Huu Muungano wa kijeshi?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly versionSend to friend

MIAKA 45 ya Muungano. Sherehe nzito. Kubwa. Nene. Wanasema ya kukata na shoka: Viwango vya kale kabla misumeno kutinga. Kabla ya mashine za gilotini katika viwanda vya kisasa.

Bali Uwanja wa Taifa, pale Bandari Salama. Umati wamiminika kuona matunda ya Muungano. Waona bunduki. Waona askari. Waona magwaride. Matunda yako wapi?

Miongo minne na nusu. Ya siasa za mkumbatiano. Ya kanzu moja wawili. Ya ndugu kitanda kimoja. Ya maapizo na kula yamini. Ya majaribio na kutenda. Ya kupanda na kuvuna, lakini si kwa mtindo wa DECI.

Umati waja kuona, ndani ya uwanja mpana. Kuna nini? Walovaa magwanda. Saresare. Saluti kedekede. Huitwa walinzi – Askari wa Jeshi, Polisi na Magereza. Miaka 45? Tuone hao tu? Matunda yako wapi?

Ni umri wa nchi mbili, miaka 45. Ndogo na kubwa bali hakuna kaka wala mdogo. Hadhi sawa. Umri sawa katika kuwekeza. Matumaini manene na mazito na mfumbato wa dira. Mfano pekee Afrika na majigambo nyota za anga.

Kwenye sherehe nendeni, miaka 45. Unaonani? Watoto wa shule. Gwaride lao. Halaiki yao. Nyimbo zao na mashairi. Yako wapi matunda ya Muungano? Labda nje ya uwanja huu.

Hesabu kumikumi mara nne na tano uongeze. Umri wa mtu mzima. Vyuo vyote kumaliza na kazi kukalia. Biashara kunogesha na uhondowe kufyonza. Miaka mingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Fikeni Uwanja wa Taifa. Kunani? Walozaliwa 1964. Walopanda baisikeli – wa Bara na Visiwani. Bendera wapeperusha na nyonga kupindapinda. Ni matunda ya Muungano?

Ni nusu karne kasoro mitano miaka. Wengi wataka kuona matunda ya mfumbato. Watoto wataka kuona dira ya waasisi. Dunia yataka kuona faida ya kuwa pamoja. Unahitajika ufunuo.

Bali nenda Uwanja wa Taifa. Mwaka hadi mwaka. Askari katika magwanda. Magwaride. Tutashangilia kishindo cha wanawake na wanaume wakakamavu. Basi. Yako wapi matunda ya Muungano?

Uzeeni waelekea Muungano wa Tanzania. Watu husema, maisha huanzia 40 miaka. Sasa arobaini kapita na mvi zaanza kutanda. Tunaonyeshani? Viongozi waseme. Mbele ya kadamnasi walete. Hili. Hili. Hili! Ushahidi wa ubora wa mkumbatiano.

Lakini Uwanja wa Taifa nendeni. Ndege za kivita juu zapasua anga. Mbwa wa polisi waonyesha umwamba. Pikipiki zao mia zatanda kwa madoido. Yako wapi mazuri ya Muungano? Kipi kilengwa na kipi mepatikana?

Hapa kuna uchumi. Muungano kaletani? Kuna siasa. Muungano kalindani? Kuna demokrasia. Muungano wateteani? Kuna ubora wa maisha. Muungano kafikapi? Kuna matarajio twendako. Muungano kapangani?

Siku hiyo ikifika, Uwanja wa Taifa kufika. Hakuna ulotaraji. Miaka nenda miaka rudi – ni magwaride na ngoma za asilia. Hivi hakuna kilofanyika, kuendeleza Muungano?

Kuna misukosuko, kumenyana kwa kauli. Kuna kusutanasutana, mithili ya nyani mitini. Kuna kubembelezana kama wachumba mbalamwezini. Kuna kulipukiana kama wasiojuana. Bali kuna kutulizana ili wawili kanzu wavae. Na miaka inateleza.

Bali Uwanja wa Taifa ukienda, maadhimisho kuona. Ni walozaliwa Muungano ulipoanzishwa. Ni marudio: gwaride, halaiki na sarakasi. Hakuna hotuba ya mtawala wala ya mtawaliwa. Wamechoka kusema au hawana la kunena?

Muungano wasogea mipaka ya nusu karne. Maadhimisho yafana kwa mabuti kwenye lami. Vigelegele vyazonga mbwa walofunzwa, wahalifu kutafuta. Ngoma asili zalia: Ndi! Ndi! Ndi. Nkulundindi. Meno yatoka kwa shida watawala kulaghai!

Uwanja wa Taifa kimya! Hakuna ujumbe. Hakuna tafakuri. Hakuna ripoti. Ni kelele za viatu, sauti za askari na washereheshaji. Jukwaa limesheheni mabubu waso na jambo. Si juu ya tulivyo sasa wala huko tuendako. Na miaka inasonga mbele mithili ya mshale wa saa.

Miaka 45 hakuna cha kusema? Hakuna cha kulilia? Hakuna cha kukumbuka? Hakuna cha kutamani na kutaraji? Hakuna cha kuonya wala kusifia? Ni miaka ya kuonyesha misuli ya watawala kama kwamba Muungano walindwa na jeshi?

Usiache Uwanja wa Taifa kwenda. Mwaka hadi mwaka utaona. Mabubu wakaa jukwaani maaskari na wanafunzi uwanjani wajiviringisha. Kimoja waambulia: Makofi. Anayebahatika: Vigelegele. Mwenye ngekewa: kupungiwa mokono.

Muungano wa nani, tuulize kitulivu. Waliungana wakubwa au na wadogo wamo? Taarifa ziko wapi siku ya maadhimisho. Dira mpya iko wapi ili twende kwa faraja? Mafanikio yakoje na changamoto ziko wapi? Mbona twaswagwa kizembe hata swali hatunalo?

Siku inapowadia, Uwanja wa Taifa sogea. Askari jeshi, Polisi na Magereza wa buti ndiyo alama Muungano. Ndege za jeshi angani kunguruma kwa makeke. Wanafunzi na halaiki na ngona za asilia. Huo ndio mwisho wa Muungano?

Rais hukaa kimya, vivyo hivyo ndugu zake kitabaka. Kama hivi majuzi, hata mwenziye Visiwani kutofika. Uwanjani na Ikulu Kikwete katinga kipweke na wadogo wa Visiwani. Kitendawili tegua Karume wapi kaenda. Uwanjani na Ikulu sura yake ipotee. Ni dharura ni uchovu au mikiki ya Muungano? Twabaki kukodoa kama wataparurana.

Nendeni siku ikifika Uwanja wa Taifa muone. Ujumbe ni marufuku na taarifa ni kufuru. Kilicho gwaride la majeshi kama Muungano ni vita. Nukuu na uchambue mwaka hadi mwaka, misuli ndiyo maadhimisho.

Tumeyachoka mabuti na silaha mikononi. Tunazitaka hoja siyo madege angani na mizinga ardhini. Twataka majibu haraka kama matatizo yataisha na mbele tukasonga. Pumzisheni gwaride, hoja mwanana tupate.

Maadhimisho Muungano ni misuli ya kijeshi. Sababu haijatolewa kama Muungano hatarini na ulinzi kustahili. Nani twatishia? Kama ridhaa washindwa na hoja kuu kuhimili; Muungano rejesheni kwa wanaoumiliki – Wananchi.

0
No votes yet