Hapa ndipo JK na Ridhiwani walipokosea


Rogath Masawe's picture

Na Rogath Masawe - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Wazo Mbadala
Ridhiwani Kikwete

HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kumtumia mwanawe, Ridhiwani Kikwete, kumtafutia wadhamini ili awanie urais kupitia CCM ilikuwa ni makosa.

Nilishangazwa na kauli za viongozi wa juu wa chama tawala walipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wiki iliyopita na kudai kwamba hatua hiyo haikuwa na mgogoro wowote.

Kwa wale wanaojua namna utaratibu huo mzima ulivyoendeshwa, wanajua kwamba kuna mgogoro mkubwa katika uamuzi huo wa rais.

Na mgogoro ninaotaka kuuzungumzia mimi si ule wa kusema kwamba kumtumia mwanaye kunamaanisha hawaamini viongozi wenzake.

Mgogoro wangu mimi si ule ambao vyombo vya habari vinajaribu kuujenga kwamba kumtumia mwanaye ni vibaya. Mimi ninapingana na hilo.

Uamuzi wa Kikwete kumtumia mwanaye hauna tatizo lolote. Yeye ndiye atakayewania urais na anahitaji mtu anayemuamini kumsimamia katika zoezi hilo la kutafuta wadhamini.

Kama imetokea kwamba yeye anamuamini zaidi mtoto wake kuliko mtu mwingine yeyote hilo ni suala lake binafsi. Kila mtu ana mtu anayemuamini zaidi.

Labda niulize jambo moja. Kama mtu hawezi kumuamini mtoto wa kumzaa mwenyewe, anaweza kumuamini nani mwingine?

Tatizo langu na hatua hii ya Kikwete linakuja kwenye ukweli kwamba miongoni mwa wajumbe wa kamati ya kumtafutia wadhamini ni Benno Malisa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Kamati hiyo inaongozwa na Ridhiwani ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM. Maana ya uteuzi huu ni kwamba Ridhiwani anamtuma Malisa kwenye kamati hii.

Hili nafikiri ni tatizo. Malisa ni bosi wa Ridhiwani katika chombo kikubwa kama UVCCM. Kama mtoto huyu wa rais anaweza kumtuma Malisa katika mambo haya ya sasa, anaweza pia akamtuma kufanya mambo mengine ndani ya umoja wa vijana.

Haiwezekani kwa mtu mwenye wadhifa mkubwa kama Malisa (kumbuka UVCCM haina Mwenyekiti kwa sasa na hivyo Malisa ndiye bosi kwa sasa) kutumwa na mtu aliye chini yake katika mazingira yoyote.

Halafu hapa linakuja suala lingine la kimaadili, kama Benno anamtafutia wadhamini JK, itakuaje atakapojitokeza mtu mwingine ndani ya CCM akitaka kushindana na Kikwete?

Je, hatua hii ya Malisa haiwezi kuonyesha kwamba tayari UVCCM imetangaza kumuunga mkono mgombea mmoja ndani ya chama jambo ambalo si sahihi?

Ninachofahamu mimi ni kwamba lengo la Kikwete kumtumia mwanaye lilikuwa ni kuhakikisha hatumii viongozi wa chama katika mambo yake. Uteuzi huu wa Malisa unaleta picha mbaya.

Unaleta picha kwamba tayari UVCCM inamuunga mkono Kikwete katika kipindi ambacho wanachama wote wa CCM wanatakiwa kuwaunga mkono wagombea wake wote wanaojitokeza kwa sasa.

Kuna ushahidi pia kwamba katika baadhi ya mikoa ambako fomu hizo zimepelekwa, viongozi wa UVCCM wa mikoa husika ndiyo waliosimamia zoezi hilo. Hili ni tatizo.

Ni vema viongozi wa CCM, akina Yusuf Makamba na Pius Msekwa, wakawa wakweli kwa chama na wanachama wao na kueleza kwamba kinachofanyika ni makosa.

Nimeyasema haya kama mwana TANU na mwana CCM ambaye nimewahi kuapa kwamba; Nitasema kweli Daima, Fitina Kwangu Mwiko.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: