Hoja ya Mwanakijiji ina mapungufu

MAKALA ya mwandishi M.M. Mwanakijiji, iliyozungumzia uongozi wa miaka mitano wa waziri wa katiba na sheria, Mathias Chikawe, imejaa mapungufu mengi.
Ni kweli kwamba hoja nyingi kuhusu wanasiasa hujengwa kwa kutumia mafanikio au matatizo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hii ni sahihi kwani wanasiasa hupimwa kwa kile walichoahidi na kile walichotekeleza.
Kwa hiyo, nilipomsoma kuwa waziri Chikawe ni miongoni mwa wabunge na mawaziri wasiopaswa kurudi bungeni na katika utawala wa serikali ijayo, binafsi nilishangaa sana.
Nilishangaa kwa sababu niliona uchambuzi ulikuwa umeandaliwa na mtu ambaye hafahamu mazingira ya kisiasa nchini au aliyeamua kupotosha ukweli kwa makusudi.
Sina lengo la kufafanua kila neno alilosema Mwanakijiji. Lakini kama mdau wa karibu wa sekta ya sheria nchini naamini kuna mambo ya kuweka sawa kutokana na uchambuzi ule.
Wizara ya Katiba na Sheria ni kitu gani? Kwa lugha nyepesi, huu ndiyo mhimili wa masuala yote ya kisheria katika nchi yetu. Inagusa idara, taasisi na maeneo yote yanayohusiana na sheria na utekelezaji wake.
Kwa uhusiano huu, mtu ambaye hajafanya utafiti kidogo anaweza kudhani yule anayepewa mikoba ya u-waziri wa katiba na sheria basi ndiye kamanda au tuseme mtoa amri kwa taasisi zote zinazohusiana na sheria. Hili si kweli.
Ingawa wizara hii ina uhusiano na taasisi nyingine zinazoshughulikia sheria, utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo hauwezi kusukumwa na mkono wa siasa. Unasukumwa na Katiba na sheria zilizoziunda. Kutosukumwa huku na mkono wa siasa ndiyo kunajenga na kuiimarisha dhana ya utawala wa sheria na ulio bora.
Kwa mfano, kama sheria mama - katiba, Ibara ya 59B inampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote ya jinai nchini, sote tunapaswa kutii hili. Sheria inayosimamia uendeshaji Mashtaka (National Prosecution Service Act, 2007) inafafanua kwa kina maelekezo haya ya katiba.
Labda swali linaloweza kusumbua msomaji ni Waziri wa Katiba na Sheria ana mamlaka gani juu ya taasisi hizo? Je, nani kati ya Waziri na Wakuu wa Taasisi hizo ana mamlaka ya kutoa mwanga kwa kile kinachojulikana kama utawala wa sheria?
Kuna maoni tofauti kuhusu mamlaka ya taasisi nilizozitaja.
Maoni mengine yanakosa utafiti na hivyo kupwaya. Hizi ni hoja zinazojikita katika ubabe wa kisiasa.
Wanaojenga hoja hizi wangependa kuona mkono wa siasa unaelekeza fulani atuhumiwe, achunguzwe, akamatwe, ashitakiwe na ahukumiwe. Akili ya kawaida inayoamini katika kile tunachoita “utawala wa sheria” haiwezi kukubaliana na hili.
Hivyo aliyepewa wadhifa huu wa waziri wa Katiba na Sheria anaposema kuna vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi; vyenye mamlaka ya kuanzisha na kuendesha mashtaka na vile vyenye mamlaka ya kutoa kuhukumu, anakuwa anatetea kile kinachoitwa utawala wa sheria.
Kuna hoja nyingine katika uchambuzi wa Mwanakijiji ambayo nayo inapwaya. Hili la taarifa kuwa waziri mkuu mstaafu atashtakiwa, lilishatolewa ufafanuzi. Hii ilikuwa Agosti mwaka juzi Chikawe alipolifafanua katika mkutano na wanahabari pale jengo la Haki, mtaa wa Luthuli Dar es Salaam.
Waziri Chikawe alisema kuwa taarifa zinazomhusu yeye kuzungumzia Jaji Warioba zilizoandikwa kuwa yeye (Chikawe) amesema Serikali ina mpango wa kumshitaki Warioba, si za kweli na zimejaa ushabiki.
Alisema yeye kama waziri wa Katiba na Sheria hana mamlaka ya kumchunguza mtu na kwamba mamlaka hayo yapo kwa vyombo husika ambavyo vimepewa mamlaka na Katiba na sheria.
Kwa maoni yake, vyombo hivi kama TAKUKURU au polisi ndivyo vinavyopaswa kuulizwa kuhusu suala la Jaji Warioba. Alifafanua zaidi kuwa mwenye mamlaka ya kuanzisha, kuendesha na kusimamia mashtaka yote ya jinai nchini ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Kwa hiyo, kujenga hoja (ya kuhusisha waziri kutenda au kutotenda), bila kuzingatia ufafanuzi kama huu uliotolewa kwa uwazi katika mkutano na wanahabari, ni jambo lisiloingia akilini.
Katika uchambuzi ule kuna hoja nyingine. Kwamba Chikawe ameshindwa kuishauri serikali kufuata maelezo ya Katiba katika suala la mgombea binafsi.
Turejee Katiba yetu ibara ya 59 (3). Ipo wazi kabisa na inasema kutakuwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali katika mambo yote yanayohusu sheria. Hivi ndivyo Katiba inavyosema. Nani mwingine wa kuipinga?
Chikawe alifafanua mara kadhaa kwa nini Serikali imewasilisha rufaa yake Mahakama ya Rufani kuiomba itamke kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutamka au kufuta kipengele cha Katiba. Hili ndilo limepotoshwa sana kuwa Serikali inapinga mgombea binafsi.
Hoja hapa sio mgombea binafsi. Hoja ya Serikali hapa ni wapi Mahakama Kuu ilipata mamlaka ya kutamka au kufuta kipingele cha Katiba kupitia sheria inayosimamia haki za msingi na wajibu (Basic Rights and Duties Enforcement Act).
Hoja hii ya Chikawe inamfanya kuwa mlinzi na mshauri mzuri wa Katiba na si kinyume chake. Tupaswa kujiuliza, itakuwaje iwapo Mahakama Kuu kesho itaamua kufuta kipengele kingine chochote cha Katiba, tuseme kile cha 2(b) katika ibara ya 67 kinachomkataza mgonjwa wa akili kugombea ubunge.
Nimalizie kwa kusema kuwa kupwaya kwa hoja katika mjadala wowote ni jambo la kawaida pale ambapo mtoa hoja anakuwa hajafanya utafiti wa kina kuhusu mada husika.
Hili tumelishuhudia katika mijadala ya Bunge, maofisini au hata katika vijiwe mbalimbali. Mada inaweza kuwa na kichwa murua, aya ya kwanza murua lakini aya thelathini zinazofuata zikakosa mantiki. Ukiona hivyo, unatulia, unafanya utafiti na kujenga hoja upya.
Ni matumaini yangu kuwa mchango wangu kuhusu hoja ya Mwanakijiji katika gazeti hili unaendeleza kazi nzuri ya vyombo vya habari ya kuelimisha na kuamsha mijadala ambayo kwa kweli inajemga demokrasia.