Hila za mafisadi kutumia kifo cha Wangwe zimeshindwa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version
Marehemu Chacha Zakayo Wangwe

WIKI iliyopita, Watanzania hususani wananchi wa jimbo la Tarime na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walipatwa na msiba wa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, ambaye alifarikia katika ajali ya gari iliyotokea eneo la kijiji cha Pandambili, Kibaigwa wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma.

Kwa hali zote ulikuwa ni msiba mkubwa wenye sura ya kitaifa. Ni jambo la bahati mbaya kwamba kambi ya upinzani imepata pigo kubwa hasa ikizingatiwa idadi ndogo ya wabunge wao katika Bunge lililofunikwa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi-CCM, kutokana na kuwa idadi kubwa ya wabunge.

Kwa kuwa ajali haina kinga na kwa kuwa kila mmoja ataonja mauti, binafsi naamini Wangwe amefariki dunia katika ajali mbaya, na kwa kweli ilikuwa ni ajali.

Yawezekana tukajadili kama ingewezekana ajali hiyo kuzuiwa isitokee au la, lakini kwa sasa mjadala huo ni jambo lisilokuwa na manufaa yoyote ya maana kwa yote yaliyotokea.

Hata hivyo, msiba wa Wangwe umetufundisha na kutufungua macho kiasi cha sasa kutambua kwamba siasa zetu zimeingiliwa.

Ni jambo la hatari kubwa kwamba wakati Watanzania wakiomboleza kifo cha Wangwe, wapo wanasiasa wengine bila aibu si tu walithubutu kuwaza uovu juu ya msiba wa Wangwe, ila walichukua hatua kutengeneza zengwe kwa nia ya kujinufaisha na kifo hicho.

Ni jambo la hatari sana katika siasa za taifa hili kwamba kundi la watu wanaoandamwa na tuhuma kubwa za ufisadi sasa wanatafuta kila upenyo kujiondoa katika dhambi waliyotenda. Wanatafuta kila upenyo kuchomeka mambo yao ili kusalia salama. Ndivyo msiba wa Wangwe ulivyotumika.

Baada ya kifo cha Wangwe watu hawa wasio na hata chembe ya soni katika nyuso zao, waliamua kupanga, wakaelekeza ulaghai wao ili ionekane kwamba kifo cha Wangwe kilipangwa na viongozi wa CHADEMA.

Eti kwa kuwa wakati wa uhai wake Wangwe alikuwa ametofautiana na viongozi wenzake na kufikia hatua ya kusimamishwa uongozi kama Makamu Mwenyekiti wa chama hicho; uamuzi ambao yeye hakuuafiki, basi kwa hali hiyo wakazusha viongozi hao walikuwa wanamuwinda ili wammnalize.

Kwa mafisadi eti ajali iliyomuua Wangwe Dodoma ni matokeo ya mpango wa viongozi wa CHADEMA.

Ulaghai huo ukahamasishwa Tarime, watu wakapangwa, wakasafirishwa kwa magari ili kwenda kujenga picha hiyo Tarime.

Waandishi wa habari uchwara, wenye upeo mdogo na wasioheshimu dhima ya kazi hii inayohitaji utendaji adilifu na adhimu, wakakubali kuandika waliyoaandika kulipa fadhila za bahasha walizopewa.

Wakakubali kutumika kuusadikisha umma kwamba sasa nguvu ya uasi wa umma imeibuka dhidi ya CHADEMA, dhidi ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, dhidi ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, dhidi ya chama kizima. Aibu!

Waandishi wakakubali kugeuka kuwa Yuda Iskariyote, yule aliyepokea vipande thelathini vya fedha kutoka kwa Wayahudi ili kumsaliti Yesu, wakapokea wakapanga habari wakapeleka kwenye vyumba vya habari, wahariri wenye haraka zao, wasiotaka kukaa kuwaza na kuwazua, wakabeba habari hizo nzima nzima, wakazipachika kwenye magazeti yao, lakini nguvu ya Mungu ilivyo kubwa, umma ukataa kuwasadiki.

Ukajua kuna mkono wa mtu, ukajiuliza na kudadisi vipi habari ya kifo inataka kugeuzwa kuwa kaburi la CHADEMA na viongozi wake, nani anafanya hivyo na kwa faida ya nani?

Ndiyo maana leo hii tunapata hoja ya kusema kwamba mafisadi wamejikuta wakishindwa tena katika mpango wao huu haramu wa kuua hoja ya ufisadi.

Waliamini kwamba sasa CHADEMA ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwalipua na kuwaanika hadharani kitaingia kwenye mgogoro wa ndani, chama kifikie mwisho.

Mafisadi waliamini kwamba sasa mabomu ya mbunge wa Karatu, Dk Wibroad Slaa na wenzake hayatafyatuliwa tena.

Waliamini mgogoro waliokaa mezani na kuupanga na kutumbukiza kwenye vyombo vya habari, utakuwa kama ule ulikumba NCCR- Mageuzi baada ya mwaka 1997.

Mungu akasimama upande wa CHADEMA. Haki ikajiinua juu ya dhuluma na uovu, ukweli ukajulikana kwamba kifo cha Wangwe hakiwezi kuwa mwisho wa CHADEMA na wala njama za mafisadi kugeuza ajenda.

Kilio na mapambano ya wananchi dhidi ya ufisadi yanaendelea, umma unataka kujua mwisho wa kila tuhuma inayokabilia wakubwa.

Wanataka kujua hatima ya EPA na Sh bilioni 133 zilizoibwa, wanataka kujua mwisho wa Richmond/Dowans; wanataka kujua mwisho wa mikataba ya madini, ya TICTS na yote inayofanana na hiyo.

Katika kutafakari kifo cha Wangwe ukweli mmoja unajidhihirisha kwamba mafisadi hawalali, wapo wanasaka mwarobaini wa kuzuia vita hii ambayo kila siku zinavyokwenda ndivyo hasira ya umma inavyozidi kukolea.

Kila mtu mwenye kuitakia nchi hii mema, anajiunga na vita hii, hata kama hasemi lolote, kukasirika moyoni au kusonya tu kwatosha kabisa kuongeza nguvu ya vita.

Umma sasa unatambua kwamba zile zama za kusifia wezi na kuwatukuza zimepitwa na wakati, kwamba hata kama fedha kiasi gani ikitumika kujaribu kugeuza uongo uwe ukweli hakuna manufaa yoyote mafisadi watapata.

Vita itaendea kukolea na kuongeza wigo, na mwishowe umma utashinda.

Jaribio lililoshindwa la kutumia kifo cha Wangwe ili kujiponya dhidi ya hasira ya umma; jaribio la kutaka kukimaliza kabisa CHADEMA; jaribio la kuzima sauti za kijasiri za akina Kabwe, Slaa, Mbowe na wengineo ndani ya chama hicho kidogo lakini makini, hakika ni ushindi mwingine dhidi ya ufisadi.

Vitaa hii ni takatifu Mungu yu upande wa umma hakika mafisadi hawatashinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: