Hii ndiyo njia ya kupita Rais wangu Kikwete
HASIRA, kama ilivyo matusi, ni sawa na ugomvi. Hivyohivyo, ugomvi ni kama vita. Vitu hivyo haviwezi kujenga, bali vinabomoa. Sijawahi kuona au kusikia vita ikajenga. Nilichoweza kushuhudia ni uharibifu.
Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kwa wafanyakazi mwezi uliopita, imeleta uharibifu mkubwa. Hata hivyo, tukiyazingatia kwa makini yaliyotokea, tutaweza kupata mwelekeo mpya wa kutatua matatizo yetu bila kuleta uharibifu.
Kuna habari kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Godon Brown, alipoelezwa na mtu mmoja tu kuwa hatampa kura yake, alienda kumuomba radhi. Kura moja katika nchi inayoendesha uchaguzi wake kwa uhuru na haki ni kubwa.
Sijui mtu kama Godon Brown angeambiwa na watu 450, 000 kuwa hawatampa kura hali yake ingekuwaje.
Lakini rais Kikwete amezikataa mwenyewe kura zaidi ya milioni moja na bado ana matumaini makubwa ya kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Sielewi maana yake hasa lakini mtumishi wa Mungu mmoja, aliniandikia kwa kusema, “Nakusalimu. Kura moja ni tishio kama demokrasia haijafa. Olimpiki wanashinda kwa nusu dakika.”
Haki isipokuwapo mtu anaweza kushinda bila kura, ingawa zimepigwa. Mwingine akaandika, “…Rais wako amekataa kura zetu. Basi huenda anajua atakachofanya ili aendelee kutawala.”
Nchi hii ni yetu wote. Amani ya nchi ni amani ya wote walionacho na wasio nacho. Kama kuna mahali viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) wanastahili pongezi, basi ni pale walipoamua kufuta mgomo.
Hata Kikwete anaweza kuwa ametambua kuwa alikosea. Je, tufanye nini ili twende mbele. Tusiseme kuwa rais kamwaga ugali, wacha nasi tumwage mboga. Madhara ya njaa yatatusibu wote.
Hasira ni sehemu ya mapungufu aliyoumbwa nayo mwanadamu. Wengine wakikasirishwa na wake zao, au waume zao huishia kuwachapa watoto wao.
Kama rais aliona viongozi wa Tucta ndio wanaowapotosha wafanyakazi, basi angekataa kura za viongozi hao tu, siyo za wafanyakazi wote.
Rais hajagombana na wafanyakazi wote. Amegombana na Nicolas Mgaya, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA.
Hata wafanyakazi hawajawahi kukorofishana na rais wao moja kwa moja. Hivyo uamuzi wa rais wa kukataa kura zote za wafanyakazi, wauchukulie kwa busara zaidi.
Wamuone kama mzazi mwenye hasira aliyecharaza watoto wake viboko baada ya kukasirishwa na mzazi mwenziwe.
Ni muhimu wakatambua kuwa rais ni babu nao ni wajukuu. Anawapenda na kuwathamini, bali kutumia wasaidizi wake wabaya shetani alimpitia.
Ndiyo hao waliomchomekea hadi barua za uongo ili aonekane mbaya mbele ya watu wake. Kwa hili, wabaya hawa wamefanikiwa.
Naye, tayari amekwishalitambua hili na kuwatambua wafitini wake. Ni wale wanaotumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja – Kikwete na wale wanaowatuma.
Yatupasa kuelewa kuwa wakati mwingine baba aweza asiombe radhi kwa watoto wake. Anachoweza kufanya ni kwenda dukani kuwanunulia nguo mpya, wakati ambao si wa sikukuu.
Wale wakubwa hutambua baba yao ameomba msamaha. Binafsi, siandiki kumsemea rais wangu, maana hiyo siyo kazi yangu. Ninachokifanya mimi ni kumuonyesha njia nyingine isiyo na miiba ya kuwafikia wananchi.
Rais wangu Kikwete, wanachodai wafanyakazi ni malipo ya haki kwa kazi wafanyayo. Wanalalamikia makato na wanatuhumu utawala wako kupunja mafao yao wakati wa kustaafu.
Wanadai haki yao. Haki inapominywa au kudhulumiwa hudaiwa. Haki haiombwi. Wanaodai haki hii ni tabaka la kati na lile la chini. Si wateule wako, maana wao wengi hunufaika na mfumo wa sasa wa mishahara na marupurupu.
Jingine ambalo umelisahau ni kuwa wewe ndiye mwajiriwa Na. 1, lakini hujatangaza kushiriki katika mgomo.
Mawaziri, wakurugenzi na makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge hadi makamishina katika wizara, wote ni waajiriwa wenzako.
Lakini kama ulivyo wewe, nao hawajashiriki katika mgomo. Wengine hata wanawatishia watakaogoma. Mishahara na marupurupu yao ni minono. Wanaoteseka ni waajiriwa wa tabaka la kati na lile la chini.
Sasa nimeamini maneno ya wahenga, “Ashibaye hamjui mwenye njaa.” Hawa ni tabaka la juu la waajiriwa. Ni hawa waliopanua pengo kati yao na wafanyakazi wa chini.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alionya mapema kuwa hali hii itakapofikiwa mlipuko ni lazima. Tayari tumefika hapo.
Watu watafukuliwa kutoka katika mahekalu yao na kushushwa kutoka katika mashangingi ya umma na wale waliodhulumiwa.
Hawa hawataki unono, wanataka mishahara yao ikidhi angalau mahitaji yao ya lazima. Kwa kuwa wanachodai ni haki yao, na kwa kuwa ni wahitaji, sioni sababu ya serikali kuendelea kuwakatalia stahiki zao.
Angalia askari polisi mwenye cheo cha chini ambaye wakati mwingine maisha yake hutolewa anapopambana na majambazi, anavyolipwa ujira kiduchu wa Sh. 150,000 kwa mwezi, lakini akiwa anafanya kazi ngumu.
Lakini mbunge anayefanya kazi kwenye viyoyozi, hulipwa posho mbilimbili na mshahara mnono wa Sh. 7.6 milioni kwa mwezi.
Haya usipoyazingatia na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu, amani uliyoirithi kutoka kwa watangulizi wako, itabaki kuwa historia.
Unahitaji busara kutenda na kutambua kuwa mwalimu anayezalisha mawaziri, wabunge na rais; anayetenda kazi katika mazingira magumu, analipwa mshahara usiotosha hata matumizi ya nusu mwezi.
Sifahamu kosa lake ni nini. Sijui ana mkosi gani. Maana hata akiwa Profesa lakini, kwa kuwa ni mwalimu mafao yake ya uzeeni ni utata mtupu!
Mbunge hata kama vyeti vyake ni vya kughushi, kiinua mgongo chake cha miaka mitano tu, kinatosha kuishi hadi mwisho wa maisha yake.
Posho ya siku moja ya mbunge inapita mshahara wa mwezi mzima wa mfanyakazi wa ngazi ya chini. Hiyo ni nje ya kinachoitwa leo “mfuko wa jimbo.”
Hata hivyo, wakati haya yanafanyika, Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, na wenzake wanaendelea kukukandamiza kwa kutetea ufisadi huu.
Siamini kama anayafanya haya kwa maslahi yako na chama chako. Bila shaka anafanya haya kwa maslahi yake binafsi.
Angalia mbunge wa Karatu, Dk. Willibord Slaa anavyokupenda, hata kama yeye anatoka upande wa pili. Anapinga wabunge kulimbikiziwa mamilioni ya shilingi, wakati huu wa taifa linapoyumba kiuchumi huku wananchi wakishindwa kumudu mlo wao wa siku moja.