Henjewele na Tarime, Shelutete na Geita


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

WIKI iliyopita nilifuatana na kundi la viongozi wa dini kutoka ndani na nje ya Tanzania, kutembelea maeneo ya migodi ya dhahabu huko Tarime, mkoani Mara na Geita mkoani Mwanza. Ndani ya kundi hilo walikuwamo wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na viongozi wa dini.

Kutoka nje ya nchi, walikuwapo wawakilishi wa nchi za Canada, Afrika Kusini, Zambia, Botswana, Msumbiji na Norway. Niliyoyaona kwa macho yangu na kuyasikia kwa njia ya simulizi mbalimbali za wenyeji, yananifanya niandike makala hii nikiwaangalia wakuu wa wilaya hizo mbili.

Huko Tarime tulipata nafasi ya kuonana na Mkuu wa Wilaya hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Henjewele. Nitamkumbuka daima ofisa huyu wa serikali kwa mambo mawili makubwa. Kwanza kwa tabia yake ya kukosa hisia na heshima kwa watu wa Tarime, na pili, kwa fikra zake zinazoweza kutafsiriwa kuwa ni mhaini japo yeye hajajifahamu. Nitaeleza.

Mkuu wa Wilaya anadai watu wa Tarime hawatawaliki. Anasema mbele ya wageni, wakiwamo maaskofu kuwa watu wa Tarime si wastaarabu hata kidogo, na ndiyo maana wanatawaliwa kipolisi polisi.

Akautisha ujumbe wetu kuwa tusiende Nyamongo na kama tutakaidi maelekezo yake, yeye hayuko tayari kuwajibika kwa ajili ya ukaidi wetu maana anawajua vizuri watu wa huko walivyo na vurugu.

Akaendelea kutoa maelezo kuwa, umefanyika utafiti juu ya watu wa Tarime na kubaini kuwa watu wa Tarime si Watanzania, wala si Wakenya, bali ni “Watarime”. Ndipo zikaingia fikra za kihaini pale alipodai kuwa Tarime ni taifa pekee na huru nje ya himaya ya Tanzania, na yeye ndiye rais wa taifa hilo.

Kwa mteule wa rais wa nchi, aliyetumwa kuongoza eneo kisha akalitangaza kuwa ni taifa maalumu na watu wake ni watu maalumu, ni fikra za hatari sana. Yawezekana aliyasema haya kwa kejeli na utani uliozidi mipaka, lakini maneno haya kusemwa mbele ya wageni wa kutoka nje ya nchi, tafsiri yake ilikuwa mbaya sana.

Sisi watanzania tuliokuwa ndani ya msafara huo tulipata taabu sana kujibu maswali ya wageni kuhusu matamshi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Henjewele.

Baada ya maelekezo yake hayo na zuio lake la kututaka tusiende maeneo ya mgodi, tuliamua kwenda kwa ridhaa yetu wenyewe. Tulipofika kule, tulipokelewa vizuri na wananchi wa huko, na bila kuwauliza lolote juu ya mkuu wa wilaya, walianza kutueleza jinsi mkuu huyo wa wilaya anavyotumikia wawekezaji wa mgodi.

Walikwenda mbali na kusema watoto wa mkuu wa wilaya wanalipiwa karo na wawekezaji, na kuwa posho anayopata kutoka mgodini ni kubwa mara kumi kuliko mshahara wa serikali. Yawezekana sana huu ni uwongo lakini ambao umechochewa sana na tabia ya mkuu wa wilaya ya kuwatelekeza wananchi wake na kuwatumikia wawekezaji.

Wananchi walitupokea kwa amani na walitulia wakati wote wakieleza kero zao mbalimbali na madhara ya kiafya, kiuchumi na kijamii wanayoyapata kutokana na uchimbaji wa dhahabu. Wageni wetu walishangaa kukuta wananchi wale ni wakweli, wanaoongea kwa vielelezo na ustaarabu mkubwa. Baadhi yao waliongea kwa jazba zinazotokana na ukandamizaji wa muda mrefu kutoka kwa wawekezaji na watendaji wa serikali.

Huko Geita nako tulikumbana na kigingi cha kwanza baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo aitwaye Shelutete alipokataa kukutana na ujumbe wetu kwa madai kuwa mkuu wa mkoa alikuwa anafika wilayani humo.

Mwenye hekima angedhani mkuu wa wilaya angetumia fursa hiyo kukutana na ugeni huu mkubwa akiwa na mkuu wake wa mkoa, lakini haikutokea hivyo.

Umbali usiozidi kilomita moja kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya, kuna kambi ya wakimbizi wa ndani ambayo imekuwa hapo kwa takribani miaka mitatu sasa. Watu hao ambao sasa wamebakia familia ishirini, wanaishi kwenye mahema yaliyotolewa na makanisa na misikiti ili kuwasitiri baada ya kudhulumiwa ardhi yao na wawekezaji katika migodi.

Tulipofika katika kambi hiyo inayosikitisha, tuliwaona watoto wadogo waliozaliwa ndani ya kambi hiyo, akina mama wajawazito, wazee na wagonjwa. Mateso wanayoyapata watu hawa yaliwafanya baadhi ya wageni kutoa machozi na kuuliza ikiwa kuna serikali katika eneo hilo.

Mkuu wa wilaya ya Geita anadaiwa kukaa sana wilayani humo. Hata baadhi ya wakuu wa mikoa waliowahi kukaa mkoa wa Mwanza wanashangaa kwa nini mtu huyu ameachwa na kuota mizizi katika wilaya hii.

Fikra kwamba anatumiwa na wakubwa zinaibuka haraka, na sasa hata fikra za kutumiwa na wawekezaji zimezagaa mji mzima wa Geita. Utendaji wa serikali hauendeshwi na fikra za barabarani, lakini mtendaji wa serikali asiyeshtushwa na hali ya mateso ya watu wake, anasababisha yeye mwenyewe kufikiriwa na watu wa barabarani kuwa anawatumikia wawekezaji.

Wakimbizi hao walisimulia kwa kirefu historia ya kuwa kwao pale, na kuwa hata mkuu wa wilaya hataki hata kuwasikiliza kwa sababu ni yeye aliyegoma kutekeleza amri ya mahakama ya rufaa iliyowapa haki ya kukaa katika ardhi yao mpaka hapo kesi ya msingi itakapomalizika kusikilizwa.

Taarifa hiyo iliwashtua sana wageni na viongozi wa dini waliotaka kujua ikiwa wakuu wa wilaya wana mamlaka kuliko mahakama ya rufaa! Jibu lilipatikana kuwa wawekezaji ndio wana nguvu kuliko mahakama, na mkuu wa wilaya ni mtumishi wa wawekezaji wenye nguvu nyingi.

Hali hii pia ilidhihirishwa na mkimbizi mmoja mwanaume aliyesimama mbele ya wageni na kuomba kuwa mkimbizi katika nchi zao ili iwe rahisi kupata matibabu kwa sababu amekuwa anaumwa muda mrefu na akienda hospitali hapati huduma yoyote.

Inakatisha tamaa sana kuona raia wa nchi wanakuwa wakimbizi katika nchi yao na viongozi wa serikali wanageuka watumishi wa wageni. Hali iliyo huko Geita na Tarime inakatisha tamaa sana na kuzua fikra za ikiwa kweli tunahitaji uwekezaji huu.

Muda si mrefu, maofisa wa serikali na hata wa vyombo vya dola, wataanza hata kutoa siri za nchi kwa wawekezaji, na hatimaye kuhujumu usalama wa nchi yetu. Hatukujua kama tunawekeza hata usalama na roho za wananchi wetu.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)