Hawa Ng'humbi: DC mchapakazi Mvomero


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 March 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Ana kwa Ana

HAWA Ally Ng'humbi hawezi kusahau tarehe 8 Machi 2007. Ni siku alipotangazwa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Hawa ni mkuu wa wilaya wa kwanza wa Mvomero; wilaya iliyotokana na kugawanywa kwa iliyokuwa wilaya ya Morogoro Vijijini.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, ofisini kwake mkoani Morogoro, Hawa anasema, “Nilishtukizwa. Hakika, sikuwa na hisia za kuteuliwa kushika nafasi hii.”

Anasema, “Nilijisikia vizuri. Nilifarijika maana niliona kwamba wakuu wangu wana data (takwimu) katika utendaji wangu wa kazi. Niliona ni changamoto mpya, lakini nilijipa moyo na kusema nitaweza.”

Kabla ya kushika nafasi hiyo, Hawa alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Hawa anasema wakati akichukua nafasi hiyo, wilaya ya Mvomero ilikuwa ikishika mkia katika kufaulisha wanafunzi wa shule za msingi.

Anasema hakupandwa hasira kama ilivyokuwa kwa Albert Mnali, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera. Mnali alipiga walimu viboko kwa kuwatuhumu kuwa chanzo cha wilaya yake kushindwa katika elimu.

Hawa amejijengea sifa kwa kukaa na wadau wa elimu wilayani humo ili kutatua migogoro na kukabiliana na changamoto za elimu na walimu.

“Mimi sikupiga watu bakora. Nilikabiliana na tatizo. Nadhani mwenzetu Mnali alikutana na ibilisi,” anasema.

Mama huyo ambaye hupenda kuzungumza kwa takwimu, anasema aliamua kuketi na wadau wa elimu, ambako pamoja na mambo mengine, walichambua changamoto zilizosababisha wilaya kuzorota katika elimu.

Katika mkutano na wadau wa elimu, walibaini kuwa miongoni mwa matatizo yaliosababisha hali hiyo, ni utoro wa walimu na wanafunzi mashuleni; uhaba wa nyumba za walimu, uchache wa madarasa, upangaji mbovu wa walimu kwa maana ya eneo moja kujaza wengi na kwingine kukosa.

Tatizo jingine walilokumbana nalo ni mwamko duni wa wananchi katika elimu, ukosefu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa umeme na asilimia 45 ya wilaya kuwa milimani.

“Tukatengeneza mikakati kukabiliana na hali hii. Tukaweka vitabu vya mahudhurio kwa  walimu na wanafunzi mashuleni, wakati wa kutoka na kuingia. Pia tukapeana semina juu ya kurudisha nidhamu ya kazi,” anasimulia Hawa kwa taratibu.

Anasema, “Walimu walibanwa kutoa mazoezi ya mara kwa mara na kusahihisha kazi za wanafunzi huku walimu magwiji wa hesabu na sayansi wakipewa nafasi za kusaidia shule nyingine.”

Anasema walijiwekea malengo ya kuwa na vikao vya mara kwa mara kati ya wazazi na walimu huku suala la motisha kwa walimu, wanafunzi na shule iliyofanya vema vikipewa kipaumbele.

Matokeo yake, Hawa anasema, Mvomero kwa mwaka huu, imeshika nafasi ya tatu kati ya wilaya sita za mkoa wa Morogoro.

“Shule ya msingi Kisimagulu, iliyoko Kata ya Hembeti, imeshika nafasi ya tatu katika mkoa na 76 kitaifa,” anasema.

Anasema, “Mwaka jana, tumetoa wanafunzi 4,333 wa kuingia sekondari ambao ni sawa na asilimia 55.1. Tunatarajia mwakani tutoe asilimia 75 na kama itashindikana basi tucheze kwenye asilimia kati ya 60 na 70.”

Akiongea kwa kujiamini, Hawa amekabiliana pia na tatizo la uhaba wa madarasa ambako watu mbalimbali wamekuwa wakichangia baada ya kuombwa na uongozi wake.

Alipotakiwa kueleza ana uhakika gani wa watu wanaochangia kuwa hawataki uongozi wa kisiasa, Hawa alijibu haraka, “Wanaotusaidia  wako wengi. Yupo mheshimiwa Mbunge na  watu wengine wenye nafasi zao mbalimbali katika serikali na jamii, wakiwamo wazaliwa wa Mvomero na wengine. Lakini kubwa zaidi ni kwamba wananchi wanatumia nguvu zao.”

Anasema, “Hivyo basi, sioni kama kuna dhambi kuomba kama mtu una shida. Siwezi kuacha kuomba msaada wakati tunashida; kama nitaondolewa kwa sababu ya kuwaomba wadau, sawa lakini ninachofanya naamini ni sahihi.”

Anasema, “Jambo kubwa hapa ni maendeleo. Hii ni wilaya mpya. Mwaka huu Mpango wa Maendeleo wa Shule za Sekondari (MMES), hawakutoa fedha. Tumepata ruzuku ya Mpango wa Kukuza na Kurekebisha Uchumi (MKUKUTA) tu.”

Akizungumzia ugomvi wa wakulima na wafugaji, Hawa anasema, “Hapa napata homa maeneo yale tambarare, tarafa za Mlali na Turiani, lakini dawa yao iko, maana nasikia wale wafugaji kutoka Kilosa wameingia; nikimaliza hili la shule, tutaanza operesheni kuondoa wafugaji waliovamia Mvomero.”

Ofisi ya wilaya ya Mvomero iliyojengwa Dakawa na kugharimu Sh. 1.3 bilioni imekamilika na itaanza kutumiwa Juni mwaka huu. Kwa sasa ofisi ya mkuu wa wilaya ipo Morogoro mjini.

Hawa, mke wa Mhandisi wa Umeme, Ramadhani Hamisi Ng’humbi, ni mama wa watoto watano aliyezaliwa Gonja-Maore, Same, mkoani Kilimanjaro. Baba yake, Ally Kengera na mama yake, Mwanaidi Mrutu, ni marehemu.

Amepata elimu katika Shule ya Msingi Gonja-Maore, wilayani Same, Shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira na baadaye Kilakala kwa elimu ya kidato cha Tano na Sita.

Kabla ya kujitosa kwenye siasa mwaka 2000, Hawa alikuwa Meneja Utawala na Fedha wa Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO). Kabla ya hapo alikuwa ofisa mwandamizi wa TPBC ambayo baadaye iligeuka na kuwa GASCO.

Aliajiriwa TPBC, mwaka 1980, muda mfupi tangu ahitimu shahada ya kwanza katika Taasisi ya Uchumi na Mipango cha Odessa, Moscow, nchini Urusi.

Hawa amefuata masomo pia katika Chuo Kikuu cha Salford cha Manchester, Uingereza na Taasisi ya Delft ya Uholanzi ambako alichukua kozi ya utawala katika viwanda.

“Sasa wakati naingia kwenye siasa, nia yangu kubwa ilikuwa ni lazima nipate ubunge lakini mambo ya siasa hayaji moja kwa moja; lazima ujifunze,” anasimulia.

Akaanza mchakato wa kujifunza na kuomba nafasi katika udiwani, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam. Mwaka 2000 alibahatika kuteuliwa kuwa diwani wa viti maalumu kupitia CCM.

Wakati anaendelea na udiwani huo, mwaka 2003 aliwania na kushinda Uenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake, wilayani humo.

Safari yake kisiasa iliendelea mwaka 2005, alipoomba nafasi ya Ubunge kupitia Viti Maalumu, lakini hakubahatika kupata nafasi hiyo. Alishika nafasi ya tatu nyuma ya kina Janet Kahama na Janet Masaburi, walioteuliwa kuwa wabunge.

Mwaka huo 2005, aliteuliwa kuwa Meneja wa Kampeni katika Jimbo la Ubungo ambapo Charles Keenja wa CCM aliibuka mshindi.

Anakumbuka kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa na wa aina yake. Keenja alikuwa anachuana na kijana John Mnyika wa Chadema.

0
No votes yet