Hakuna ukabila CHADEMA - Muslimu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Muslimu Haiderally Hasanali

HANA jina kubwa. Lakini ni mmoja wa wanasiasa wanaoamika ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Ni Muslimu Haiderally Hasanali.

Ndani ya CHADEMA, Muslimu ni mjumbe wa Bodi ya Wadhamini tokea mwaka 2003 akiwa na jukumu la kulinda mali na rasilimali nyingine za chama.

Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, Muslimu amechaguliwa na Kamati Kuu (CC) ya chama chake kuwa katibu wa kamati ya kutafuta fedha za kampeni.

Mwenyekiti wa kamati ya kutafuta fedha za uchaguzi wa CHADEMA, ni mbunge wa Viti Maalum na mkurugenzi wa Rasilimali wa chama hicho, Suzana Lyimo.

Katika mahojiano yake wiki hii na MwanaHALISI, Muslim (26) anasema amepania kujitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini katika uchaguzi mkuu ujao.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Muslim kuwania ubunge katika jimbo hilo. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, akiwa ndiyo kwanza ametimiza umri wa miaka 22 alikuwa miongoni mwa wagombea wa ubunge katika jimbo hilo. Hakubahatika kushinda.

“Mwaka 2005 mimi ndiye niliyekuwa mgombea ubunge mwenye umri mdogo kuliko wote hapa nchini. Bahati mbaya sikushinda. Uzoefu nilioupata ndiyo itakuwa silaha yangu mwaka huu endapo chama changu kitanipitisha kuwania jimbo hilo,” anasema Muslim kwa kujiamini.

Anasema CHADEMA ni chama chenye nguvu kubwa mkoani Kigoma kuliko vyama vingine vyote, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ndiyo maana anaamini kina nafasi kubwa ya kufanya vizuri mwaka huu.

Akizungumzia jimbo lake la Kigoma Kusini, Muslimu anasema hivi sasa nguvu imehamia kwa CHADEMA badala ya NCCR-Mageuzi kama ilivyokuwa zamani.

“Pale Kigoma Kusini, NCCR Mageuzi ilikuwa na nguvu sana. Lakini hivi sasa na hasa baada ya Kiffu Gulamhussein Kiffu alipokuwa mtu wao. Kuhamia kwake na kurejea CCM miaka michache iliyopita kumewavunja moja watu wengi,” anasimulia Muslimu.

Anasema, “Kutokana na hali hiyo, Watanzania sasa wanategemea makubwa kutoka kwetu (CHADEMA). Wana imani na CHADEMA kwa vile wanajua mgombea wa chama hiki hatawasaliti kama alivyofanya Kiffu.”

Anasema kinyume cha dhana kwamba CHADEMA mkoani Kigoma ilikufa baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, Dk. Amaan Walid Kabourou, chama hicho kimeimarika zaidi.

Kabourou alikuwa kiongozi wa kitaifa wa CHADEMA kwa hiyo kuondoka kwake kulitushtua kidogo. Hata hivyo, tulijipanga na sasa CHADEMA kina nguvu kuliko ilivyokuwa enzi za kigogo huyo ambaye sasa ni Mbunge wa Afrika Mashariki.

Kwa kuthibitisha hoja yake hiyo, Hassanali anatoa mfano wa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana ambapo CHADEMA kilipata 12 kulinganisha na nane vya CHADEMA.

“Jambo zuri ni kwamba hata katika baadhi ya maeneo ambayo NCCR ilishinda, sisi tuliwaunga mkono. Kama maelewano yetu na NCCR yataendelea hata wakati wa uchaguzi mkuu, tutachukua jimbo hili bila shida,” anasema.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, jimbo la Kigoma Kusini lilinyakuliwa na Kiffu Gulamhussein. Alivuliwa ubunge wake na mahakama baada ya Manju Msambya kufungua kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Tabora.

Kwa sasa, jimbo hilo linashikiliwa na Msambya (CCM) ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2005 alipata kura 35,000 miongoni mwa kura 72000 zilizopigwa.

Hassanali anasema kama vyama vya upinzani vingeungana mwaka 2005, mgombea wa upinzani angepata kura 37,000, kiasi ambacho kingetosha kutwaa nafasi hiyo.

“CHADEMA tunapenda ushirikiano wa vyama vya upinzani. Tayari tulijua kwamba Kiffu ana mpango wa kuhamia CCM. Ndiyo maana tukasema vyovyote itakavyokuwa sisi tutasimamisha mgombea,” anasema.

Hassanali anasema kwamba Tanzania inahitaji kuwa na Bunge lenye idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama vya upinzani ili nchi iende vizuri.

Anasema katika hali ya sasa ambapo asilimia 86 ya wabunge wanatoka CCM, ni vigumu kwa upinzani kushinikiza kufanyika kwa mabadiliko muhimu kwa vile chama tawala kinakwamisha.

“Napenda kutoa wito kwa Watanzania kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu, wanatakiwa kuchagua wabunge wengi iwezekanavyo kutoka vyama vya upinzani ili nchi yetu iendelee,” anasema.

“Mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Kamati Kuu ya chama,” anasema Muslim Hassanali.

Bodi ya Udhamini ya chama hicho ina mamlaka makubwa ikiwamo kumvua madaraka Mwenyekiti wa chama hicho, lakini Hassanali anasema hakuna mchaga yeyote katika bodi hiyo.

Anasema CCM imesababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi. Kuna kitu kimoja cha msingi ambacho wananchi wanapaswa kukifanya.
CHADEMA ni chama mbadala. Katika hali hiyo, anasema amedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli.

“Kama nitafanikiwa kushinda, nitaweka msingi mema wa mambo,” anasema.

Akizungumzia madai ya ukabila ndani ya chama chake, Muslimu anasema “kama kungekuwa na ukabila ndani ya CHADEMA kama kinavyodaiwa na CCM, mimi nisingefika hapa nilipo. Ningebaguliwa mapema.”

Anasema, “Mimi nisingechaguliwa katika Bodi ya Wadhamini. Lakini leo niko hapa na nimeingizwa katika kamati nyeti ya kutafuta fedha. Hakuna ukabila pale, hicho kinachosema ni porojo za CCM.”

Anasema ndani ya CHADEMA kila mwenye sifa anapewa nafasi ya kuongoza, bila kujali dini, kabila au jinsia.

“Angalia mimi, nina umri mdogo. Ni Mha wa Kigoma lakini mwenye asili ya kihindi. Bado changu kimeniamini na kunipa madaraka yote hayo,” anasema.

Muslimu Hassanali alizaliwa 27 Septemba 1973 mkoani Lindi. Alipata elimu yake katika shule ya Mama Clementina iliyopo mkoani Kilimanjaro.

Wakati huo, wazazi wa Hassanali walikuwa wakiishi mkoani Lindi ingawa babu yake ni mzaliwa wa kijiji cha Simbo kilichopo katika jimbo la Kigoma Kusini.

Ana shahada ya juu katika masuala ya Kompyuta aliyoipata nchini India.

Alijiunga rasmi na CHADEMA mwaka 2002 na mwaka 2003 akateuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya mkoa.

Mwaka 2004 aliteuliwa kuwa mjumbe wa CC nafasi anayoishikilia hadi sasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: