Gavana Benno Ndullu: Nia yangu kutumikia taifa, basi!


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 January 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Ana kwa Ana
Gavana Benno Ndullu

"NILIKUBALI kurejea nchini kufanya kazi hii kwa sababu kubwa tatu. Kwanza, nilitaka kutoa mchango wangu kuisaidia nchi yangu kama gavana".

“Pili, nilitaka kurejesha heshima ya BoT na taswira ya benki kwa jumla ili kuiweka mahali inapostahili. Hii inahusu pia kujenga kada mpya ya watumishi wa benki hii na mwelekeo wa kibenki nchini kwa jumla.

“Lakini la tatu, na lenyewe si dogo, ni kwamba nilikuwa na imani na Rais Jakaya Kikwete aliyeniteua kuwa gavana mwaka 2008.

“Niliwahi kufanya kazi kwa karibu na Rais Kikwete wakati alipokuwa Waziri wa Fedha na ni imani yangu hiyo kwake ndiyo iliyonifanya niache kazi nilikokuwa na kukubali kurudi nyumbani,” anasema.

Kabla ya uteuzi wake kuwa gavana wa Benki Kuu, Ndullu alikuwa miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu katika makao makuu ya Benki ya Dunia jijini Washington D.C., Marekani.

“Dhana kwamba mimi nilirejea nchini kwa sababu nilitaka kuchuma, si sahihi. Mshahara na marupurupu niliyokuwa nikilipwa huko nisingeweza kulipwa na serikali yetu.

“Achilia mbali mshahara. Kama ningefanya kazi hadi kustaafu, ningekuwa nalipwa mafao ya zaidi ya Sh. 10 milioni kila mwezi. Kwa hiyo utaona sikuja Tanzania kutafuta pesa. Nilirudi kwa ajili ya kuitumikia nchi yangu,” anasema.

Gavana Ndullu anajadili tuhuma za kuishi kwenye jumba linaloitwa la kifahari la thamani ya Sh. 1.4 bilioni linalodaiwa kujengwa na BoT kwa ajili yake.

“Kwanza niweke wazi kwamba sikuagiza ujenzi wa nyumba hiyo. Wakati nilipoanza kuwa gavana, tayari mpango wa ujenzi wa nyumba hiyo ulikuwa umepitishwa.

“Kwa hiyo mimi nilipokuja kazi yangu ilikuwa ni kuhakikisha sheria zote, hasa ile ya Manunuzi ya Umma (PPRA), zinafuatwa kuanzia kutangaza zabuni hadi kushinda tenda.

“Lakini naomba niweke baadhi ya vitu wazi. Kwanza, kabla sijahamia kwenye nyumba hiyo mpya, nilikuwa naishi kwenye nyumba ya kupanga iliyokodishwa na BoT ambayo haikuwa kama hii ya sasa. Kama mimi ningekuwa nachagua nyumba nisingekubali kukaa pale.

“Pili, mimi nina nyumba binafsi kama hii mpya ya BoT kule Washington. Na hii si siri. Kama ingekuwa taabu yangu ni kukaa pazuri, ningekaa kwenye nyumba yangu Marekani bila ugomvi na mtu.

“Hata hapa Dar es Salaam nina nyumba yangu nzuri tu kule Mbezi na ningeweza kuishi bila tatizo. Lakini Mbezi ni mbali na nilikuwa natumia karibu saa tatu njiani kwa siku; kwenda ofisini na kurudi kabla sijahamia kwenye nyumba hiyo ya kupangiwa na BoT.

“Zaidi ya kutumia muda mwingi njiani, usafiri huo pia ulikuwa ni hatari kiusalama kwangu. Mimi ni Gavana wa BoT na kuwa barabarani kwenye foleni na kwa wakati huo, ni hatari kwangu na kwa nchi. Huo ndio ukweli.

“Halafu, nyumba niliyokuwa nimepangiwa na BoT ilikuwa inalipiwa dola 7,000 kwa mwezi. Maana yake ni kwamba baada ya miaka 10, benki itakuwa imelipa fedha sawa na thamani ya nyumba hii mpya. Hii si nyumba ya Profesa Ndullu, hii ni nyumba ya gavana wa BoT hata miaka 100 ijayo,” anasema.

Katika mazungumzo hayo na Ndullu yaliyodumu kwa saa moja na dakika 34, gavana alisema yeye si mgeni kwa vitendo vya kuchafuana, fitna na majungu katika sehemu za kazi.

Alisema katika sehemu nyingi alizowahi kufanya kazi, alikumbana na mambo mengi na kuongeza, “Kitu kinachonishtua hivi sasa ni kwamba watu wameamua kuchafuana kupitia vyombo vya habari. Hili sikuwahi kukumbana nalo.”

Anasema miongoni mwa changamoto kubwa alizokumbana nazo wakati alipoanza ugavana ilikuwa ni ukweli kwamba wengi wa watumishi waandamizi wa BoT wanakaribia kustaafu na hivyo benki inahitaji kujiandaa kwa hilo.

“Kwa hiyo hapa kuna changamoto ya kukabiliana na hili na pia kuingiza damu mpya ambayo itaiendesha benki katika dunia ya sasa na ijayo. Hii ni kazi inayohitaji kuwa makini,” anasema.

Anazungumzia vipi kuhusu tuhuma za yeye kuanzisha mpango wenye utata wa kuwakopesha wafanyakazi wa BoT mamilioni ya shilingi kwa ajili ya mikopo ya nyumba?

“Ni kweli mpango huo upo. Lakini kuna vigezo na masharti ambavyo vimewekwa kwa ajili ya wote wanaotaka kupewa mikopo hiyo. Wale ambao hawana sifa hawatapata mikopo.

“Benki yetu haipati ruzuku yoyote kutoka serikalini. Fedha tunazokopesha wafanyakazi wetu ni fedha zetu wenyewe na kuna bima maalumu kwa wanaokopeshwa, kiasi kwamba benki haitapata hasara.

“Hivi sasa tuna akiba ya Sh. 794 bilioni. Hivi kuna ubaya gani kuwakopesha wafanyakazi wako fedha zao ambazo watazirudisha kwa faida? Hivi wafanyakazi wa BoT hawatakiwi kujenga nyumba?” anauliza.

Ndullu anasema ana imani maneno yote mabaya yanayoenezwa dhidi yake binafsi na BoT kwa ujumla, yana lengo la kumkatisha tamaa yeye na wafanyakazi wa benki hiyo, lakini akasema hatakata tamaa.

“Ninafahamu kwamba kuna watu walikuwa wanafaidika na mapungufu yaliyokuwapo BoT siku za nyuma na ambayo tunajitahidi kuyaondoa.

“Na ukaguzi katika baadhi ya maeneo bado unaendelea. Pengine wanahofu tutabaini makubwa zaidi kuliko yale yaliyokwishafahamika. Lakini sisi tutaendelea na kazi na Mungu atatutangulia,” anasema Ndullu.

Kuhusu hali ya uchumi nchini na mafanikio katika BoT tangu alipoingia madarakani, Ndullu anasema hadi sasa ameridhishwa na maendeleo yaliyopatikana.

“Unajua nilianza ugavana wakati mambo yale ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) yakiwa yamepamba moto na tukasema tutatoa ushirikiano. Nadhani hilo limefanyika.

“Pia kipindi changu kiliendana na anguko kubwa la uchumi duniani ambalo liliathiri nchi nyingi duniani, zikiwamo baadhi ya nchi jirani.

“Kulinganisha na baadhi ya wenzetu, nafikiri tumefanya vizuri kidogo katika kuilinda nchi yetu dhidi ya anguko la uchumi. Tanzania ilikuwa na kiwango cha chini kabisa cha mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki wakati wa kilele cha anguko hilo,” anasema.

“Wakati nilipoanza ugavana, akiba ya nchi ya fedha za kigeni ilikuwa dola 2.5 milioni lakini sasa imefikia dola 3.5 milioni. Hiki si kiasi kidogo kwa nchi zetu masikini.

“Pia akiba yetu ya ndani sasa imefikia Sh. 794 bilioni. Wakati nilipoingia ilikuwa Sh. 330 bilioni. Nafikiri haya ndiyo mambo ya kuzingatia,” anasema.

Profesa Ndullu ni miongoni mwa wachumi wanaoheshimika barani Afrika na amefanya kazi serikalini na katika mashirika mbalimbali ndani na nje ya nchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: