Na hili Rais Kikwete ashindwe mwenyewe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KWA muda mrefu sasa serikali imekuwa ikifunika au ikifanya kazi ya ziada kuwasafisha vigogo mbalimbali wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Mwaka 1998 Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilikumbwa na kashfa baada ya watendaji kuwapa bahasha zenye fedha, waandishi wa habari ili waandike mambo mazuri tu kuhusiana na makadirio ya bajeti ya wizara hiyo.

Kamati iliyoundwa kuchunguza madai hayo ilifanya kazi ya kusafisha wahusika na waandishi wakadaiwa wazushi.

Mwaka 2006 iliibuka kashfa nzito inayoisumbua serikali hadi sasa. Viongozi waandamizi wa serikali walihusika kuipa kwa upendeleo zabuni ya kufua umeme, kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na uwezo wa kifedha wala uzoefu.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ilipotakiwa kuchunguza tukio hilo, ilifanya kazi ya kusafisha. Lakini Kamati Teule ya Bunge ilifichua uozo wote na ripoti yake ilisababisha serikali ya awamu ya nne kuanguka Februari 7, 2008.

Kitu cha kushangaza serikali ilipotakiwa kuwachukulia hatua za kinidhamu wote waliohusika katika kashfa ile, ama iliwaacha wastaafu utumishi wa umma au ilifanya kazi ya kuwasafisha.

Tabia ya serikali kukingia kifua watuhumiwa wa ufisadi imejitokeza hata katika mikataba ya IPTL, ununuzi wa rada na wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT).

Kwamba pamoja na kuwepo ushahidi wa kutosha na baadhi ya watuhumiwa kushtakiana mahakamani, bado serikali imedai haina ushahidi wa kuwafungulia kesi.

Mwezi huu, vigogo katika Wizara ya Nishati na Madini waliripotiwa kutoa mlungula kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ili waridhie makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/ 2012. Taarifa zilipotolewa, serikali ikafumba macho na masikio.

Tunaamini kwamba kitendo cha kigogo wa wizara hiyo kuandika barua akitaka kila idara na taasisi iliyo chini ya wizara hiyo kuchangia Sh. 50 milioni na kuweka katika akaunti maalum, ni kielelezo cha kukithiri kwa ufisadi serikalini.

Tunaishauri serikali ichukue hatua za makusudi kabisa kufanya uchunguzi wa kina na wahusika wote, siyo tu kwamba wachukuliwe hatua za kinidhamu, bali pia wafikishwe kortini.

Barua ya kigogo huyo itaelekeza idara na taasisi zote zilizohusika kutoa fedha na wahusika. Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete atumie fursa hii kuisafisha serikali yake ambayo inalalamikiwa kwa ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: