Hayuko wa kulinusuru taifa


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

WAKATI umefika kwa Watanzania wote, kwa umoja wetu, bila kujali tofauti za kiitikadi na kidini, kuungana  na kuinua macho juu, tutazame milima, kuona msaada wetu utatoka wapi! Nchi imefunikwa na blanketi la malalamiko na sononeko.

Nimetahadharisha kwa muda mrefu, kuwa watawala wetu wamekuwa sawa na mtu aliyedungwa sindano ya ganzi naye hasikii maumivu.

Ugumu wa maisha kwa wananchi hauonekani kwao; wamejikita katika mambo madogomadogo ambayo yana mwonekano wa anasa, usanii na utoto mwingi.

Misiba isiyokuwa na tija ndiyo wanaikimbilia kuhani huku nyuma wanatuletea siasa za udaku, fitina na majungu. Miaka inakwenda, moja jema la mfano hakuna.

Wamo ziarani. Wananchi wanashuhudia watawala wao wakijirundikia ukwasi mkubwa mpaka wanashindwa kujieleza.

Wengine wanatembea na silaha za kivita kulinda raslimali za nchi walizopora! Haonekani wa kulinusuru taifa maana ukiwatazama wanaonekana kufanana kwa matendo yao.

Ukimya wa serikali umepitiliza. Umemsukuma  Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi kupinga hadharani na bungeni dhambi za mawaziri. Akasema, “Serikali ipo kama haipo.” Wizi unafanywa na serikali yenyewe.

Katika hali kama hiyo nani amkemee nani? Aliyetakiwa kuwa mkemeaji, ndiye mtetezi wa wezi. Kama siyo mshirika basi ni nani?.

Jenerali Ulimwengu katika safu yake kumaliza kila kitu akisema, “Kusema kweli, sura iliyojitokeza wiki iliyopita ni kwamba hatuna serikali inayofanya kazi kama serikali, bali tuna mkusanyiko wa maofisa waliokabidhiwa ofisi mbalimbali ambazo wanazitumia kadri wanavyojua wao na wala hawana udhibiti wa kati.”

Akaongeza, “Tunachokishuhudia ni msambaratiko ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi hii, serikali iliyoparaganyika, mawaziri wenye kauli za kitoto, wakuu wa serikali wasiokuwa na maamuzi, waziri mkuu kivuli asiyekuwa waziri mkuu na mkuu wa nchi mtoro”

Nani sasa kati yao atasimama ili Taifa lipone? Uongozi wetu umeikatisha tamaa nchi.

Kufichuliwa kwa wizi wa raslimali, ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyoainishwa na kamati za kudumu za Bunge na pia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kumeonyesha namna viongozi wote wenye jukumu la kusimamia mawaziri walivyoshindwa kazi.

Hali hii inaonyesha kwamba viongozi wanaowasimamia mawaziri ama ni legelege sana na dhaifu kiuongozi, au wao wenyewe ni sehemu ya uozo huo. Si kupwaya tu hawafai kuendelea kuitwa viongozi.

Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilikutana eti kukubaliana kuwa viongozi waliotuhumiwa na kamati za kudumu za Bunge na ripoti ya CAG wawajibishwe na Rais Jakaya Kikwete.

Sijui nani katoa wazo mufilisi kama hili. Ni aibu kwa watu hawa kungoja kuwajibishwa na kuondoshwa kwa aibu badala ya wao wenyewe kuwajibika na kuondoka wakiwa na heshima zao.

Wanafanya watu wahisi kuwa walijua kuwa aliyepaswa kuwawajibisha asingewawajibisha kwani ni mwenzao. Upepo uliotamkwa uliikoleza imani hiyo. Masuala mazito yanayotishia usalama wa nchi yanafananishwa na upepo uvumao. Uongozi aina hii ni mkosi!

Kinachoongeza uchungu zaidi ni habari zilizofichuliwa kutoka ndani ya kikao kilichoitishwa kwa ghafla kuwa mwenyekiti wa CCM eti alilazimishwa kujadili suala la mawaziri, uchafu wao na kutakiwa kwao kujiuzulu.

Habari zinasema mwenyekiti ambaye pia ni rais hakuwa na nia ya kulijadili na wala halikuwa sehemu ya ajenda. Hajui afanyeje au hataki?

Kama Wabunge wametia saini zao kutaka kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili ikiwezekana apoteze kazi yake, kitendo ambacho kitasababisha kuvunjika kwa baraza zima la mawaziri, kuipuuza hoja hiyo inashangaza.

Mwenyekiti anashangaza maana kama vyama vya siasa vimeazimia kwenda kwa wananchi kukusanya saini zitakazotosha rais mwenyewe kupigiwa kura kutokuwa na imani naye, kutochukulia hoja hii katika umuhimu unaostahili ni bahati mbaya.

Tukiuchekea utoto huu tunaikejeli amani yetu. Nasema hivi kwa sababu kufanyiwa mzaha jambo kubwa kama hili ni sawa na mwendawazimu kuchekea kitanzi ambacho kiko tayari shingoni mwake. Kukubali kuongozwa kisaniisanii ni ukondoo, nalo ni tusi kwa yeyote aliyetimamu.

Kuibuliwa kwa kashfa ya Richmond kulisababisha baraza la mawaziri kuvunjika kwa mara ya kwanza katika awamu ya nne. Baraza la mawaziri lilivunjika baada ya aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Akateuliwa Pinda kuchukua nafasi ya Lowassa na kisha baraza likasukwa upya. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 likaundwa baraza jingine, lakini hata kabla ya kufika nusu ya muhula wake limejiingiza katika ufisadi wa kutisha.

Wabunge wamechachamaa na CC imeshinikiza baraza livunjwe katika kipindi ambacho Spika wa Bunge Anna Makinda akitakiwa kuitisha kikao cha Bunge kuamua hatima ya Waziri Mkuu.

Kwa hiyo, njia pekee ya kuokoa serikali kuvunjika tena bungeni ni Rais Kikwete kuwafukuza mawaziri wote waliotuhumiwa na kuwafungulia mashtaka. Hivi baraza hili litavunjwa mara ngapi? Kwanini hivi lakini? Tatizo ni mawaziri au mteua mawaziri?

Hili linanikumbusha kesi ya jirani yangu aliyeshitakiwa mahakamani kwa kosa la kumuua mkewe. Alimfumania mke wake akifanya mapenzi na mwanaume mwingine. Kuona hivyo alichomoa bastola na kumpiga risasi mkewe.

Jaji alipomuuliza mtuhumiwa kwanini aliamua kumuua mke wake badala ya kumuua yule mwanaume mgoni wake, mtuhumiwa alijibu, “Mheshimiwa Jaji, niliona ni busara kuua mtu mmoja mara moja. Kwa tabia aliyokuwa nayo mke wangu, ningeamua kuua mgoni wangu ingenibidi niwe naua watu wawili mpaka watatu kila wiki.”

Tatizo hapa ni nini? Tatizo hapa siyo mawaziri wezi. Wezi wapo kila mahali hata katika hao wapya watakaoteuliwa wezi watakuwapo. Tatizo ni nchi kukosa kiongozi wa kusimamia mawaziri wasiibe.

Mkiwa na kiongozi asiye ‘uti wa mgongo’ lazima nchi itayumba. Kiongozi asiyejua tofauti ya nguvu kati ya kamati kuu ya chama chake na nguvu ya Bunge la nchi yake ni wa hatari kwa amani ya nchi.

Mustafa Nkullo waziri wa fedha na mwanachama wa CCM amesema hawajibiki kwa kamati kuu ya CCM.

Hiki ni kiburi lakini namuunga mkono. Kwangu mimi nisiyekuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa CC ya chama chochote inanihusu nini?

Ikiwa rais ana washauri wabovu, lakini yeye mwenyewe hana akili? Katika hali kama hii Watanzania wafanye lipi? Waamue kuua mtu mmoja mara moja kama alivyofanya yule jirani yangu au waendelee kuona baraza la mawaziri likivunjwa na kuundwa na kisha kuvunjwa tena? Wanatolewa wezi wa zamani na kuingizwa wezi wapya?

Kama tatizo ni uongozi mwenye jukumu la kurekebisha ni nani? Si watu wote wana uwezo wa kuongoza wenzao? Kushindwa kuongoza ni bahati mbaya, lakini kung’ang’ania kuongoza huku ukijua kuwa huwezi ni dhambi kubwa kama ilivyo dhambi ya uhaini.

Katika kufanya hivyo unapoteza maisha ya watu na kusababisha dhiki kubwa kwa watu wengi. Nchi inasimama na wakati mwingine kuporomoka. Kuondoka kwa hiari ni uungwana lakini kuondolewa madarakani kutokea kwenye mitaro ya majitaka kwa nguvu ya umma ni malipizi kwa mtu king’ang’anizi.

0713 334239
0
No votes yet