Hali ya uhalifu, Kikwete alipaswa kukaza maneno zaidi

MIONGONI mwa mambo aliyozungumza Rais Jakaya Kikwete wakati wa hotuba yake ya kuaga Bunge Ijumaa iliyopita ni kuvishukuru vyombo vya usalama kwa kudumisha amani, utulivu na ulinzi wa mipaka yetu.
Alisema utendaji wa vyombo vya usalama—kwa maana ya majeshi ya ulinzi na Jeshi la Polisi—umefanikisha kutimia kwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais alisema: “Uhalifu, hasa wa kutumia silaha, bado ni changamoto kwa usalama wa watu wetu na mali zao. Tulipoingia madarakani tulikuta wimbi kubwa sana la uhalifu, na nikaahidi hapa Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi watambe. Jeshi la Polisi lilifanya kazi kubwa kututoa katika wimbi lile la uhalifu. Uhalifu upo, lakini sio kama ilivyokuwa wakati ule.
“Jeshi letu linaendelea kudhibiti kuzagaa kwa silaha na kukusanya taarifa za uhalifu na wahalifu na kuvunja mitandao yao. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuiwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Na siku hizi, tofauti na mwaka 2005, tukio likitokea haichukui muda mrefu wahusika kutiwa nguvuni na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria. Napenda kulipongeza jeshi letu la polisi kwa kazi nzuri.”
Kimantiki aliyosema Rais ni ya kweli, hakuna ubishi kwamba Desemba 2005 na hasa mwanzaoni mwa mwaka 2006, hali ya ujambazi mkubwa wa kuvamia mabenki, kupora kwenye vituo vya mafuta tena mchana kweupe ulikuwa mkubwa.
Kweli kuna juhudi kubwa zimefanyika kuzima mirindimo ya kiwango kile, kwa maana hiyo si vema wala haki kusema kwamba hakuna kilichotendeka kwa miaka karibu mitano sasa.
Kwa hiyo pamoja na mlolongo wa mafanikio aliyoeleza Rais kwenye hotuba yake iliyokuwa ya kutathmini ile aliyofungulia Bunge Desemba 30, 2005, ni kumdhulumu kusema hana alichotekeleza; muungwana ni vitendo, tunapongeza aliyofanikisha.
Lakini wakati huo huo tukiwataka kukaa chonjo na changamoto ambazo bado zinakera wananchi.
Si nia ya uchambuzi huu kuangazia mafanikio yote, lakini leo nijikite tu kwenye suala la ulinzi na usalama. Hapa ninazungumzia zaidi kuhusu ulinzi wa maisha na mali za raia ukiwa ni wajibu namba moja wa Jeshi la Polisi.
Kwa takriban mwaka mmoja sasa, hasa miezi ya karibuni katika Jiji la Dar es Salaam, kidogo kidogo tumeshuhudia kuzorota kwa hali ya usalama hasa kwa wakazi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa katikati ya jiji.
Siku hizi ni nadra sana kupita siku bila kusikia kwamba majambazi yamevamia nyumbani kwa mtu, yakaua na kupora mali. Matukio haya yamekuwa mengi na sasa hakuna ubishi yanatisha mno.
Mlolongo wa mauaji haya ni mkubwa na unatisha. Kwa mfano, wakazi wa maeneo ya Kimara, Mbezi Luis, Mbezi Juu, Salasala, Segerea kutaja kwa uchache tu, wanatambua nini maana ya kurejea kwa ujambazi kwa kasi.
Wote tunakumbuka kwamba kiwango cha ujambazi kilichofikiwa wakati wa IGP Omar Mahita kilikuwa cha kutisha. Lakini ukweli ni kwamba kilifikia hapo kwa sababu nyingi, moja ni kukua kidogo kidogo kama ambavyo sasa mwelekeo unaonyesha, na mwisho wa siku hali ikawa mbaya kweli.
Tofauti na nyakati za IGP Mahita, Jeshi la Polisi limewezeshwa zaidi, zimebuniwa mbinu mpya zaidi kama vile kuundwa kwa kanda za kipolisi katika maeneo korofi kwa uhalifu kama ilivyo Dar es Salaam na wilaya za Rorya na Tarime mkoani Mara, nia ikiwa ni kupambana na uhalifu.
Kuna misaada mingi sana imekuwa inatolewa na wananchi katika dhana ya polisi jamii; kama vile vyombo vya usafiri, zikiwamo pikipiki, kwa nia ya kufanikisha uharaka wa askari polisi kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kufualitia usalama wa raia.
Kwa mfano, wapo askari wa Kikosi cha Kuliza Ghasia (FFU) wanaotumia pikipiki wakishika doria mitaani. Hawa pamoja na kusaidia kuhakikisha kwamba sheria za usalama barabarani zinafuatwa, pia wapo kwenye doria kwa maana ya kuwa maeneo tofauti ili kuwa tayari kuitikia mwito wowote wa matukio ya uhalifu.
Kwa mfano, katika matukio ya ujambazi yakitokea katika mitaa ya pembezoni mwa jiji, askari hawa kwa sababu ya kuwa na usafiri rahisi zaidi, yaani pikipiki, ilidhaniwa wangekuwa wepesi zaidi kufika katika maeneo hayo. Nina hakika wananchi ni mashuhuda kuwa askari hawa hawajawa na msaada mkubwa katika eneo hilo la mwitikio wa haraka kukabilia uhalifu.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba kuna kila dalili baadhi ya askari hawa, FFU, ambao awali walionekana kuwa walinda usalama wasiokuwa na suluhu na yeyote, siku hizi wanaonekana mitaani wakijadiliana na watu wanaodaiwa kuvunja sheria kwa njia moja au nyingine na mwisho wa siku ‘wanamalizana’ mitaani na sheria inakuwa imepindishwa.
Kwa nini ninatoa mfano wa polisi wa doria wa pikipiki katika hoja ya kuanza kukomaa kwa uhalifu, ni kwa sababu nia ya kuwaweka mitaani ni kubadili mwenendo mzima wa kukabili uhalifu.
Lakini kama wahusika wanabadili mwelekeo katika kufikia malengo ya wao kuwapo mitaani na si kambini tena kama ilivyozoeleka, basi nao wanastahili kubebeshwa sehemu ya lawama ya kwa nini ujambazi unazidi kurejea kwa kasi.
Mwalimu Nyerere alisema kwamba watu wana hulka ya kutokusahau mambo yao; ndiyo maana ukabila na udini ni mambo yanayoogopwa sana, kwa sababu mtu akibanwa kidogo na hali fulani ni rahisi sana kukimbilia ama kwenye kabila lake au dini yake. Hii ni hulka na kuibomoa ni lazima kazi ya ziada ifanyike.
Vivyo hivyo, utamaduni wa kutokuwajibika katika jamii hujengwa kwa miaka mingi sana, watu hudhani kwamba kutokuwajibika ni sehemu ya maisha yao, hapana shaka ndiyo maana watu hukataa mabadiliko kwa sababu wamezoea kufanya kazi hivi na si vile, ukiuliza kwa nini unapinga njia mpya na mbinu mpya, jibu ni jepesi mno, ‘tumezoea kufanya hivi’ hata kama hana sababu ya mazoea haya.
Kwa upande wa walinda usalama wetu, yaani Jeshi la Polisi, hata pale uongozi wa juu unapobuni mbinu na mikakati mipya na ya kisasa namna gani; hata pale wanapochukua hatua za kuwashirikisha raia (polisi jamii), kama utamaduni ulioachwa kuwa sehemu ya utendaji wa baadhi ya askari polisi hautabadilika, kuna kila sababu ya uhalifu kumea na kukomaa kwa haraka hata pale ambapo ulikuwa umekatwa.
Ndiyo maana tunasema ingawa ujambazi hautikisi katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kweli unatikisa pembezoni, na kwa bahati mbaya zaidi huko pembezoni ndiko wanakoishi wakazi wengi wa jiji.
Hili halina ubishi. Ukubwa wa msongamano wa magari katika barabara kuu zinazoingia na kutoka katikati ya jiji ni kilelezo tosha kwamba wananchi wengi wanaishi wapi.
Kwa maana hiyo kuyadhibiti majambazi katikati ya jiji na kuyaacha yakiwanyima usingizi wananchi kwenye makazi yao, si sawa na ni haki kabisa kusema kuwa uhalifu ni tatizo kubwa ambalo bado linakabili taifa hili.
Ni kwa maana hiyo, pamoja na kutambua mafanikio yaliyofikiwa na vyombo vya usalama kupunguza lile wimbi la uhalifu la mwishoni mwa miaka 2005 na mwanzoni mwa miaka ya 2006, tunajawa na hofu zaidi sasa kuwa tunarejea kulekule tulikokuwa. Kwa hali hii tunataka kauli kali na maneno mazito zaidi kuelezea hali hiyo.