Fomula ya Stars kufuzu kimiujiza


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version

JAN Borge Poulsen alianza vizuri kibarua cha kuinoa timu ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Kilimanjaro Stars ilitwaa taji hilo kwa kuilaza Ivory Coast bao 1-0 katika mchezo mkali uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Halafu akaijengea matumaini Taifa Stars ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kushinda mechi moja, kufungwa moja na kutoka sare moja. Stars ilianza kwa sare ya 1-1 na Algeria, halafu ikalambwa bao 1-0 na Morocco kabla ya kuishushia kisago Jamhuri ya Afrika Kati (CAR) cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Lakini kipigo ilichopata mwishoni mwa wiki iliyopita cha mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano kutoka CAR jijini Bangui kimefifisha ndoto ya kufuzu kwa fainali za 2012.

Taifa Stars yenye pointi nne inakabiliwa na hesabu ngumu. Fomula inayopaswa kutumiwa ni kutandaza soka ya ushindi na maombi. Kwamba Stars inapaswa kushinda mechi zake zote mbili dhidi ya Morocco ugenini na Algeria nyumbani.

Halafu, Watanzania watatakiwa kuombea miujiza itokee Morocco na CAR zinazoongoza msimamo baada ya kufikisha pointi saba zitoke sare na zifungwe mechi za mwisho.

Kwa fomula hiyo, yaani kama Stars itashinda kimiujiza mechi zake itafikisha pointi 10, na ikiwa CAR na Morocco zitatoka sare na zikafungwa mechi za mwisho, zitaishia kuwa na pointi nane. Hata ikitoka sare moja na kushinda moja, Stars inaweza kujikuta ikifuzu kwa idadi nzuri ya mabao.

Hiyo ndiyo miujiza inayosubiriwa na Stars vinginevyo, Mdenmark huyo, hatua kwa hatua atakuwa anafuata nyayo za mtangulizi wake Marcio Maximo kutoka Brazil kushindwa kuipeleka timu hiyo kwenye fainali za Afrika.

Maximo alitua nchini kwa ajili ya kibarua cha kuipeleka Stars kwenye fainali za mwaka 2008 na za mwaka 2010 na fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini. Hakufanikiwa.

Njia mbadala

Tangu ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980, kucheza fainali zilizofanyika Nigeria,  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF zamani FAT), limejitahidi kuandaa Stars ifuzu bila mafanikio.

Baada ya kuwa na uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki elfu sitini na viwanja vingine kama Amani wa Zanzibar, na CCM Kirumba wa Mwanza, TFF ishirikiane na serikali kuandaa mikakati madhubuti ya kimchezo na kiuchumi ili iombe kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika miaka sita ijayo.

Baada ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga kuwa na uzoefu wa kutosha kutokana na kushirikishwa kwenye kamati za maandalizi ya mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), anaweza kuangalia faida za kuandaa michuano hiyo.

Tanzania imeshajipima kiasi cha kutosha juu ya uzito wa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa baada ya mara kadhaa kuandaa mashindano ya Kombe la Challenge.

Andishi zuri, lenye mvuto, lenye uchambuzi wa kina juu ya faida za fainali hizo katika kusaidia kuibua vipaji vya chipukizi, kuhamasisha soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na litakaloonyesha utayari wa serikali kusaidia kufanikisha maandalizi, bila shaka litakubaliwa na CAF.

Mapema mwaka jana Tanzania ilikubali ziara ya timu ya taifa ya Ivory Coast iliyokuja nchini kwa maandalizi ya michuano ya fainali zilizofanyika Angola. Stars ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Didier Drogba.

Baadaye Juni ilitumia Sh. 3bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kampeni za mapambano dhidi ya malaria kwa ajili ya kugharimia safari ya timu ya taifa ya Brazil kucheza na Taifa Stars mechi ya kirafiki. Stars ilichapwa mabao 5-1.

Awali serikali ilionyesha utayari wake kuhamasisha wafanyabiashara wachangie mabilioni ya shilingi kwa ajili ya ziara ya Real Madrid ya Hispania kwa ajili ya sherehe za uzinduzi wa Uwanja wa Taifa uliojengwa kwa msaada wa serikali ya China.

Matukio hayo na dhamira iliyoonyeshwa na serikali kugharimia na kushirikisha jumuiya ya wafanyabiashara kuchangia ni ishara nzuri kwa wadau wa michezo. TFF inaweza kukaa na serikali kuomba wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika miaka minne baadaye. Hii ndiyo njia mbadala.

Visingizio

Tangu baada ya mwaka 1980, Stars ilipofuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali zilizofanyika Nigeria, miaka mingine yote iliyofuata imejaa shutuma kuwa serikali inahusika kudunisha ufanisi.

Mwaka 1985 wadau waliilaumu serikali kwa kujitoa kugharimia michezo japo iliendeleza mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi (Umitashumta) na ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari (Umisseta).

Tangu mwaka 1997 ililaumiwa kwa kufuta Umisseta na Umitashumta. Mwaka 2006 Serikali ya awamu ya nne ilijivua lawama kwa kurejesha michezo hiyo na sasa imeanza kushamiri tena.

Serikali pia inagharimia mishahara ya makocha wa kigeni wa michezo kama netiboli, ngumi, riadha na soka. Pamoja na mchango mkubwa wa serikali, Tanzania haijapiga hatua.

Mathalani, riadha wamevurunda katika mashindano ya Kanda ya Tano Afrika yaliyomalizika hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa; kocha wa netiboli amejipa kadi nyekundu yeye mwenyewe, na Stars ya Poulsen inasubiri fomula ya miujiza ili isonge mbele.

Serikali ya awamu ya nne bado inaweza kuangalia fomula ya kusaidia kuileta michuano hiyo mikubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

0
No votes yet