Hoja ya Rais kushindwa kazi

- Serikali Kilosa ilivyopora wafugaji
NINACHANGIA mjadala ulioibuliwa na Profesa Ibrahim Lipumba, aliyesema Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kazi; ukweli unaowakera wapambe wa Kikwete.
Wawili miongoni mwa wakereketwa hao ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu na mbunge wa zamani wa Temeke, John Kibasso ambao waliandika kumtetea Kikwete.
Reyemamu na Kibasso wanamsifu Kikwete kuwa shujaa aliyefanikiwa kujenga shule katika kila kata. Shule hizi za sekondari za serikali za kata hazistahili hata kuiitwa shule.
Si Mwanahawa Kikwete alihitimu Darasa la Saba mwaka 2007 katika shule ya Trust Saint Patrick, Sakina, Arusha, badala ya shule zilizopo Bagamoyo? Si Esupat Lowassa anasoma Darasa la Nne C katika shule hiyohiyo badala ya “pango” mojawapo Monduli?
Tutazame ukatili dhidi ya wafugaji wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Akihutubia Bunge jipya 30 Desemba 2005 Rais Kikwete alisema, "Mheshimiwa Spika, tutachukua hatua za dhati kuboresha ufugaji wetu. Hatuna budi tutoke kwenye uchungaji wa kuhamahama na kugeuza nchi nzima malisho; sasa tuwe wafugaji wa kisasa."
Kikwete aliubeza ufugaji wa asili, "Ng’ombe hanenepi, mfugaji hanenepi." Hawa ng'ombe wasionenepa hawana kichaa, wanavumilia ukame, magonjwa na kutelekezwa na serikali. Na pia ni watamu. Lakini pili, wafugaji wanenepe ili iweje?
Kuna uhasama wa kihistoria Kilosa kati ya Wamasai na Wakaguru. Karibu na uchaguzi wa 1958, Zuberi Mtemvu, Mkaguru wa Kilosa, alijitoa TANU na kuanzisha chama cha Tanganyika African National Congress (ANC). Hata hivyo TANU iliishinda ANC.
John Shibuda, Mbunge wa Maswa, anasema TANU iliahidi kuheshimu haki za wafugaji. Hivyo Wamasai wengi waliiunga mkono TANU; jambo lililowaudhi Wakaguru. Uhasama huu unaendelea hadi leo hii.
Mwaka 2000 watu zaidi ya 40 waliuawa katika mapigano kati ya Wamasai na Wakaguru pale Rujewa, Kilosa. Rais Kikwete akasema wafugaji wadhibitiwe.
Kilichofuatia? Tarehe 27 Oktoba 2008 mkulima alimpiga risasi na kumuua mfugaji. Siku hiyohiyo wafugaji walilipiza kisasi kwa kuwaua wakulima saba. Polisi waliingilia kati. Wafugaji wakayakimbia makazi yao.
UJAKI, sungusungu Wakaguru wa zama za Mtemvu, wakapora ng'ombe 1,599, mbuzi 886, kondoo 73 na magunia 60 ya mahindi na kuteketeza nyumba 70 za wafugaji kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mabwegere.
Mkuu wa Wilaya Kilosa wakati huo, Athumani Mdoe, alitoa tangazo lisilo na tarehe akiwaamuru wafugaji waondoke Kilosa. Tarehe 18 Novemba 2008 Mkurugenzi wa Wilaya Kilosa wakati huo, Ephraim Kalimalwendo, naye aliwaamuru wafugaji waondoke Kilosa ndani ya siku saba.
Tarehe 7 Desemba 2008 Rais Kikwete alihutubia viongozi wa Mkoa wa Morogoro pale Morogoro Hotel. Alikaririwa akisisitiza kuwa wafugaji "waondolewe…watafute sehemu nyingine…"
Wakati huo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Meja Jenerali Msataafu Said Kalembo alinukuliwa akisema wafugaji lazima wahamishwe kwani ni “waharibifu wa mazingira …”
Baraza la Madiwani Kilosa, 18 Desemba 2008 liliazimia kuwafukuza wafugaji kwa madai kuwa ni “haramu Morogoro.” Madiwani wote Kilosa ni watoto wa wakulima.
Hato ndipo ulipoanza ukatili usiomithilika. Uporaji mifugo ulianza rasmi 29 Januari 2009. Viongozi wa Wilaya Kilosa, akiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, OCD, Maofisa Watendaji wa kata na vijiji wakitumia polisi wenye silaha kali na wanamgambo, walitumia mabavu kuwafilisi wafugaji.
Wafugaji walitozwa kile kilichoitwa faini, Sh.30,000 kwa kila ng'ombe waliyekamata na Sh.10,000 kwa kila mbuzi au kondoo. Mfugo ukilala kwenye “mahabusi” ya mifugo kwa usiku mmoja, mfugaji anatozwa Sh.5,000, maarufu kwa jina la “malipo ya gesti.” Waporaji walijenga mahabusi za mifugo pale Kimamba, Kivungu, Dumila na Msowero.
Waporoji waliwandaa wanunuzi wao na kuwauzia mifugo ya wafugaji kwa bei za kutupa. John Shibuda, Mbunge wa Maswa, anasema ng'ombe aliyestahili kuuzwa Sh.400,000 aliuzwa Sh.60,000. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, tayari amethibitisha hilo.
Doto Dofu ni Msukuma mfugaji katika Kijiji cha Mlangali, Kilosa. Alilazimishwa kulipa waporaji walichoita faini Sh.390,000 na kupewa stakabadhi Na. 0426653 31 Januari 2009.
Siku tatu baadaye Dofu alitozwa tena Sh.6,660,000 na Sh.4,250,000 na kupewa stakabadhi Na. 0426676 na 0426677. Waporaji waliponogewa na fedha, walikamata ng'ombe wake 1,500 wenye thamani ya Sh. 1,200,000,000. Ndama wachanga 80 wenye thamani ya Sh.8 milioni walikufa.
Dofu aliendelea kuandamwa. Tarehe 4 Februari 2009, alitozwa tena (faini) ya Sh.75 milioni. Lakini safari hii waporaji walimwandikia stakabadhi Na. 0426824 inayoonyesha kuwa alilipa Sh.42,780,000 tu. Kesho yake alitozwa tena Sh.1,000,000 na kupewa stakabadhi Na. 0445602.
Siku sita baadaye alilipa tena Sh.40 milioni na kupewa stakabadhi Na. 0428024 inayoonyesha kuwa alilipa Sh.15,180,000 tu. Nilipokutana naye Dodoma 5 Julai 2009 alisema kuwa alishatumia Sh.6 milioni akihangaika bila mafanikio kutafuta haki yake.
Kochocho Simbokwa ni Mmasai mfugaji katika Kijiji cha Kiduhi. Tarehe 2 Februari 2009 waporaji walipora ng'ombe wake 458, mbuzi 103 na kondoo 97. Siku iliyofuata alitozwa Sh.4,290,000 na Sh.715,000 na kupewa stakabadhi Na. 0426686 na 0426687. Tarehe 4 Februari 2009 alitozwa tena Sh.9,450,000 na kupewa stakabadhi Na. 0427156. Familia yake ina watu 50 wanaomtegemea. Amepokonywa mifugo yote.
Inakadiriwa wafugaji Kilosa wamepata hasara ya zaidi ya ng'ombe 500,000 na mbuzi pamoja na kondoo 300,000 bila kuhesabu punda na wanyama wengine. Hii ni karibu sawa na Sh.200 bilioni, bila kuhesabu vipigo, vitisho na ukatili mwingine.
Wafugaji walichapwa viboko kama watumwa vile. Wengine wakatupwa mahabusi bila chakula. Baadhi wakashitakiwa. Baadhi wakaikimbia Kilosa kwenda kusikojulikana baada ya kufilisiwa.
Job Ndugai, Mbunge wa Kongwa, aliliambia Bunge 3 Julai 2009, "Wamasai ni jasiri. Unaweza kumkata mkono bila ganzi akavumilia. Lakini wazee na morani wanalia machozi kama watoto kutokana na unyama waliofanyiwa Kilosa."
John Cheyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, aligadhabishwa mno na ukatili huu na 5 Februari 2009 alimuuliza Waziri Mkuu: “Serikali inataka wafugaji waende wapi?” Mizengo Pinda alijibu, "Ukiniuliza wafugaji waende wapi, nami nitakuuliza walitoka wapi?"
Kwanza, John Last katika makala yake “A Journey into the Unguru Country from Mamboia,” yaliyochapishwa mwaka 1882, anaandika kuwa kulikuwa na Wamasai Kilosa miaka ya 1800. Hawa ni wenyeji Morogoro kama Pinda alivyomwenyeji Rukwa.
Pili, miaka ya 1970 serikali ilipora ardhi ya Wabarbaig Hanang na kuanzisha kilimo cha ngano kwa msaada kutoka Canada. Maeneo ya malisho yamegeuzwa hifadhi za taifa, ranchi za taifa na mashamba. Hii ndio sababu wafugaji wanateseka.
Katika mazingira haya, yuko wapi Rais Kikwete ambaye Rweyemamu, Kibaso na wengine wanaimba kuwa amefanikiwa. Amefanikiwa vipi wakati wafugaji wanaishi kama wakimbizi katika nchi yao?