Hekima iwaongoze CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Mtazamo
Mary Chatanda

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Arusha, Mary Chatanda hakubaliki. Anashutumiwa nje na ndani ya chama chake na kwamba yeye ni kiini cha matatizo ya kisiasa Arusha.

Analalamikiwa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutokana na ushiriki wake usiohalali katika uchaguzi wa meya wa jiji la Arusha. Hivi sasa ananuka ndani ya CCM.

Katibu huyo, ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum (CCM), kwa taratibu anapaswa hushiriki vikao vya Baraza la Madiwani katika halmashauri husika. Mary alipata ubunge huo kupitia mkoa wa Tanga, hivyo alipaswa kushiriki vikao vya halmashauri yoyote ya wilaya za mkoa wa Tanga na siyo Arusha.

Kwa hiyo, ushiriki wake katika kikao cha kumchagua meya wa halmashauri ya Arusha ulikuwa batili na hiyo ndiyo sababu ya CHADEMA kuandaa maandamano ya amani kupinga taratibu zilizotumiwa kumpata, meya Gaudence Lyimo.

Serikali ya CCM ilituma mamia ya Polisi wa Kuzuia Ghasia (FFU), ambao walifyatua risasi za moto na kuua watu watatu na kujeruhi kadhaa. CHADEMA walilaani mauaji hayo na hadi leo serikali haijatengua matokeo yale.

Dhambi ile imemtafuna Mary na serikali safari hii amekuwa chanzo cha vurugu ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM mkoa wa Arusha.

Madai ya vijana hawa yana sura mbili—upande mmoja wanaunga mkono madai ya CHADEMA kwamba Mary arudi kwao Tanga ambako ni mbunge wa Viti Maalum.

Upande wa pili vijana hao, ambao Mei 19, mwaka huu waliandamana katika makao makuu ya CCM mkoa, wanataka yeye pamoja na Mjumbe wa Baraza la Vijana mkoani Arusha, Mrisho Gambo "wajivue gamba".

Ujumbe wa vijana hao, wapatao 500 uliokuwa kwenye mabango ulisomeka, "Chatanda umehujumu uchaguzi kwa siasa zako za makundi zilizojaa chuki, ubinafsi na ubabe usio na manufaa kwa Chama Cha Mapinduzi".

Bango jingine lilisema, "Chatanda kwa siasa zako za ubabe umetuchonganisha na viongozi wa dini”.

Madai haya ni mazito. Siku ya pili yake Mary aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo alijibu kwa nguvu. Kwanza alirusha shutuma kuwa mandamano yale yaliandaliwa na mafisadi na siku tatu baadaye kundi jingine liliandaa maandamano likitaka mafisadi wajivue gamba.

Pili akasema hatojiuzulu kwa shinikizo la vijana kwa madai hawajui kanuni za chama kwani yeye alichaguliwa na mkutano mkuu wa CCM hivyo hawezi kujiuzulu kwa majungu ya UVCCM.

Kadri kada mmoja wa CCM anavyojibu tuhuma kutoka kwa wapinzani wake, ndivyo mambo mapya huibuka.

Majibu ya Mary yanaonyesha ndani ya CCM mkoa pia kuna mafisadi; kuna majungu, na wengi hawajui taratibu za kuwasilisha hoja kwenye vikao halali. Kama kawaida, Mary naye hakutaja mafisadi na wapikamajungu.

Ugonjwa huu ndio unautafuna mkoa wa Dar es Salaam. Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan alipotaka kamati ya siasa ya mkoa wa Dar es Salaam ijivue gamba, katibu wa CCM mkoa, Kirumbe Ng’enda akarusha shutuma nzito ya kuwa Azzan anauza dawa za kulevya. Baada ya malumbano makali Ng’enda akaomba radhi eti alikuwa anatania.

Hivi, mtendaji mkuu wa ngazi ya mkoa anawezaje kutoa shutuma nzito katika vikao vinavyojadili masuala mazito ya chama halafu akaachwa eti alikuwa anatania?

Kama Azzan ameadhibiwa kwa kutoa rai ya kujivua gamba nje ya vikao, anaachwaje anayetumia vikao halali kuingiza majungu? CCM watumie busara zaidi—warudi kwenye darasa elekezi—waangalie wamejikwaa wapi hadi wanakumbatia dhambi ya majungu na fitina.

Aidha, mtafaruku wa Arusha ambao unachukua sura tofauti kila uchao, unahitaji hekima usiwe kiini cha umwagikaji mwingine wa damu.

0789 383 979 jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: