Hasira zako Dk. Shein, ni hasara kwako


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ni dhahiri amepandwa na hasira. Naona tayari “watu wake” wamemlisha fitna.

Inawezekana kweli amechukizwa kubaini kundi kubwa la wananchi wa Zanzibar limepata hamasa ya namna ya kuja kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Katiba ya Tanzania au kuikwepa wasiione.

Wapambe watakuwa wamempa taarifa sizo. Na desturi inaonyesha mtu alopewa taarifa za uongo na kuziamini kwa kuwa waliompa ni “watu wake” anaowaamini, hujenga hasira.

Sasa rais amepandwa na hasira. Nimethibitisha kwa matamshi yake alipokuwa kwenye hafla ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – katika kijiji cha Koani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Wakati nilipokuwa naandaa makala hii, pembeni yangu alikuwepo jamaa yangu mmoja kutoka Fuoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, aliyekuja kunisalimia ofisini, akanihoji, “Mbona unasema hafla ya chama chake wakati taarifa nilizosoma zimeonyesha rais alikuwa katika ziara ya kiserikali akizuru mikoa yote ya Zanzibar na alianzia kisiwani Pemba.”

Sasa niseme sina hakika ziara yake ni ya kiserikali au ya kichama. Sikupata mtu wake ili kuthibitisha jambo hili. Angalau katika moja ya picha nilizoziona kupitia vituo vya televisheni vya Dar es Salaam, nimeona wanaokuwa chini yake ni wakuu wa mikoa zaidi ya ilivyo wenyeviti wa CCM wa mikoa anamopita.

Lakini hiyo si mada leo. Akili yangu imenielekeza katika kile ninachokiona kama matokeo ya watu wa Dk. Shein kumpotosha rais, na sasa kukuta tunaye rais aliyejaa hasira rohoni.

Tatizo la hasira, ni kwamba mtu mzima anapokasirika hata watoto watagunduwa haraka atakapojitokeza kwao. Wananchi wa Unguja na Pemba, tayari wanajua “baba yao” – Rais Dk. Shein – amekasirika.

Sikiliza anachokisema Dk. Shein: “Naelewa fika kuna watu wanaoleta mambo ya ajabu ajabu lengo lao likiwa ni kuvuruga amani tuliyonayo.”

“… lakini nasema tena, maana nimeshasema hakuna mwenye ubavu wa kuivunja amani ya Zanzibar na kama mtu kachoka na amani iliyopo, ahame hapa hapamfai; atafute sehemu nyingine akaishi.”

Rais akamalizia, kauli ambayo naifananisha na alichowahi kukisema rais mstaafu mmoja mwaka aliokuwa anatafuta ridhaa ya mara ya pili ya uongozi. Alitaja “mapanga, myundu na mashoka” yaliyotumika kufanikisha mapinduzi.

Dk. Shein yeye hakutaja majina hayo ya silaha makini na za asili, bali alichokisema kinafanana. Amesema hivi: “Hii (Zanzibar) ni nchi ya kimapinduzi.” Anakumbusha yaleyale.

Tafsiri yangu kwa matamshi haya, ni kwamba ukurasa mpya wa uongozi wa mabavu (wengine wanaweza kusema ni udikteta) umefunguliwa.

Kweli Zanzibar ilifanya mapinduzi 12 Januari 1964 baada ya Wazanzibari waliokuwa mbele ya harakati za kuondoa utawala wa wageni, kutoridhika na uongozi wa serikali ya uhuru iliyoundwa kufuatia uhuru wa 10 Desemba 1963, kupindua serikali hiyo.

Lakini uhuru huu si ushetani kama unavyoonekana na wapinduzi hao. Ikiwa hivyo ndivyo, basi huko ni kufuta historia ya kule nchi hii ya visiwa vikuu viwili na vingine vingi vidogo, ilikotoka.

Ukweli ulio mchungu kwa baadhi ya makada wa CCM hasa wasiopenda mabadiliko ya mfumo na sera za uongozi wa nchi, ni kwamba kama si uhuru huo, hakungekuwa na mapinduzi. Wangempindua nani?

Dk. Shein huna haja ya kukasirikia wananchi. Badala yake ni muhimu sana utambue kuwa hata wao wanaipenda nchi yao kama uipendavyo wewe na ujivuniavyo kuiongoza. Wanaipenda sana.

Hebu afikirie kwani wananchi wanaposema “hatutaki Muungano huu” unadhani tafsiri ni kutaka uvunjike au uvunjwe? Hapana. Wanataka viongozi wao mtambue maoni yao na kuyafanyia kazi.

Dk. Shein una bahati kuiongoza Zanzibar ndani ya zama za mapambazuko. Hakuna hata moja sasa linaloweza kufichwa lisijadiliwe na wananchi. Usikhofu maoni ya watu bali yazingatie, ndio sauti yao.

Zama hizi zinahitaji sana uongozi unaosikiliza kile wanachokisema wananchi. Hawa wananchi wanaosema hawataki “muungano huu” si wajinga.

Wanajua wanachokisema, nawe wapaswa kujiuliza, “Lakini kwanini hawautaki.”

Itakuwa ni jambo la hatari iwapo Dk. Shein na serikali unayoiongoza mtapuuza maoni ya; mtayachukulia kama ni kelele za mlango; mkiyachukulia ni kero kwenu. Viongozi mtakuwa mnafanya kosa kubwa ambalo linaweza kuwagharimu.

Siku hizi, kiongozi anayestarehe madarakani ni yule anayefikiria wananchi wake wanachokitaka. Wanasema nini? Wanachokifikiria. Wanawaelewa vipi viongozi wao. Haya ni mambo muhimu viongozi kuyajua.

Hivi tuseme Dk. Shein unakosa nini kuwasikiliza wananchi wanaoamini muungano hauwanufaishi bali unawakandamiza? Sasa si ndivyo waonavyo? Kumbe mtu kufikiri hivi anakusumbua rais?

Dk. Shein kama unataka kuongoza vizuri, basi zingatia vilio vya wananchi unaowaongoza. Tena ungeshukuru na kufurahia kuwasikia wanasema au kulalamika hadharani.

Kama hujanielewa ninachokusudia, panda ndege hadi London. Fika pale eneo ambapo serikali ya Uingereza imefunga vinasa sauti na kupandikiza makachero na kuruhusu watu kutoa maoni kuhusu wanavyoiona serikali yao na wanavyomuona kiongozi wao mtukuka Malkia.

Kama kupuuza maoni ya watu ni ushujaa, wangeanza viongozi Uingereza. Hawapuuzi bali wanayasikiliza maoni au malalamiko ya Waingereza. Na si hivyo tu, wanayafanyia kazi yanayosemwa.

Kama ni kero viongozi hujitahidi kuziondoa, kama ni uchafu wanausafisha na kama ni vikwazo vya kupatikana kwa maisha bora, wanaviondoa.

Sasa Dk. Shein unataka wananchi walale usingizi hata pale unapohutubia? Unataka uongoze mazombi au majuha kalulu? Uongoze watu wasiofikiri siyo, wala kujinafasi pao? Unataka kuongoza watu muflisi?

Itakuwa ni bahati mbaya sana – kuongoza watu majuha kalulu. Kumbuka tayari Wazanzibari kiasili ni watu wenye akili sana, wanafikiri kabla ya kuamua, wanauliza maswali wakitaka majibu.

Dk. Shein unajua vizuri kwamba kwa sababu ya ukweli huo, ndio maana Wazanzibari wengi wanafanya kazi kubwakubwa kwingineko Afrika, na hasahasa Marekani, Ulaya na Uarabuni.

Unajua fika mamia kwa mamia ya wale walioondoka nyumbani kukimbia vitimbi vya utawala mbaya baada ya mapinduzi, wamejijenga na kukabidhiwa dhamana zenye hadhi kubwa ughaibuni.

Ni muhimu kutambua vipaji/vipawa vyao. Ukitambua hili huwezi kupata shida kuwaongoza. Utakuwa unajua tangu awali unao watu makini ambao ukiwatumia vizuri watakusaidia kuibadilisha nchi iwe kweli ya maziwa na asali badala ya tope na harufu mbaya.

Ila ukiamua kuwapuuza na kuwakandamiza, utabaki kuongoza kwa shida. Huwezi kuwashinda japo una dola, maana wao ndio wenye dhamana ya uongozi.

Nakuaidhi punguza hasira maana hujaipata bado sababu ya kukasirikia wananchi wasioridhika na mfumo wa muungano. Hivi hutaki kujisikia raha kwa kuongoza watu ndani ya mfumo wanaoukubali? Nakusihi sasa, hasira zako ni hasara kwako!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: