Hawa wanastahili kurudi bungeni?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 12 May 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Musa Azan Zungu, Mbunge wa Ilala

MATATIZO mengi yanayoonekana kwenye baadhi ya majimbo yetu ya uchaguzi yanahusiana moja kwa moja na watu wanaotuwakilisha.

Upo uwiano wa matokeo kati ya aina ya wabunge tunaowapeleka bungeni na kiwango cha uongozi unaopatikana katika majimbo yao.

Ninaamini kabisa kuwa wabunge goigoi na wasio na uwezo kiuongozi wataenda Dodoma kama wasindikizaji tu, na matokeo yake ni kwamba miaka mitano itapita na matatizo kwenye majimbo yao yatakuwa ni yale yale kama siyo kuongezeka.

Hivyo, unapokuja uchaguzi huu mkuu ni jukumu la wananchi kupima vizuri ni wawakilishi gani wanawapeleka bungeni na wanatarajia nini kutoka kwa wawakilishi hao.

Haitoshi kuwapigia kura watu na kuombea kuwa wakifika bungeni basi watafanya tunachotarajia. Ni muhimu kuwajua wagombea hao kabla hatujawapa kura zetu na kuwachuja mapema pale fursa itakapopatikana.

Kutokana na ukweli huo, binafsi ninaamini kuwa Watanzania wanahitaji kwa mara nyingine kama nilivyoonesha huko nyuma kupewa zana zote muhimu za kuwasaidia hatimaye kufanya uamuzi sahihi kabla ya kufanya uchaguzi.

Kuna makundi makubwa manne ya wabunge ambayo ningependa kuyaongelea.

Wapo wabunge waliozoea uchafu na kuuvumilia, wabunge waliokumbwa na kashfa nzito, wabunge watetezi wa mfumo wa utawala wa kifisadi, na wabunge ambao uwepo wao bungeni hakuna faida yoyote zaidi ya gharama kwa wananchi.

Katika makala hii hata hivyo nataka kuanza na kundi maalum la wabunge ambao niwaita “waliozoea uchafu na kuuvumilia.” Hawa ni wabunge wote wa mkoa wa Dar es Salaam.

Kule Marekani kuna msemo kuwa “jinsi California inavyowekenda, ndivyo Marekani nzima inakwenda.” Kwa maneno mengine, California ndiyo jimbo ambalo linatoa mwelekeo wa mambo mbalimbali hasa katika masuala ya kijamii na tamaduni na hata kisiasa.

Kwa upande wetu, Dar es Salaam ndio jiji linalotoa mwelekeo kwa taifa na pale ambapo uongozi unakosekana Dar es Salaam, basi kuna uwezekano mkubwa sehemu kubwa ya nchi ya nchi nayo ikafuata mfano wake.

Jiji la Dar es Salaam halina mfano mzuri wa usafi au ubora kwa taifa; ni chafu linaongoza kwa kuwa na watu wenye kuvaa nguo nzuri na wenye kuendesha magari mazuri, lakini wakiwa wakiwa wamezungukwa na uchafu!

Siku chache tu zilizopita ambapo mvua kubwa zimenyesha, sura halisi ya Dar es Salaam imeonekana. Sitakuwa mtabiri endapo nitawaambia wananchi kuwa muda si mrefu tutasikia kipindupindu kimeibuka kutokana na uchafu uliokobuhu na uliosababishwa na maji machafu kusambaa ovyo mitaani.

Lakini si katika uchafu tu, jiji hili lina matatizo mengi ikiwamo usimamizi na matumizi ya fedha za walipa kodi.

Naweza kutoa mifano mingi lakini itoshe kusema, wabunge wa Dar es Salaam wameshindwa kusimamia maslahi ya watu wao katika masuala ya usafi na usimamizi wa fedha.

Kutokana na kushindwa kwao wamekuwa washirika wa ufisadi mbaya zaidi kwani kutokana na uzembe wao na kutowajibika kwao kwa kuonesha mfano wa uongozi unaostahili, Dar es Salaam imeendelea kuwa kituko cha maendeleo.

Wabunge wa Dar es Salaam ambao wote wanatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni, Musa Azan Zungu (Ilala)

Makongoro Mahanga (Ukonga), Ritha Mlaki (Kawe), Idd Azzan (Kinondoni) na Charles Keenja (Ubungo).

Wengine ni Mwinchumu Abdulrahman (Kigamboni) na Zuberi Abbas Mtemvu (Temeke). Ni Keenja tu ambaye ametangaza kutogombea tena katika uchaguzi ujao.

Wawakilishi hawa wa wananchi wameshindwa kutetea walipa kodi wa Dar es Salaam na wameshindwa kutoa mfano wa uongozi unaohitajika.

Kwa wananchi wa Tanzania, Dar es Salaam ndiyo New York yetu, ndiyo London yetu, na ndiyo Tokyo yetu; hata kama tungeshindwa kuwa na miji yote mizuri, misafi na uwajibikaji tungetarajia kuona jiji hili haiwi hivi lilivyo.

Lakini kutokana na uwakilishi mbovu wa wabunge hawa, Dar es Salaam limeendelea kuwa kituko na fedha za walipa kodi wa jiji na nchi wahisani, zimeendelea kutafunwa ama kwa kushiriki au kunyamazia.

Wabunge hawa wameshindwa kuwa wapiga kelele dhidi ya ufisadi uliokubuhu kwenye halmashauri zao na hata pale walipopiga kelele hawajawahi kuonekana wako tayari kutaka watu wawajibishwe.

Lakini zaidi kwa miaka hii minne iliyopita wabunge hawa wameshindwa kuwa mfano wa uongozi wa taifa. Wakiwa ni wabunge wa kutoka jiji letu kuu tulitarajia ndio wangekuwa watetezi wa kwanza wa maslahi ya taifa.

Wameshindwa kupiga kelele bungeni kutaka genge la wezi wa utajiri wa urithi wa watoto wetu washughulikiwe bila huruma. Baadhi yao, hasa Mahanga amekuwa mtetezi mkuu wa mafisadi.

Mara kadhaa amekuwa akitoa wito kwa serikali na chama chake kumsafisha waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa Richmond, Edward Lowassa.

Ninazungumza kwa uhakika wa nisemacho kwani baadhi yao wakati nashughulikia suala la watoto waliotelekezwa na serikali ya CCM kule Ukraine waliogopa hata kuchukua msimamo. Nilipojaribu kuwatafuta ili wawe watetezi wa vijana ambao asilimia kubwa walikuwa wanatoka Dar es Salaam, wengine walikimbia.

Lakini kuna mifano ya mambo mengine ambayo yametokea kwenye halmashauri zao kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Katika ripoti yake ya mwaka 2008/2009, CAG anaonyesha jinsi mamilioni ya shilingi yanavyoendelea kukwapuliwa mambo ambayo mwakilishi wa kweli makini asingelala hadi anayapatia ufumbuzi.

Kwa mfano katika manispaa ya Ilala: Hati za malipo zenye jumla ya Sh. 39,213,953 hazikuonekana wakati wa ukaguzi.

Malipo yenye jumla ya Sh. 3, 7 bilioni kwa mwaka 2008/2009 imebainika kuwa yalikuwa na nyaraka pungufu.

Hata malipo ya awali ya Sh. 364, 534, 000 kwa ajili ya uwekezaji katika kiwanda cha chuma cha M/s East Africa MEATCO Ltd ambacho hakijaanza na uwezekano wa kurejeshewa fedha ni mdogo.

Je, wabunge walioko Ilala wamefanya nini kushughulukis suala hilo? Je, endapo ndugu zetu hawa watagombea tena, hatimaye watajua cha kufanya!? Hakika, Ilala inahitaji wabunge wapya!

Angalia Kinondoni: Kiasi cha Sh.66,981,600 kimelipwa kwa kampuni ya M/S TRACTOR LTD ikiwa asilimia 70 ya malipo ya awali ya ununuzi wa matrekta matatu yaliyokwisha tumika ambayo uongozi wa manispaa ulidai kuwa mapya.

Aidha, maduhuli toka kwa mawakala wa ukusanyaji yenye jumla ya Sh.326,506,358 hayakuwasilishwa katika Manispaa.

Kiasi cha Sh. 277,268,946 kilipokelewa kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato hakikuingizwa katika vitabu vya manispaa na hazikupelekwa benki.

Je, katika mazingira haya, wananchi wa Kinondoni bado wanataka kuchagua wabunge hawa kuwawakilisha? Kwa ujiko gani walionao?

Hata katika wilaya ya Temeke hali ni hiyohiyo. Shilingi 151,552,986.56 zinaonekana katika daftari la fedha, lakini hakuna taarifa za kibenki zinazoonesha kuwa fedha hizo zimeingizwa benki.

Aidha, uongozi wa manispaa ya Temeke umeonyesha hundi zenye thamani ya Sh. 181,432,365.93 ambazo hazikuwasilishwa benki!

Je wananchiwa Temeke wanastahili watetezi walewale waliowasaliti kwa muda wa miaka mitano iliyopita?

Ninapozungumzia wabunge wa maeneo hayo bila ya shaka nawafikiria na madiwani wao vile vile kwani wote wanachaguliwa kuwawakilisha wananchi katika ngazi mbalimbali za utawala.

Lakini jukumu la kwanza la kuwazuia wabunge hawa kurudi tena linawaangukia wana CCM wa mkoa wa Dar es Salaam; lakini kwa vile wana CCM hao wameshaonesha udhaifu mkubwa wa kuonesha mfano wa kulipatia taifa viongozi wazuri basi hukumu ya mwisho ni lazima itolewe na wakazi wenyewe wa Dar es Salaam kwenye sanduku la kura! Hili linawezekana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: