kuvusha karafuu kwenda Kenya, waliombewa msamaha na ofisi ya mkuu wa mkoa.

Mfanyabiashara mmoja wa magendo alilia sana kwenye kituo cha Polisi cha Konde arudishiwe gari lake lililokuwa limekamatwa likiwa limebeba magunia ya karafuu kavu lakini polisi walikataa.

Mgomo wao ukaishia walipoamriwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini wamrudishie gari lake. Amri hiyo ilikuwa kumkingia kifua mhalifu huyo ili asibanwe na mkono wa sheria.

Waliokuwa wamegoma ni askari polisi wakiwemo wakuu wa vituo. Kituo cha Konde kinajulikana kwa kuwa na nguvu kubwa katika kuzuia magendo ya karafuu.

Ni kituo hiki kinachoelezwa kwamba askari wake wamekumbwa na kadhia ya kuhamishwa ghafla kwa sababu ya hatua aliyoichukua RC Dadi – kuwachongea kuwa wanahujumu kampeni.

Ukweli unaojichomoza ni kwamba nguvu zilezile za kuzuia karafuu kuibwa na kutoroshwa kwa magendo walizozitumia polisi, ndiyo zilezile leo zinawafitinisha hadi kuhamishwa ghafla.

Nguvu zilezile za masheha kujitahidi kuisaidia serikali tangu wakati tuhuma zilipotoka kwamba baadhi yao wakisaidia kuhifadhi mali za wakubwa zao, ndio zilezile leo zinatumika kuwafitinisha na kusimamishwa usheha.

Sasa hii ni hatari. Tuhuma zinapotokea kwa kiongozi wa juu dhidi ya aliye chini yake, au yule ambaye hawezi kujitetea haraka kwa sababu ya mfumo mbaya wa “amri amri” kwa hawa wana ulinzi na usalama, zinahitaji kuchunguzwa.

Ukifanyika uchunguzi na ikithibitishwa kuwa aliyetuhumiwa ametenda kosa kweli, hapo ndipo hatua ya kinidhamu ikiwemo ya kumshitaki mahakamani, inasihi kuchukuliwa.

Je, masheha wametolewa ushahidi upi? Na hawa askari polisi wametajiwa ushahidi hata kuthibitika kuwa wamesaidia mipango ya waendesha magendo ya karafuu?

Hakuna kitu kama hicho. Ni tuhuma na shutuma pekee. Mbona tuhuma zile zilizothibitishwa na watu wanaoheshimika kama wawakilishi hazikutiliwa maanani licha ya kuthibitishwa?

Dk. Shein alisema wakati akizindua kampeni ya kuilinda karafuu kwamba pamoja na dhamira ya serikali katika suala hilo, hatarajii kusikia wananchi wanaonewa.

Indhari aliyoitoa rais lazima izingatiwe. Haiwezekani watumishi wa serikali wakatuhumiwa na kuhukumiwa pasina ushahidi kutolewa nao kupewa nafasi ya kujitetea. Ni kumhukumu mtumishi kumpa amri ya kuhama kituo cha kazi kwa sababu ya tuhuma. Inaingia katika kumbukumbu za utumishi wake. Ni haramu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: