Hoja ya mbunge Nyalandu bomu


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Imejaa chembechembe za udikiteta
Lazaro Samuel Nyalandu

HOJA binafsi ambayo mbunge Lazaro Samuel Nyalandu anataka kuwasilisha bungeni kuziba mijadala inayohusu imani na madhehebu – dini, haina maana.

Nyalandu aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, kuwa ataomba bunge kupitisha azimio la kutoruhusu mijadala juu ya masuala ya imani na dini ndani ya bunge.

Alisema kuruhusu mijadala hiyo “ni hatari kwa amani ya nchi yetu, na ni uvunjaji wa masharti na misingi ya Katiba ya nchi yetu ambayo serikali yake haina dini.”

Bunge ni baraza la wawakilishi. Wawakilishi wana maoni na imani zao. Lakini wawakilishji wanafanya kazi ya waliowachagua ambao pia wana maoni na imani zao.

Imani na hata dini ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu; tena maisha ya kila siku. Huwezi kutenganisha maisha ya watu na imani zao. Hata katika uwakilishi, huwezi kusema umeingia bungeni kuwakilisha wasiokuwa na imani. Hawapo.

Imani na hata dini ndivyo vinaumba fikra, tabia na hata sura za watu tunaokutana nao. Mfinyango wa sura na tabia ni sehemu ya matokeo ya utu wa mtu; kwa kuyaangalia waweza kujua aina ya mtu unayeongea naye na matakwa yake.

Matakwa ya watu, ambayo yanatokana na utashi wao unaojidhihirisha katika imani zao na matendo yao ya kila siku, ni moja ya mambo ambayo mwakilishi, mbunge anapaswa kujadili.

Katika misingi hii utakataa vipi kuwa na mjadala juu ya watu binafsi, matendo yao, imani zao na mwenendo wa madhehebu yao?

Mbunge Nyalandu anasema anataka kulikumbusha bunge kujadili “masuala yenye maslahi kwa taifa na yasiyokinzana na Katiba ya nchi.”

Kwa maana hiyo anasema, mambo ambayo yanaumba utu wa mtu, yakiwemo imani yake, siyo ya maslahi kwa taifa! Hapa, amechemsha.

Kwamba katiba inatamka kuwa serikali haina dini, haina maana kwamba chombo cha uwakilishi cha wananchi kisijadili mambo yanayowahusu wananchi na imani zao.

Aidha, haina maana kuwa serikali isisikilize watu na imani zao, maoni yao na utashi wao, hata kama wahusika ni wachache.

Kwamba katiba inasema serikali haina dini, ni maelekezo rasmi kwamba serikali isikilize kila mmoja, katika imani yake na imtendee bila upendeleo na bila kujali kama anatoka madhehebu haya au yale.

Kwa serikali kutokuwa na dini, maana yake ni kwamba serikali ina dini zote; inatawala watu wenye imani mbalimbali na ichukue kila hatua kuheshimu na kulinda imani za watu wake. Ni jukumu ambalo haipaswi kulikimbia.

Labda mbunge anachanganya mambo mawili: Kujadili na kuidhinisha. Hata mifano anayotoa ya Mahakama ya Kadhi na kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC) hayapaswi kukimbiwa na serikali wala bunge.

Kinachohitajika hapa ni serikali kusikiliza mwananchi au wananchi wanasema nini; asasi zao zinataka nini. Kama kuna kitu ambacho serikali haiwezi kuamua bila kupitisha kwenye bunge, basi kipelekwe bungeni.

Katika nafasi yake ya ushauri, ni bunge lenye uwezo wa kuipa mawazo serikali juu ya kuheshimu na kushughulikia asasi za kidini na wenye imani katika madhehebu yao mbalimbali.

Tunasema hiyo ni kazi ya bunge kwa kuwa wabunge wako karibu na wananchi wenye imani tofauti na katika madhehebu na asasi tofauti.

Na kazi hii ya ushauri juu ya suala la imani na asasi za kidini, siyo la mara moja katika maisha ya taifa. Ni la kudumu na la kushughulikiwa kadri fikra mpya zinapojitokeza.

Kwa hiyo, hoja ya kutafuta azimio la kuzima mijadala ya dini au juu ya imani na dini, ni hoja iliyojaa woga. Lakini kwanza ni hoja ya kishetani.

Hii ni hoja inayolenga kufunga ndimi za wabunge. Vilevile inalenga kufunga fikra za watu wa imani mbalimbali juu ya mambo yanayowahusu; kwani wabunge wanatoka kwa wananchi.

Visingizio vya hoja za aina hii ni kwamba watoa hoja huwa wanakimbilia kudai kuwa wenye maoni tofauti wanatumiwa na “maadui wa nchi” – wale maadui wa kufikirika.

Ni hoja dhaifu kwani inaonyesha kuwa wananchi hawana uwezo wa kufikiri mpaka watu wa nje wafikiri na wao waige tu kama kasuku. Ni hoja inayokimbia wajibu kwa visingizio vya “kuepuka hatari ya amani kuvunjika.”

Hadi hapa, hoja ya mbunge inafutika. Kipi kinaweza kuleta au kuwa hatari: Kuziba fikra za watu na midomo au kuwaacha wakazungumza ili ijulikane wanataka nini?

Kipi kinaweza kuleta hatari: Kusikiliza wenye imani zao wanataka nini na kuwajibu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu; au kukandamiza mawazo yao kwa kuwanyima fursa ya kusikika?

Kipi ni hatari: Kuzima mijadala na kujidanganya kuwa “yameisha,” wakati ndani ya mioyo ya wengi kumejaa mikakati mikubwa ya njama za maasi dhidi ya udikiteta; au kuruhusu kauli zitoke na kutafutiwa ufumbuzi wa wakati uliopo?

Kadri siku zinavyokwenda na miaka inavyopita, suala ambalo halikutatuliwa linaota usugu na kujenga chuki.

Sasa kipi kitaleta hatari: Kutoa uamuzi wa mazingira ya sasa na labda ya baadaye au kuacha chuki ikamea, kukomaa na kuwa na wajukuu wa migogoro?

Kwa nini bunge, kwa mfano, lijishawishi au lishawishi serikali, kuacha suala la OIC na mahakama ya kadhi bila kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi leo hii? Haya yatajadiliwa lini? Kiporo hiki anaachiwa nani?

Mbunge kijana, Nyalandu anahitaji msaada. Anachotaka kifanywe na bunge ni kukimbia wajibu na kupanda mbegu ya udikiteta katika asasi ambayo moja ya kazi zake kuu ni kuhakikisha unakuwepo uhuru wa maoni kwa kila raia.

Lakini haiingii akilini kuona mbunge anataka afungwe mdomo juu ya suala hili au lile. Inawezekana ameamua kuwa chombo cha kupitishia hoja ya baadhi ya viongozi serikalini wanaotaka kukimbia wajibu.

Kwa hoja mbili ambazo mbunge amelenga – Mahakama ya Kadhi na OIC, serikali ina uwezo wa kutoa maamuzi.

Hoja ya Nyalandu inataka kuzima fikra za wananchi. Inataka kuwanyang’anya wabunge uhuru wa kujadili na kushauri serikali, wakati wowote suala la imani za wananchi linapojitokeza.

Sitashangaa kusikia mbunge huyu anaunga mkono kibano cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wabunge wanaojadili ufisadi kwa sauti kubwa na nguvu zote.

Hoja ya Nyalandu ife. Ni bomu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: