Huu ndio upofu wa Kamati Kuu ya CCM


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

MIONGONI mwa maamuzi ya kuchekesha ambayo yalifanywa na Kamati Kuu (CC) ya chama kilichopo ikulu – Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilipokutana hivi karibuni ni kuitaka serikali kuhakikisha kwamba bei ya mafuta haipandi ovyo kwa kuwa inawapa wananchi ugumu wa maisha.

Pamoja na CC kutoa angalizo hilo, hasa kuhusu bei ya mafuta ya taa, hali ya soko la mafuta nchini imeendelea kuwa tete kuliko maelezo. Takribani wiki moja tu baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) Agosti 2011 kutoa bei mpya elekezi ambazo zilishusha kwa kiasi bei ya nishati hiyo katika soko la ndani, hali imegeuka na makali yameendelea kuuma wananchi kama kawaida.

Kutokana na maamuzi ya Ewura ya kupunguza baadhi ya tozo kwenye mafuta ambazo zilikiwa zinanufaisha taasisi za serikali, kama Ewura yenyewe, Tiper, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Shirika la Viwango (TBS), Mamlaka ya Bandari (TPA), Wakala wa Vipimo na Mamlaka wa Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), nafuu iliyopatikana ilidumu kwa muda wa wiki moja tu!

Jumatatu wiki hii bei zilirejea tena juu. Kisa. Ewura wanasema ni mambo mawili, moja kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, lakini kibaya zaidi kuendelea kudhoofika kwa sarafu ya Tanzania.

Tangu mwaka 2005 sarafu imepoteza thamani yake kwa takribani asilimia 50. Yaani wakati dola moja ya Marekani mwaka 2005 ilikuwa ikibadishwa kwa Sh. 1,000, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kwamba sasa thamani yake imefikia Sh. 1,624 kwa dola moja.

Kwa maneno mengine ni sawa na kusema kwamba uwezo wa wananchi wetu wa kumudu mahitaji yao siku baada ya siku unaporomoka kutokana na kuzidi kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Kwa muda mrefu watu wengi wamekuwa wanajiuliza ni nini hasa kinasababisha sarafu yetu kuyumba kwa kiwango hicho, zipo sababu zinazotolewa na wadau mbalimbali juu ya kuyumba huko; moja ni mahitaji makubwa ya dola ya Marekani kwa ajili ya kuagiza vitu nje ya nchi ambavyo nchini havipatikani. Vitu hivi ni kama mafuta, vipuri vya mitambo na mashine mbalimbali, magari na vipuri vyake, kutaja kwa uchache tu.

Lakini pia kuna sababu inayotolewa kwamba kwa muda mrefu Tanzania imeporomoka kwa kiwango cha uuzaji wa bidhaa nje; hizi hasa ni kama mazao ya biashara kama kahawa, korosho, katani, pamba; lakini pia kuna fedha za kigeni zinazoingia nchini kwa njia ya utalii. Njia zote hizi ni vyanzo vya fedha za kigeni nchini.

Zimetolewa sababu nyingi kuhusu kushuka kwa mauzo nje, lakini hata kupungua kwa mapato ya utalii yakifungamanishwa na msukosuko wa uchumi duniani.

Hata hivyo, kwa kiwango kikubwa si serikali au hata chama tawala ambacho kinaisimamia serikali wamekuwa radhi kueleza bayana kwamba matatizo haya ya kuyumba kwa kasi kwa sarafu ya Tanzania ni matokeo ya kuzorota kwa uzalishaji kunakochangiwa hasa na mgawo wa umeme. Changamoto za umeme kwa muda mrefu zimekuwa ni kikwazo kikubwa cha uzalishaji.

Kwa mfano, wakati kati ya Januari 2005 na Desemba sarafu ya Tanzania dhidi ya dola iliporomoka kwa Sh. 113.57 dhidi ya dola ya Marekani, kiwango cha kuporomoka kwa sasa kinatisha, wa sasa Shilingi kwa wiki moja tu inapoteza thamani yake kwa Sh. 33.86 dhidi ya dola.

Hizi ni bei za BoT na si za kwenye maduka ya kubadili fedha ambazo hata hivyo hali ni mbaya zaidi. Agosti 03, 2011 siku bei mpya elekezi ya Ewura inaanza dola moja ya Marekani ilikuwa inabadilishwa kwa Sh. 1,586.00 lakini ilipofika Agosti 12, 2011, yaani siku tisa baadaye, dola moja ilikuwa inabadilishwa kwa Sh. 1,619.86; hali ilikuwa mbaya zaidi ilipofika Jumatatu wiki hii kwani dola moja ilikuwa ni sawa na Sh. 1624.17.

Haya yote yakitokea, bei ya dhahabu katika soko la dunia inapaa kwa kasi ya ajabu. Kwa mujibu wa takwimu za BoT bei ya onsi/wakia moja ya dhahabu Alhamisi iliyopita yaani Agosti 11 mwaka huu, ilikuwa ikuzwa kwa dola za Marekani 1,813.29. Bei hizi zimevunja rekodi kwa mwaka huu.

Cha kushangaza ni kwamba wakati kwa sasa Tanzania inatajwa kama nchi ya tatu Barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu, baada ya Afrika Kusini na Ghana, dhahabu hii haionyeshi ikisaidia chochote kumarika kwa sarafu yetu.

Maelezo ya uzalishaji wa dhahabu yamethibitisha sawa kabisa na upatikanaji wa gesi asilia nchini. Itakumbukwa kwamba wakati harakati za kujenga bomba la gesi kuja Dar es Salaam ilijengwa dhana kwamba tatizo la umeme ni kama lilikuwa limefikia ukomo.

Kwa mshangao wa wengi, si tu kwamba gesi asilia hajaweza kusaidia taifa hili kuandokana na adha ya mgawo wa umeme, bali pia imethibitisha kwa mara nyingine kuwa wanaonufaika na rasilimali za nchi hii zinazovunwa ni makampuni ya uwekezaji. Gesi ipo Ubungo, Dar es Salaam lakini makali ya mgawo wa umeme ni kama kawaida, tena kwa makali makubwa zaidi.

Ukweli huu unafanana na hali halisi ya uzalishaji wa dhahabu kwani wakati serikali ya awamu ya tatu inavutia wawekezaji wakubwa katika uchimbaji wa madini, husasan dhahabu, waliwajengea wananchi matarajio kwamba mambo yetu kama taifa yangebadilika.

Wananchi walijengwa hadi wakaamini kwamba uchimbaji wa madini hayo ungekuwa na maana kwa uchumi wao. Miaka zaidi ya 10 sasa kila kinachopatikana katika migodi hakionyeshi kusaidia uchumi wa nchi, wala kusaidia kumarika kwa sarafu ya Tanzania.

Ndiyo maana leo hii, taifa lenye gesi asilia, linalochimba madini ya dhahabu kwa kiwango kikubwa hivyo, tena katika kipindi ambacho bei ya dhahabu iko juu mno katika soko la dunia, linashindwa kabisa kuwaeleza wananchi wake ni kwa kiwango gani rasilimali hizi zinazovunwa na makampuni zimesaidia kuimarisha uchumi wake.

Ni kweli mafuta yanapaa bei katika soko la dunia, lakini ni kweli pia kuwa dhahabu nayo inapaa bei katika soko hilo hilo , cha ajabu taifa hili halina maelezo ni kwa nini basi sarafu yetu haipati nafuu kutokana na hali hiyo mbali ya mambo kuzidi kudidimia kila uchao?

Hili ndilo suala ambalo Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kuiliza serikali yake ilipokuwa inatoa maagizo ya kutekelezwa na serikali hiyo ambayo kimsingi mambo yake yanazidi kuwa magumu siku hadi siku.

0
No votes yet