Haya ni madudu ya kamati ya uchaguzi Yanga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend

JUNI 6, mwaka huu mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Imani Madega aliitisha mkutano mkuu wa kujadili marekebisho ya katiba, lakini mwishoni akaporwa madaraka na kamati ya uchaguzi.

Madega aliwatangazia wanachama kwamba uchaguzi mkuu ungefanyika Julai 4, lakini kamati ya uchaguzi ikashinikiza uchaguzi urejeshwe nyuma, ufanyike Juni 27.

Kama nilivyoeleza katika makala iliyopita ni kwamba Madega aliondoka kwenye mkutano aliouitisha yeye mwenyewe akiwa hana uhakika kama bado anaendelea na kiti chake au la.

Siku ya pili yake akatoa barua nzito kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akihoji ushiriki wa makamu mwenyekiti na mwanasheria wa TFF katika mkutano huo.

Nadhani ni kutokana na barua ile, TFF ilijadili kwa kina na kamati ya uchaguzi ikatazama ukomo wa mamlaka yao wakaamua kumtambua Madega kama mwenyekiti wa klabu.

Sawa. Katika mkutano wa Juni 6, kwa vurugu vurugu na hasa kwa vile kulikuwa na kichocheo cha pilau na tiketi za bure kuingia kwenye Uwanja wa Taifa kuona pambano kati ya Brazil na Taifa Stars, kamati ya uchaguzi ikaingiza suala la kihisia.

Kamati hiyo ilidai kwamba “sheria za uchaguzi mkuu zinazuia chaguzi ndogo kufanyika katika kipindi cha miezi minne cha kuelekea uchaguzi mkuu,” lakini baada ya kufanya uchunguzi kamati ikaja na wazo jipya.

Kamati hiyo ilidai baada ya kufanya uchunguzi wa kina eti wamegundua sheria ile haijapitishwa. Masikini, kwa vile watu wengi hatusomi na hatujui sheria, wapinzani wa Madega wakalipuka kukubaliana na kitu ambacho hakijapitishwa.
Inasikitisha kuona kwamba waliowasilisha hoja hiyo kwenye mkutano ule wa wanachama ni wanasheria waliobobea, ambao kimsingi walipaswa kuwa msaada mkubwa kwa wanachama.

Wiki moja baadaye wanasheria hao bobezi; kamati ya uchaguzi wanakuja na tarehe mpya ambayo inakwenda mbali zaidi ya muda aliopanga Madega kung’atuka.

Madega alipanga uchaguzi mkuu ufanyike Julai 4, lakini kutokana na upinzani tu ukarudisha nyuma hadi Juni 27, lakini tena hao hao walioshawishi urudishwe nyuma wameibuka na kusema uchaguzi ufanyike Julai 18.

Kama hivi ndivyo, uko wapi ubaya wa Madega? Iko wapi dhana ya Madega kwamba anataka kuendelea kukaa madarakani? Hivi Julai 4 na Julai 18 tarehe ipi iko mbele?

Hivi kamati haikujua kwamba mamlaka yao ni katika kuratibu na kusimamia uchaguzi mkuu na wala si kuongoza klabu? Kuna sehemu yoyote katika muhtasari palipoandikwa kwamba wamekabidhiwa klabu?

Haya ni madudu. Hivi kwa nini isilaumiwe kamati ya uchaguzi ambayo ilikuwa mstari wa mbele kumvuruga Madega? Tazama, kuna tofauti ya siku 14 kutoka Julai 4 hadi Julai 18, hivyo Madega ataendelea kukaa madarakani kwa wiki mbili zaidi.

Msemaji wa kamati hiyo aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba sababu zilizochangia kubadilika kwa tarehe hiyo ni pamoja na klabu hiyo kutokuwa na kanuni hivyo wanatakiwa kutumia kanuni za uchaguzi za TFF. Pia amesema muda wa kuitisha uchaguzi mkuu unapaswa kuwa siku 40.

Kama kasoro hizo mbili zingesababishwa na mtu au mwanachama mwingine yeyote asiye na ujuzi na sheria tusingembebesha lawama.
Katika hili mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi anastahili kulaumiwa na hata pale anapowataka wanachama wa klabu hiyo wawe na subira na wasilete malumbano ambayo mwisho wake ni vurugu, ajue amechangia hali hiyo.

Kwani alipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi hakujua Yanga haikuwa na kanuni hadi baada ya kumvuruga Madega? Hivi hakujua, kama klabu haina sheria au kanuni inapaswa kutumia zile za TFF?

Mbona hilo ni jambo la kawaida! Ndiyo maana hata baadhi ya wanachama wa Simba waliouburuza uongozi wa klabu kortini tulionya kwa kutumia Katiba ya FIFA?

Isitoshe, hata hicho kinachodaiwa kuwa ni sheria inayozuia chaguzi ndogo kufanyika katika kipindi cha miezi minne kuelekea uchaguzi mkuu, ilitangazwa usiku nyumbani kwa mwanasheria mmoja ili kumzuia Augustino Mrema aliyekihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) asifanye mkutano wa hadhara.

Tangazo hilo liliiathiri pia Yanga lakini walipoomba ufafanuzi, taratibu ziliendelea kama kawaida. Miaka 15 baadaye “sheria isiyo sheria” inafufuliwa kumvuruga Madega.

Watu wanaodhani wanapendwa sana na wanachama ndani ya klabu wajiangalie; wanachama hawana rafiki wa kudumu na hawana adui wa kudumu. Waliokuwa wafadhili tegemeo waliwahi kuondolewa kwa bakora na wengine walizuiwa walipogoma kutoa pesa za nauli.

Baadhi ya viongozi waliowahi kupendwa sana klabuni akiwemo Rashid Ngozoma Matunda waliondolewa kwa aibu na hata Tarimba Abbas aliyeendeleza wazo la Yanga kuwa na kampuni, walipata shida.

Mathalani, katika mkutano wa kupitisha wazo la kuwa na kampuni kwenye kituo cha utamaduni cha Urusi (Russia), ni wajumbe wanne tu waliopinga, lakini kadri siku zilivyopita, Tarimba alibakiwa na watu wanne tu wanaomuunga mkono kuhusu kampuni.

Na kwa vile wazo na uendeshaji wa Yanga kampuni ni Tarimba tu aliyekuwa anajua, seneta Francis Kifukwe aliyerithi mikoba hakumudu. Kampuni ikabaki kwenye makaratasi kama Ujumaa ulivyobaki kwenye makaratasi ya CCM.

Methali ya Kiswahili inasema, “Ajidhaniaye amesimama aangalie asije kuanguka.”

Hao “wanaoipelekesha” Yanga leo wakijiona kuwa wao ni marafiki wapendwa, wajiangalie, kwani wanachama watakapogundua wanaburuzwa kwa ajili ya kufanikisha maslahi ya mtu aliyetoa pilau na tiketi za kuiona Brazil ikionyesha samba, watageuka kuwa maadui wakubwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: