Haki za binadamu ziheshimiwe
HAKI za binadamu bado haziheshimiwi kwa kiwango kinachostahili nchini. Kwa hali inavyoendelea, ni kama watawala hawataki kusikiliza sauti za wanaotaka haki hizo zitekelezwe.
Watoto hawa hawapati huduma muhimu: Chakula, makazi bora, tiba na elimu. Wala hawana mtetezi.
Kwa mfano, siku chache baada ya serikali kutangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba, tayari kunaibuka taarifa za baadhi ya wanafunzi kukabiliwa na kikwazo cha kujiunga na elimu ya sekondari.
Sababu ni uhaba wa madarasa. Kwamba serikali imeshindwa kupanga mipango endelevu ya kuwahakikishia watoto waliomaliza darasa la saba fursa ya kuendelea na masomo yao ya sekondari.
Wengine wanashindwa kutimiza ndoto walizonazo za kupata elimu hadi ya chuo kikuu kwa sababu ya mfumo mbaya uliowekwa na serikali.
Mfumo ulioandaliwa tangu mwaka 2006 – wa kuwakopesha – umekuwa na urasimu; unavunja moyo badala ya kuwajenga imani na umeibua tatizo la ubaguzi miongoni mwao.
Wale wenye watu wa kuwasaidia wanapitisha ushawishi wao kwenye Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kufanikiwa kuwapatia fedha. Wasiopenya hapo, wanaadhirika.
Watanzania wanaoishi maeneo ya vijijini, wanaporwa ardhi ambazo wamekuwa wakitumia tangu mabibi na mababu zao enzi na dahari.
Wananyimwa haki ya kutumia ardhi wanayoitegemea huku unyang’anyi huo ukiendelea kwa kasi chini ya kisingizio cha “uwekezaji.”
Serikali imekuwa ikilalamikiwa kwa watendaji wake kutotimiza wajibu katika kutumia raslimali za taifa – zikiwemo fedha za umma – kwa nidhamu na hivyo kuzorotesha kampeni ya kutokomeza umasikini.
Kutoweka kwa nidhamu katika matumizi ya raslimali za nchi kumeibua uovu mkubwa wa rushwa na ufisadi na matokeo yake ni kuwajenga wananchi hasira isiyokwisha dhidi ya serikali yao.
Utumishi wa umma unaojali uadilifu na nidhamu umepotea na kinachoonekana kushamiri kwenye sekta ya umma, ni utumishi usio adilifu na hivyo kuchochea kuwanyima wananchi haki yao ya kutumikiwa vizuri na serikali.
Haki za binadamu zimezorota. Kila kukicha kunasikika taarifa za wananchi wa sehemu fulani ya nchi kunyimwa haki hii au ile na wakati mwingine wananyimwa kwa njia za kikatili.
Wakati Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya haki za binadamu inahitaji kutafakari tatizo la uadilifu kupotea na kupelekea haki za watu kunyongwa ovyo. Lazima tubadilike.